Jun 07, 2016 08:31 UTC

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Ni wakati mwingine umewadia wa kuwa nanyi katika dakika chache za kipindi chetu cha leo cha ufufuo na safari ya mja kurejea kwa Mola Muumba. Katika vipindi kadhaa vilivyopita tulizungumzia suala la mauati na maisha ya milele ya mwanadamu na kusema kuwa, itikadi ya kuwepo ulimwengu wa Akhera ni itikadi ya kimaumbile iliyopo katika fitra ya mwanadamu.

Hapa yumkini likajitokeza swali kwamba, kama kweli mwanadamu ana maisha ya milele katika ulimwengu mwingine na kwamba roho yake haitoweki na kutokomea baada ya kutengana na mwili, kwa nini basi wanadamu wengi wanaogopa kifo? Kipindi chetu cha leo kitatoa jibu la swali hili.  

Akthari ya watu wanaogopa kifo na hawana hisia nzuri kuhusiana na suala hilo. Watu hao hukiona kifo kama zimwi au ndoto ya kutisha ambayo huifanya hata asali kuwa chungu kama shubiri. Kama tulivyosema huko nyuma, mwanadamu ana hamu ya kimaumbile ya kuwa na maisha ya milele. Hata hivyo baadhi ya wanadamu –kwa makosa- huitasawari na kuiweka dunia hii ya kimaada mahala pa maisha ya milele, kwa msingi huo hukimbia na kuogopa kifo na mauti kwa dhana kwamba ndio mwisho, kuangamia na kutoweka kwao kabisa. Iwapo tunataka kutoa mfano unaohisika vyema zaidi kuhusu kifo tunapasa kusema kuwa, mauti na kifo ni mithili ya kuzama jua, kwani wakati jua linapozama katika sehemu ya dunia, huchomoza wakati huo huo katika sehemu nyingine ya dunia. Kifo ni kuzaliwa upya mwanadamu lakini katika ulimwengu mwingine sawa kabisa na jua linalozama katika sehemu moja ya dunia na kuchomoza katika dunia na ulimwengu mwingine.  

<<<<   >>>>>>

Kama tulivyoashiria hapo kabla, miongoni mwa sababu za kuogopa kifo na mauti ni ujahili na kutojua uhakika wa kifo na kuaga dunia. Imepokewa katika hadithi kwamba, bwana mmoja alikwenda kwa Imam Muhammad Jawad (as) na kuuliza: "Kwa nini baadhi ya watu wanachukia kifo? Alisema: Kwa sababu hawayajua mauti na kifo. Iwapo wangejua maana ya kifo na wakawa miongoni mwa mawalii wa Mwenyezi Mungu SW, hapana shaka wangependa kifo na mauti na wangeelewa kwamba, Akhera ni bora kwao kuliko dunia".

Ili kuweka zaidi uhakika huo, Imam Jawad (as) aliendelea kwa kuuliza: Kwa nini mtoto mdogo au kichaa hukataa kula au kumeza dawa inayotibu mwili na kuondoa maumivu yake? Bwana yule alisema: Kwa sababu hawajui faida ya dawa. Imam alisema: Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu aliyemtuma Muhammad (saw) kwamba lau wanadamu wangejua kuwa mauti na kifo kinawafikisha katika neema zipi basi wangependa mauti na kifo kuliko mtu mwenye akili na busara anayetumia dawa kwa ajili ya kutibu ugonjwa na kupata afya na uzima."

Kwa msingi huo tunatambua kuwa, kutokuwa na habari kuhusu mustakbali wa mwanadamu ni miongoni mwa sababu za kuogopa kifo na mauti.    

<<<<<    >>>>>>>

Imepokewa katika hadithi nyingine kwamba, Imam Ali al Hadi (as) alikwenda kumjulia hali mmoja kati ya masahaba zake aliyekuwa mgonjwa na kumkuta akilia kwa kuogopa mauti na kifo. Imam Hadi (as) alisema: Ewe mja wa Mwenyezi Mungu! Unaogopa kifo na mauti kwa sababu hujui hakika yake. Kisha alimuuliza: Iwapo mwili wako wote ungekuwa na uchafu na ukawa unaumia na kupata adhabu na mashaka kutokana na uchafu huo, na wakati huo kukatokea majeraha na magonjwa katika mwili wako kisha ukajua kwamba, iwapo utakwenda hamamuni na kuoga humo utaepukana na magonjwa na uchafu huo, je utapendelea kwenda hamumuni kuoga au la?

Bwana alili asema: Ndiyo sayidi wangu, nitapenda kwenda hamamu na bafuni kuoga. Imam Hadi (as) alisema: "Mauti kwa muumini ni sawa na hamamu na bafu hiyo na humsafisha na machafu yote. Machafu yaliyosababishwa na madhambi ya duniani na ambayo bado hayajafutwa, hufutika na kuondolewa na kifo", mwisho wa hadithi.

Hivyo basi woga wa kifo na mauti una sababu tofauti kulingana na itikadi za watu mbalimbali. Baadhi ya wanadamu hawayatambui mauti na kifo kuwa ni kuangamia na kutoweka kabisa na kamwe hawakani suala la kuwepo maisha mengine baada ya kufariki dunia. Hata hivyo watu hawa wanaogopa mauti na kifo. Watu wa aina hii ni wale wanaoiashiki na kuipenda sana dunia na vilivyomo. Kwa mfano wakati gundi inapowekwa katika kiganja cha mkono wa mwanadamu kisichokuwa na manyoya, gundi hiyo inapobanduliwa kiganjani hapo huwa haisababishi maumivu makali kwa mwenye mkono huo. Lakini pale gundi hiyo hiyo inaponata katika sehemu yenye manyoya au nywele nyingi ya mwili wa mwandamu, huwa vigumu sana kuiondoa mahala hapo, na kuiondoa kwake husababisha maumivu makubwa. Vivyo hivyo mwanadamu anayeiashiki, kuipenda na kuikumbatia sana dunia, kama gundi inavyonata kwenye kiungo chenye manyoya; huwa vigumu sana kwake kutengana na dunia. Imepokewa kwamba, mtu mmoja alimuuliza Mtume Muhammad (saw) sababu ya watu kuchukia mauti na kifo. Mtukufu huyo alimuusia kwa kumwambia: "Kama una mali itoe katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kipindi cha baada ya kufariki dunia, kwa sababu roho ya mwanadamu hugandamana na mali yake. Hivyo kama ataituma mapema zaidi kwa ajili ya kipindi cha baada ya mauti na kifo, atapenda kuifuata huko alikoituma, na kama mali yake itabakia hapa duniani, huwa hataki kuachilia", mwisho wa hadithi.     <<<<<    >>>>

Wapenzi wasikilizaji kipindi chetu cha leo kinaishia hapa kwa leo. Msikose kuwa nasi juma lijalo katika sehemu nyingine ya kipidi hiki kinachozungumzia maadi na marejeo ya wanadamu huko katika ulimwengu wa Akhera. Hadi wakati huo tunakutakieni kila la kheri.       

<<<<<<     >>>>>>>>

 

Tags