Jumatatu, 22 Agosti, 2022
Leo ni Jumatatu mwezi 24 Mfunguo Nne Muharram 1444 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 22 Agosti 2022 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 395 iliyopita vilijiri vita vya mwisho vya La Rochelle kati ya Wakatoliki na Waprotestanti wa Ufaransa. Vita hivyo vilianza baada ya Waprotestanti kuchochewa na Uingereza. Wakatoliki ambao walikuwa wakiungwa mkono na vikosi vya jeshi la serikali ya Ufaransa chini ya uongozi wa Richelieu, Kansela mashuhuri wa nchi hiyo, walipigana vita na Waprotestanti ambao walikuwa wakipigania maeneo yao katika bandari ya La Rochelle. Vita hivyo vilimalizika baada ya mwaka mmoja kwa kupata ushindi Wakatoliki na kutekwa La Rochelle. ***

Miaka 324 iliyopita katika siku kama ya leo, mkataba wa pande tatu wa Russia, Poland na Denmark ulitiwa saini dhidi ya Sweden. Wafalme wa nchi hizo tatu walikuwa na lengo la kumuangusha Sharel XII mfalme kijana wa Sweden ili kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Ni kwa msingi huo ndipo miaka miwili baadaye mnamo mwezi Aprili mwaka 1700 Miladia nchi wanachama wa mkataba huo wa pande tatu zikaamua kuishambulia Sweden, hata hivyo jeshi la mfalme Sharel XII likakabiliana vilivyo na kutoa pigo kwa nchi vamizi. Baada ya kufikia mapatano na Denmark, mwaka 1704 akaishambulia Poland na kuikalia kwa mabau. Hata hivyo mashambulio ya Sharel dhidi ya Russia hayakuzaa matunda. ***
Siku kama ya leo miaka 162 iliyopita Paul Gottlieb Nipkow mmoja wa wavumbuzi wa televisheni alizaliwa huko Ujerumani. Nipkow alikulia katika familia maskini, lakini juhudi na irada kubwa ilimuwezesha kuendeleza masomo yake ya fizikia hadi chuo kikuu. Paul Gottlieb Nipkow alifanya utafiti mkubwa na hatimaye alifanikiwa kuvumbua transimita ya televisheni. Chombo hicho kilichobuniwa na Nipkow kiliweza kurusha mawimbi ya televisheni katika umbali wa mita 30 na baadaye transimita iliyotengenezwa na mvumbuzi huyo wa Kijerumani ilikamilishwa na wabunifu wengine. ***
Na miaka 158 iliyopita katika siku kama hiii ya leo, mkataba wa kihistoria wa Geneva ulitiwa saini baina ya nchi kadhaa za Ulaya, Asia na Amerika. Lengo la mkataba huo lilikuwa ni kuwasaidia majeruhi katika medani za vita. Kwa mujibu wa mkataba huo, timu za madaktari, watoaji misaada na zana zao zinapaswa kutoegemea upande wowote na zisishambuliwe bali zibakie katika amani wakati wa vita. Mbunifu wa mkataba huo alikuwa Henry Dunant raia wa Uswisi. ***
