Alkhamisi tarehe 15 Disemba 2022
Leo ni Alkhamisi tarehe 20 Jumadil Awwal 1444 Hijria sawa na tarehe 15 Disemba 2022.
Siku kama ya leo miaka 762 iliyopita inayosadifiana na tarehe 20 Jumadil Awwal 682 Hijria, alizaliwa Muhammad bin Hassan Hilli mwenye lakabu ya Fakhrul Muhaqqiqiin katika mji wa Hilla nchini Iraq. Muhaqqiq Hilli alibobea na kutabahari kwenye elimu za Tafsiri ya Qur’ani, Fiqh na Usulul Fiqh. Mwanachuoni huyo alipata elimu ya kidini kutoka kwa mzazi wake, Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake. Fakhrul Muhaqqiqiin ameandika vitabu vingi miongoni mwavyo ni "Sharh Mabadiul Usul", "Tahswilul Najat" na “al Kafiya”. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 771 Hijria.

Siku kama ya leo miaka 707 iliyopita yaani tarehe 20 Jamadil Awwal mwaka 737 alifariki dunia faqihi wa Kiislamu Abu Abdullah Muhammad ibn Hajj al-Abdari al-Fasi mashuhuri kwa jina la Ibn Hajj. Al Fasi awali alipata elimu kwa maulamaa wa mji wa Fas huko Morocco ya leo. Baadaye alielekea Cairo na kuishi huko hadi mauti yalipomfika. Faqihi Abu Abdullah al Fasi ameandika vitabu vingi vya thamani kikiwemo kile cha al Mad-khal. Katika kitabu hicho, Ibn Hajj amechunguza masuala mbalimbali yakiwemo ya kiakhlaqi, kifiqi, kijamii na kiuchumi.

Katika siku kama ya leo miaka 190 iliyopita alizaliwa Alexandre Gustave Eiffel mhandisi na msanifu wa mnara mashuhuri wa Eiffel. Umashuhuri wa Alexandre Gustave unatokana zaidi na usanifu na uhandisi wake wa mnara wa Eiffel mjini Paris ulioanza kujengwa tarehe Mosi Julai 1887 chini ya usimamizi wake. Mnara wa Eiffel una urefu wa mita 324 ambapo katika zama zake ulikuwa mnara mrefu zaidi duniani. Alexandre Gustave Eiffel aliaga dunia tarehe 27 Desemba 1923 akiwa na umri wa miaka 91.
Siku kama ya leo miaka 170 iliyopita alizaliwa mwanafikizia wa Kifaransa Henri Becquerel. Henri ambaye ndiye aliyevumbua nururishi au Radioactivity baada ya kufanya utafiti katika mada za urani na vitu vinginevyo, alianza kufanya jitihada za kupata vitu vinavyotoa miali ya X baada ya miali hiyo kugunduliwa na mwanafizikia wa Kijerumani, Wilhelm Conrad Röntgen 8 November 1895. Mwaka 1896 Becquerel aligundua nururishi inayoweza kuzalisha miali ya X. Utafiti wa mwanafikizia huyo wa Kifaransa ulimfanya atunukiwe tuzo ya Nobel mwaka 1903. Msomi huyo alifariki dunia mwaka 1908.
Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, yaani tarehe 24 Azar 1329 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Hujjatul Islam Sheikh Mahdi Waidhi Khorasani. Msomi na alimu huyo wa Kiirani aliyekuwa mmoja wa watoa waadhi na makhatibu mashuhuri katika zama zake alikuwa na azma na irada imara ya kueneza na kuwafikishia walimwengu maarifa ya Uislamu na ya Ahlul-Bait (as). Sheikh Mahdi Waidhi Khorasani alikuwa akitoa mihadhara mjini Mash'had Iran na katika miji mingine na kadhalika katika Haram ya Imam Hussein (as) katika mji wa Karbala na Haram ya Imam Ali bin Abi Twalib (as) huko Najaf, Iraq. Hatimaye akiwa na umri wa takribani miaka 82 aliaga dunia katika siku kama ya leo na kuzikwa katika Haram ya Imam Ali bin Mussa al-Ridha (as) mjini Mash'had.
Miaka 66 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo alifariki dunia Walt Disney shakhsiya mashuhuri wa sekta ya filamu za watoto. Disney alizaliwa mwaka 1901 huko Marekani. Walt Disney alihitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Havard na kutunukiwa shahada ya udaktari katika sayansi ya uchoraji na uchongaji (Fine Art). Disney alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha sanaa ya filamu za katuni. Mara kadhaa alitunukiwa tuzo za Oscar katika uwanja huo wa kutengeneza filamu za katuni.
Na miaka 47 iliyopita katika siku kama hii ya leo yaani tarehe 15 Disemba 1975, majeshi ya kikoloni ya Uhispania yalianza kuondoka Sahara Magharibi. Polisario ni moja ya harakati za ukombozi wa Sahara Magharibi iliyowalazimisha Wahispania kukimbia eneo hilo. Harakati hiyo iliundwa mwaka 1973 baada ya wanamapinduzi wa Sahara kuasisi makundi kadhaa ya kupigania ukombozi wa eneo hilo.
