Jul 14, 2022 08:54 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Karibuni mjiunge nasi katika kipindi hiki cha 16 kinachozungumzia Sibtain, yaani Imam Hassan na Imam Hussein (as) katika Qur'ani na Hadithi.

Ama kwa kweli kuna swali kila baada ya fundisho, uwajibishwaji kila baada ya fadhila na neema na bila shaka jibu ndilo hubainisha na kuwatenganisha watu, anayeshukuru na kafiri, muumini na asiyekuwa muumini, mwenye takwa na fasiki, mutiifu na muasi na Mwislamu na mkaidi. Mwenyezi Mungu ambaye anajua kila jambo na yuko karibu nasi kuliko mishipa ya shingo zetu, atamuuliza mwanadamu maswali baada ya kuondoka humu duniani, kuhusiana na mambo aliyoyafanya na kuyaamini na hivyo kumlazimu kukiri mwenyewe kuhusiana na mambo hayo katika mtihani huo wa mwisho ambao hatakuwa na budi ila kuufanya.

Kuhusiana na hilo, Imam Ali (as) anasema: 'Basi mwombolezaji anayemsindikiza maiti atakaporejea na vilevile aliyepatwa na msiba (atakaporejea nyumbani pia), maiti ataketishwa kwenye kaburi lake huku akiwa na hofu kubwa kutokana na wasiwasi wa kuulizwa maswali na kuteleza (kuanguka) kwenye mtihani.'

Naye Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) anasema katika Hadithi: 'Maiti ataulizwa mambo matano atakapokuwa kwenye kaburi: Kuhusu Swala, Zaka, Hija, Swaumu na Wilaya yake kwetu sisi Ahlul Bait. Kisha Wilaya itayajibu mambo hayo manne yaliyotangulia, kutokea pembe moja ya kaburi kwa kusema: Kila mmoja wenu alikuwa na kasoro na mimi ndiye nitakayefidia na kuikamilisha kasoro hiyo.'

Nam wapenzi wasikilizaji, ni wazi kuwa kila mtu ataulizwa kuhusiana na Wilaya ya Muhammad (saw) na kizazi chake kitoharifu (as) na kuhusiana na imani na itikadi yake kwa Maimamu wa kizazi hicho cha Mtume (saw). Ni wazi kuwa muulizaji wa maswali hayo tutakayolazimika kuyajibu ni Mwenyezi Mungu mwenyewe Subhanahu wa Taala kutokana na kauli zake zinazosema: Basi Naapa kwa Mola wako! Tutawahoji wote (Hijr: 92), Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa (as-Swafaat:24) na Tena bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo juu ya neema (at-Takaathur: 8).

**********

Ndugu wasikilizaji katika Sura tukufu ya al-Hijr, Mwenyezi Mungu anamuhutubu Mtume wake mpendwa al-Mustafa (saw) kwa sisitizo maalumu kwa kusema: Basi Naapa kwa Mola wako Mlezi! Tutawahoji wote. Kwa waliyokuwa wakiyatenda. Basi wewe yatangaze uliyoamrishwa, na jitenge na washirikina.

Na hapa tunaashiria mtazamo wa mfasiri mashuhuri wa Qur'ani Tukufu ambaye ni wa madhehebu ya Hanafi naye si mwingine bali ni al-Hafidh al-Hakim al-Hasakani ambapo anasema katika Tafsiri yake ya Shawahid at-Tanzil Liqawaid at-Tafdhwil akimnukuu as-Sadiyy kuhusiana na kauli hiyo ya Mwenyezi Mungu inayosema, Naapa kwa Mola wako Mlezi! Tutawahoji wote kwamba: 'Ni Wilaya ya Ali, kisha akaendelea kusema, Kwa waliyokuwa wakiyatenda, yaani kuhusu waliyoamrishwa na kukatazwa kuyafanya na pia kuhusiana na matendo yao duniani. Kisha as-Sadiyy alisema kwamba kuhusu, Basi wewe yatangaze uliyoamrishwa, na jitenge na washirikina Abu Swalih alisema: Ibn Abbas amesema: Mwenyezi Mungu alimuamuru Mtume wake atangaze na kuidhihirisha Qur'ani na vilevile fadhila na utukufu wa Ahlul Bait wake kama alivyoitangaza Qur'ani.'

Hivyo wapenzi wasikilizaji, watu wataulizwa kuhusiana na Wilaya ya Ahlul Bait na Uimamu wao, mapenzi na utiifu wao kwao (as). Miongoni mwa watukufu hao ni Maimamu wawili wema, Mabwana wa Vijana wa Peponi, wajukuu na maua mawili ya Mtume Muhammad (saw), al-Hassan na al-Hussein na kisha baada yao ni Maimamu wengine tisa kutoka kizazi cha Imam Hussein, amani na rehema za Mwenyezi Mungu ziwateremkie wote. Watukufu hao ndio wale wale ambao Wasia, Uimamu na Ukhalifa wao inafungamana na kushikamana moja kwa moja na Wasia na Uimamu wa Imirul Mu'mineen Ali (as). Ni wazi ndugu wasikilizaji, kwamba sote tutaulizwa kuhusiana na Wilaya na Uimamu wa watukufu hawa kama anavyosema Mwenyezi Mungu Mwenyewe katika Kitabu chake kitakatifu: Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa.

Hebu sasa wapenzi wasikilizaji, tuone mtazamo wa mmoja wa wanazuoni wa Kishafi' wa Hadithi kuhusiana na maana ya Aya hii, naye si mwingine bali ni Ibn Hajar al-Makki al-Haitami ambaye amenukuu katika kitabu chake cha as-Swaiq al-Muhriqa Hadithi kutoka kwa Abu Said al-Khidr kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisema: 'Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa, wataulizwa juu ya Wilaya ya Ali.' Kisha Ibn Hajar akasema: 'Na hili ndilo lililokuwa kusudio la pekee la an-Naisaburi, (mwandishi wa kitabu cha Asbab an-at-Tanzil) aliposema: Imepokelewa kuhusiana na kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Na wasimamisheni. Hakika hao watasailiwa kwamba ni Wilaya ya Ali na Ahlul Bait wa Mtume wake, kwa sababu Mwenyezi Mungu alimuamuru Mtume wake (saw) awaambie watu kwamba hakutaka malipo yoyote kutoka kwao kutokana na tablighi pamojan na ulinganiaji wa ujumbe aliowafikishia ila upendo na mapenzi kwa Watu wa Nyumba yake (Aali zake). Na maana ya, Hakika hao watasailiwa ni kwamba, je, waliwafuata kikweli kama walivyotakiwa kufanya na Mtume (saw) au waliwakaidi na kuwapuuza na hivyo kustahiki kuadhibiwa?'

Na katika hili alimtangulia Ibn Hajar mwanzuoni mwingine mashuhudi wa Kihanafi ambaye ni Jamal ad-Deen az-Zarandi katika kitabu chake cha Nadhm Durar as-Simtain fi Fadhail al-Mustafa wal Murtadha waL Batul wa as-Sibtain, yaani al- Hassan na al-Hussein (as). Pia maana hii imeungwa mkono na Abu Bakr bin Shahab as-Deen al-Hadhrami katika kitabu chake cha ar-Rashfat as-Swadi

**************

Na Ibn Hajar ameandika katika kitabu chake cha as-Swawaiq, as-Shabrawi as-Shafi' katika al-Ittihaf Bihubbil Ashraaf, al Hadhrami as-Shafi' katika ar-Rashfat as-Swadi min Bahar Fadhail Bani an-Nabbiy al-Hadi na al-Qadhi Ayadh katika as-Shifaa Bitaarif Huquq al-Mustafa kwamba Mtume (saw) alisema: 'Kuwajua Aali za Muhammad ni kuepuka Moto, kuwapenda ni kibali cha kupita kwenye Siraat (njia nyembamba) na Wilaya yao (kufuata mwongozo na uongozi wao) ni kinga dhidi ya adhabu ya Mwenyezi Mungu…..'

Nam ndugu wasikilizaji, hii ndio njia ya wokovu na kufuzu, yaani kutambua maarifa na itikadi ya watukufu hao kwa pamoja, kuwapenda na kuwaenzi na hatimaye kuwachukia maadui wao na kufuata uongozi wao wa mbinguni. Ama kuhusu maarifa ni kama walivyosema baadhi ya wanazuoni akiwemo al-Qadhi Ayaadh anayesema: 'Ni maarifa kuhusu nafasi ya Aali za Muhammad (as) mbele ya Mtume huyo Mtukufu (saw). Ikiwa mtu ataitambua vyema nafasi hiyo basi bila shaka atatambua wajibu wa haki na utukufu wao kwa sababu ya Mtume (saw).'

Hivyo wapenzi wasikilizaji, kuna maswali, waulizwaji na anayeruliza maswali hayo pamoja na majibu ya wazi yanayostahili kutolewa na pia njia watakayoelekezwa watoaji wa majibu hayo. Mtume amelizungumzia wazi suala hilo na kuwanasihi masahaba zake kwa kusema, kama alivyonukuu Muslim na wenzake: 'Nitakuulizeni kuhusu Thaqalaini (Vizito Viwili- Qur'ani na Ahlul Bait) mtakapofika mbele yangu, hivyo tazameni mnaniwakilisha (mnanizingatia) vipi kwenye viwili hivi: Kizito kikubwa cha kwanza ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hii ni Kamba ambayo moja ya pande zake iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu na upande mwingine uko mikononi mwenu. Hivyo, shikamaneni nayo ili msije mkapotea wala kubadilika. Na Kizito kidogo (cha pili) ni Kizazi changu ambao ni Ahlul Bait wangu. Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu mrehemevu na mjuzi wa mambo yote amenipasha habari kwamba viwili hivi vyenye thamani kubwa havitatengana hadi vitakaponifikia kwenye Hodhi.'

Na katika Ahlul Bait hao wa Mtume Mtukufu (saw) ni Maimamu Hassan na Hussein (as) ambao watu wataulizwa juu yao na jinsi walivyoamiliana nao humu duniani, hivyo tutahadhari tusije tukatoa jibu ambalo litakuwa ni la kukatisha tamaa na hatimaye kutusukuma Motoni!

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Bsi hadi tutakapojaaliwa kukutana tena katika kipindi kingine, saa na siku kama ya leo, tunakuageni nyote kwa kusema Wassalam Aaleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.