Aug 25, 2022 21:54 UTC
  • Ijumaa, 26 Agosti, 2022

Leo ni Ijumaa tarehe 28 Mfunguo Nne Muharram 1444 Hijria sawa na tarehe 26 Agosti 2022.

Siku kama ya leo miaka 788 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, mji wa Baghdad uliokuwa makao makuu ya watawala wa Kiabbasi ulitekwa na Hulagu Khan Mongol baada ya kuuawa Mustaasim aliyekuwa mtawala wa mwisho wa utawala wa Bani Abbas. Mauaji ya mtawala huyo yalihitimisha utawala wa kizazi hicho uliotawala sehemu kubwa ya ulimwengu wa Kislamu kwa kipindi cha miaka 500. Hulagu Khan Mongol hakusita kufanya mauaji na jinai katika uvamizi wake dhidi ya nchi mbalimbali, na baada ya kuteka baadhi ya maeneo ya Iran na kuua watu kwa umati katika maeneo ya mijini na vijijini, aliushambulia mji wa Baghdad na kufanya mauaji ya kinyama ya maelfu ya wakazi wake. Vilevile aliharibu na kuvunja nyumba na majengo muhimu ya mji wa Baghdad. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 676 iliyopita mzinga mkubwa ulitumika kwa mara ya kwanza katika historia. Siku hiyo jeshi la Uingereza lilitumia silaha ya mzinga dhidi ya askari wa Ufaransa. Katika vita hivyo Mfalme Philip wa Sita wa Ufaransa alishindwa vibaya na jeshi la Uingereza licha ya kwamba jeshi la Ufaransa lililokuwa limekaribia kupata ushindi, lilikuwa na idadi kubwa ya askari na wapiganaji. Ushindi wa jeshi la Uingereza katika vita hivyo ulitokana na utumiaji wa silaha ya mzinga. ***

 

Miaka 279 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa mjini Paris Ufaransa Antoine Laurent Lavoisiere, mtaalamu wa kemia wa Kifaransa. Baada ya kumaliza masomo yake alianza kufanya utafiti katika elimu ya kemia. Miongoni mwa uvumbuzi wa msomi huyo ni kwamba, maji yanaundwa na vitu viwili yaani gesi za oksijeni na haidrojeni na mchango wa hewa ya oksijeni katika kuchomeka vitu mbalimbali. Mwaka 1794 Antoine Laurent Lavoisiere alituhumiwa kuwa anapinga mapinduzi na kunyongwa hapo baadaye. ***

آنتوان لوران لاوازیه

 

Siku kama ya leo miaka 126 iliyopita askari wa utawala wa Kiothmani walianza kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waarmenia. Waturuki wa Kiothmani walifanya mauaji hayo kwa kisingizio kwamba Waarmenia waliwasaidia Wagiriki katika ghasia zilizofanyika dhidi ya utawala wa Kiothamani. Maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wadogo wa Kiarmeni waliuawa kwa umati katika mauaji hayo yaliyoendelea kwa kipindi cha siku tano. ***

قتل عام ارامنه توسط نیروهای امپراتوری عثمانی

 

Katika siku kama hii ya leo miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 4 Shahrivar 1358 Hijria Shamsia, Mehdi Araghi na mwanawe Hissam waliuawa shahidi na magaidi wa kundi la Munafiqin (MKO). Mahdi Iraqi alikuwa mmoja wa shakhsia watajika wa Mapinduzi ya Kiislamju ya Iran na alifanya mapambano kwa miaka kadhaa dhidi ya utawala wa Shah. Mehdi Araghi alikuwa na uhusiano wa karibu na Imam Khomeini MA. Mwanamapambano huyo muumini alifungwa jela na utawala wa Shah kwa miaka kadhaa na kukumbana na mateso mengi. ***

 

Na siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio nambari 620 likilaani hatua ya Iraq ya kutumia silaha za kemikali. Baada ya utawala wa zamani wa Iraq kushambulia kwa mabomu ya kemikali makazi ya raia nchini Iran na kufuatia mashtaka yaliyowasilishwa na Iran, ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa katika nchi za Iran na Iraq na ukatoa ripoti mbili ambazo zilieleza kuwa, utawala huo ulitumia mara kadhaa silaha za kemikali dhidi ya majeshi na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kukiri waziwazi kwamba, jeshi la Iraq lilitumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Katika kipindi chote cha vita vya miaka 8 vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, utawala wa Saddam Hussein uliua shahidi maelfu ya wanajeshi na raia wa Iran kutokana na kutumia silaha za gesi yenye kemikali. Kwa sababu hiyo Iran inatambuliwa kuwa mhanga mkubwa zaidi wa silaha za kemikali duniani baada ya Vita vya Pili vya Dunia.