Nov 10, 2022 17:36 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (43)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 43 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho maudhui yake ya leo ni kuhusu umuhimu na udharura wa kujitawala na kujitegemea kiuchumi. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Tukiendelea na mazungumzo yetu kuhusu "Akhlaqi za Kiuchumi" tunaweza kusema kuwa mojawapo ya masuala muhimu na yenye kubadilisha hatima ya jamii ni "kujitawala kiuchumi". Vinara wa nguvu za kisiasa na kiuchumi katika mfumo wa uistikbari wa dunia wanapanga mikakati na kuandaa mbinu zenye malengo maalumu ili waweze kuyaburuza mataifa ya ulimwengu na kuyatwisha matakwa yao, kwa kuhakikisha kuwa badala ya mataifa hayo kuwa na utamaduni wa kujitawala na kujitegemea kiuchumi, yanaendelea kuwa tegemezi kiuchumi kwa madola hayo ya kibeberu. Yanachofanya madola hayo ni kuendeleza mfumo wa kusafirisha na kuuza bidhaa zao za kila aina kwa mataifa manyonge na yaliyobaki nyuma kimaendeleo; na wakati huohuo kuimarisha mihimili ya satua na ushawishi wao katika nchi hizo; na kwa njia hiyo kufanikisha malengo yao ya kisiasa na kiutamaduni ndani ya mataifa hayo. Lakini mkabala na hayo, Uislamu wa asili, unaotegemea utamaduni wa Tauhidi ambao unalinda izza, heshima na mamlaka ya Waislamu na kuzima njama za maadui, unafuata mfumo wa kiuchumi wa Uislamu ili kupambana na utegemezi wa maajinabi. Kwa kufanya hivyo unajitahidi kuhuisha ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu moyo wa "kujitegemea kiuchumi", ili katika kukabiliana na mihimili ya nguvu za kisiasa na kiuchumi ya kambi ya ubeberu, mataifa ya Kiislamu, sio tu yasijihisi dhaifu na yasiyo na uwezo, bali yawe na azma thabiti na isiyotetereka ya kuhakikisha yanajivua kila aina ya utegemezi; na badala yake kujitegemea yenyewe ili kupata nguvu, kuheshimika na kuwa na uwezo kamili.

Hapa sasa linajitokeza suali la msingi, nalo ni, vipi Ulimwengu wa Kiislamu, utaweza "kujitawala na kujitegemea kiuchumi" na kujikomboa na ubeberu wa kiuchumi na Uistikbari wa dunia? Msingi muhimu zaidi utakaowezesha Ulimwengu wa Kiislamu kuwa na utamaduni wa kujitegemea kiuchumi ni kuwa na "moyo wa kujiamini". Kinyume na siasa na sera zenye malengo maalumu za Uistikbari wa dunia, ambazo siku zote  zimekuwa zikijaribu kuhakikisha kuwa badala ya kujiamini, hisia za kujidunisha na kukosa uwezo zinaendelea kutawala katika Ulimwengu wa Kiislamu, inapasa Waislamu wafahamu kwamba, kama watautumia ipasavyo uwezo na utajiri wao wa rasilimaliwatu na maliasili chungu nzima walizojaaliwa na Mwenyezi Mungu, na wakahuisha na kudumisha utamaduni wa kuchapa kazi na uzalishaji, hakuna shaka yoyote, wataweza kujitawala na kujitegemea kiuchumi.

Mbinu na hila nyingine inayotumiwa na wenye nguvu za kisiasa na kiuchumi duniani ili kuyazuia mataifa manyonge yasijitegemee kiuchumi ni kueneza utamaduni wa utumizi wa kiisrafu ili watu wa mataifa hayo waendelee kuwa wahitaji kwao. Katika kukabiliana na mtazamo huo, Uislamu unaishajiisha jamii ya Kiislamu ilee na kukuza vipawa vyake na kuzitumia ipasavyo suhula zake za kimaada na kimaanawi ili kuweza kujitegemea na kujivua na kila aina ya utegemezi. Lakini ifahamike pia kwamba lengo la mfumo wa kiuchumi wa Uislamu si kukata mawasiliano ya kibishara na kiuchumi na nchi au mataifa mengine. Ilivyo ni kuwa, mataifa ya Kiislamu yanaweza kutumia tajiriba na uwezo wa kiuchumi wa wasiokuwa wao kwa msingi wa kuwa na uhusiano sahihi wa kiuchumi na wa pande mbili, na kwa kutumia kwa busara na kimalengo uzoefu wa watu wengine, kufikia hatua ya kujitegemea na kuondokana na utegemezi wa maajinabi.

Miongoni mwa mambo yanayoupa nguvu utamaduni wa utumizi wa kiisrafu na kushamirisha utamaduni wa utegemezi ni tabia ya "kupenda anasa". Tabia hii hubadilisha kikamilifu mtindo wa maisha na wa matumizi na kupelekea kumiminika bidhaa za gharama kubwa, za anasa na za kifakhari kwenye nchi zilizoathiriwa na Umagharibi na kuyumbisha misingi ya utamaduni wa kujiamini na kujitegemea katika jamii za nchi hizo. Uislamu unapiga vita aina yoyote ile ya kupenda anasa na maisha ya kifakhari na kuwashajiisha Waislamu waishi maisha ya kawaida na kujizoeza mtindo wa maisha ya kadiri na wastani.

Inafaa tukumbushe pia kuwa, pamoja na hayo, Uislamu unashajiisha watu kujiburudisha na mazuri ya maisha, ambayo yanatofautiana kikamilifu na mambo ya fakhari na anasa. Bwana Mtume SAW amesema: "Mwenyezi Mungu ni mzuri na anapenda mazuri".

Jambo jengine lenye taathira kubwa sana katika kufanikisha lengo la "kujitegemea kiuchumi" ni kuifanyia kazi kaulimbiu ya "tunaweza". Kwa maneno mengine ni kwamba, irada na utashi wa watu wenyewe wa mataifa ndio wenye taathira kuu katika kufikia malengo na matarajio yao. Ni kama isemwavyo katika methali moja ya Kiajemi "Kuweza ni Kutaka". La muhimu ni kwamba, ili kila taifa lifikie hatua ya "kujitegemea kiuchumi" inapasa lijipinde kwa kufanya juhudi kubwa na kuwa na irada na azma thabiti ili liweze kufikia lengo lililolikusudia pasi na kuyumba wala kuvunjika moyo au kukata tamaa kwa namna yoyote ile. Qur'ani tukufu inalizungumzia hilo kama aya ya 11 ya Suratu-Ra'ad inavyosema: "Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo naf- sini mwao…

Hapana shaka yoyote, ikiwa watu wa mataifa yenyewe wataamua, misingi ya "kujitegemea kiuchumi" itaimarika kupitia ushindani chanya na wa kiujengaji katika ulimwengu wa uchumi. Na katika hali na mazingira hayo, utamaduni wa utegemezi na kuridhia siasa na sera za mihimili ya kibeberu ya nguvu za kisiasa na kiuchumi duniani utabadilika na kuwa utamaduni wa ushindani na upigaji hatua mbele na kupatikana matunda na mafanikio makubwa.

Hatua nyingine muhimu inayopasa kuchukuliwa na mataifa, hasa ya Ulimwengu wa Kiislamu, -ambayo ni kitovu cha maliasili chungu nzima za mafuta na gesi, ardhi za kilimo zenye rutuba, aina zote za hali ya hewa na anuai za madini muhimu-, ni kuachana na utaratibu wa kuuza malighafi zao. Yanachopaswa kufanya ni kuzisarifu malighafi zao katika sura ya bidhaa, kisha ndipo yazisafirishe kwenda kuziuza nje ili kuweza kunufaika kikamilifu na matunda ya utajiri wao. Qur'ani tukufu imelitolea maelezo wadhiha na ya wazi suala hilo kama inavyoeleza aya ya 39 na 40 za Suratu-Najm: "Na ya kwamba hatapata mtu ila aliyo yahangaikia? Na kwamba aliyoyahangaikia yataonekana?"

Hatimaye hatua hizo athirifu na zenye umuhimu wa kipekee zitajenga moyo wa matumaini kwa mustakabali ung'arao, wa kuheshimika, wa kujitegemea na kujitawala Ulimwengu wa Kiislamu kupitia umoja, mshikamano na mashirikiano; na kwa auni na msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwarejeshea tena adhama yao iliyowatoka ya Ustaarabu adhimu wa Kiislamu.

Ili Waislamu wasijiegemeze na kuelekeza matumaini yao kwa maajinabi, aya ya 139 ya Suratu Aal Imran inawaambia: "Wala msilegee, wala msihuzunike, kwani nyinyi ndio wa juu ikiwa nyinyi ni Waumini." Na kwa tarjumi ya aya hiyo mpendwa msikilizaji niseme pia kuwa sehemu ya 43 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 44 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/