Jumanne, 10 Januari, 2023
Leo ni tarehe 17 Jamadithani mwaka 1444 Hijria sawa na Januari 10 mwaka 2023.
Siku kama ya leo miaka 920 iliyopita, yaani tarehe 17 Jamadithani mwaka 524 Hijiria, alifariki dunia Bari'i Baghdadi, mwanafasihi na malenga mashuhuri wa Kiarabu. Baghdadi alizaliwa mwaka 443 Hijiria na kuanza kusomea elimu ya nahau na lugha kutoka kwa maulama wakubwa wa kipindi chake. Moja ya athari mashuhuri za Bari'i Baghdadi ni kitabu cha mashairi kilichopewa jina lake. Malenga na mshairi huyo aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 81 hali akiwa ni kipofu. ***
Miaka 857 iliyopita katika siku kama ya leo kulitiwa saini makubaliano ya kisiasa ya Acre katika kipindi cha Vita vya Msalaba baina ya Waislamu na wapiganaji wa Kikristo. Makubaliano hayo yalitiwa saini kwa ajili ya kukabidhiwa mji wa Acre kwa Wakristo na mkabala wake kuachiliwa huru mateka wa Kiislamu wapatao 3,000. Hata hivyo na bila ya kuheshimu makubaliano hayo, Wakristo waliwaua mateka hao wa Kiislamu suala lililosababisha kuanza tena kwa Vita vya Msalaba ambavyo vilimalizika kwa kushindwa vibaya Wakristo. Mji wa Acre ulikombolewa na Waislamu katika karne ya 15 Hijiria na ukachukuliwa tena na Wamagharibi mwaka 587.***
Siku kama ya leo miaka 124 iliyopita yaani tarehe 17 Jumadithani mwaka 1320 Hijiria, alifariki dunia msomi wa Kiislamu Hajj Mirza Hussein Nuri. Msomi huyu mkubwa alifikia daraja ya juu katika ibada, uchamungu na ukamilifu wa nafsi. Hajj Mirza Hussein Nuri hakuwa mbali na uandishi wa vitabu. Vitabu vyake vingi vilihusu elimu za Hadithi, tafsiri ya Qur'ani na ufafanuzi kuhusiana na maisha ya wasomi wa Kiislamu na masuala mengine muhimu. Mirza Hussein Nuri Tabrasi alilipa umuhimu mkubwa suala la kueneza athari za Ahlubaiti wa Mtume (saw). Hadi sasa zipo athari kadhaa kutoka Hajj Mirza Hussein Nuri Tabrasi, ambapo miongoni mwa athari zake mashuhuri ni kitabu cha "Mustadrakul Wasaail" ambacho kimekusanya habari za hadithi na ufafanuzi wa hali za maulama wa Kiislamu.***
Katika siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, inayosadifiana na 10 Januari 1920, Jumuiya ya Mataifa ilianza shughuli zake rasmi huko Geneva, Uswisi. Jumuiya hiyo iliundwa baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia kwa shabaha ya kuimarisha amani na usalama duniani. Mwanzoni nchi za Kiafrika na Urusi hazikujiunga na jumuiya hiyo na badala yake nchi za Uingereza na Ufaransa ndizo zilizobeba jukumu la kuzisaidia nchi hizo. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, mnamo mwezi Aprili 1946, uliundwa Umoja wa Mataifa na kuchukua nafasi ya Jumuiya ya Mataifa, ingawa matatizo yaliyokuwa yakiikumba Jumuiya ya Mataifa bado yanaendelea kuukumba Umoja wa Mataifa hadi hii leo. ***
Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, wataalamu wawili wa Uswisi walifanikiwa kutengeneza saa ya elektroniki. Baada ya miaka 12 ya juhudi kubwa, hatimaye wataalamu Solvil na Titus walifanikiwa kutengeneza chombo hicho kwa kuweka vifaa kadhaa muhimu na makini. Aina hii ya saa ni makini mno na hufanya makosa machache sana ikilinganishwa na saa nyingine. ***
