Jul 12, 2022 01:26 UTC
  • Jumanne tarehe 12 Julai 2022

Leo ni Jumanne tarehe 12 Dhulhaji 1443 Hijria sawa na Julai 12 mwaka 2022.

Siku kama ya leo miaka 1311 iliyopita, kwa mara ya kwanza katika historia ya mapambano ya Waislamu, akiwa na jeshi kubwa la Kiislamu Twariq bin Ziyad aliweza kuingia Uhispania. Ushindi huo ulikuwa mwanzo wa maendeleo ya Waislamu barani Ulaya ambapo uliendelea hadi Ufaransa ya sasa. Twariq bin Ziyad aliwasili Uhispania baada ya kuvuka lango bahari kati ya Morocco na Uhispania linalojulikana kwa jina lake mwenyewe yaani "Jabal Tariq." Mlango bahari huo unatumika kama njia ya mawasiliano kati ya Bahari za Atlantic na Mediterranean. Waislamu walitawala kwa karne nane huko Uhispania na kueneza mafunzo na utamaduni wa Kiislamu barani Ulaya baada ya kutekwa Andalusia, moja ya maeneo ya hispania ya leo.

Jabal Tariq

Miaka 789 iliyopita katika siku kama ya leo, bandari ya kihistoria ya Alexandria huko Misri ilizingirwa na meli za kivita za Jeshi la Msalaba. Wakati huo Salahuddin Ayyubi alikuwa gavana wa Alexandria na hakuweko katika mji huo wakati maadui walipofanya mashambulizi. Hata hivyo wapiganaji wa Kiislamu walikabiliana kwa nguvu na Jeshi la Msalaba hadi gavana Salahuddin alipowasili. Wanajeshi wa Uholanzi waliokuwa katika safu ya mbele walipigwa vibaya na kulazimika kurudi nyuma.

 Alexandria

Siku kama ya leo miaka 205 iliyopita, alizaliwa Henry David Thoreau, msomi na mwanaharakati wa Kimarekani. David alikuwa akiheshimu mazingira asilia kama viumbe vya Mwenyezi Mungu na alisifika kwa kuwa na akhlaqi na maadili mema. Henry David alikuwa akisisitiza kuwa, haifai kuangamiza maisha ya wanadamu kwa tamaa ya kufikia mali na fedha nyingi. Aidha mwanaharakati huyo, aliamini kuwa kama vile ambavyo serikali inavyomuadhibu mtu mkosefu, kadhalika inapotokea serikali hiyo ikashindwa kutekeleza wadhifa wake wa kiuongozi, basi wananchi nao wanatakiwa kuipa adabu serikali hiyo sanjari na kuiondoa madarakani. Miongoni mwa athari muhimu za Henry David Thoreau ni pamoja na kitabu cha 'Uasi wa Kiraia' na alifariki dunia mwaka 1862.

Henry David Thoreau

Tarehe 12 Julai miaka 76 iliyopita, Hoteli ya Mfalme Daud huko Baitul Muqaddas iliripuliwa kwa bomu na kundi la Kizayuni la Irgun. Hoteli hiyo ilikuwa ikitumiwa sana na raia wa Palestina. Bomu lililokuwa limetegwa ndani ya hoteli hiyo liliripuka na kuuawa watu zaidi ya 200. Kuweko Wayahudi watano miongoni mwa waliouawa katika mlipuko huo kunabainisha wazi namna Wazayuni wasivyothamini hata maisha ya Wayahudi ili kufikia malengo yao ya kujitanua na kuzusha hofu miongoni mwa Wapalestina.

Hoteli ya Mfalme Daud

Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Ayatullah Mirza Muhammad Baqir Ashtiyani. Alimu huyo ni mjukuu wa Mirza Muhammad Hassan Ashtiyani mmoja wa viongozi wa Harakati ya Tumbaku nchini Iran. Alizaliwa mjini Tehran na baada ya kukamilisha masomo ya awali alielekea katika mji wa Najaf huko Iraq na kuhudhuria masomo ya maulama mashuhuri wa zama hizo kama Ayatullah Mirza Naini na Sayyid Abul Hassan Isfahani. Ayatullah Muhammad Baqir Ashtiyani ameacha athari nyingi za vitabu zenye thamani kubwa katika nyanja mbalimbali.

Ayatullah Mirza Muhammad Baqir Ashtiyani

Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilifanya mashambulizi ya anga na baharini huko Lebanon. Utawala wa Kizayuni ulifanya mashambulizi hayo kwa kisingizio cha kukamatwa mateka wanajeshi wake wawili na wapiganaji wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon kupitia oparesheni yake ya kujilinda. Tel Aviv ilifanya mashambulizi hayo ya kijeshi huko Lebanon ikiungwa mkono na Washington lengo lake kuu likiwa ni kuvunja uwezo wa kijeshi wa Hizbullah na kuipokonya silaha harakati hiyo inayohesabiwa kuwa nguvu kuu ya mapambano huko Lebanon mbele ya jeshi ghasibu la utawala wa Kizayuni.