Jan 14, 2023 22:52 UTC
  • Jumapili, 15 Januari, 2023

Leo ni Jumapili tarehe 22 Mfunguo Tisa Jamadithani 1444 Hijria mwafaka na tarehe 15 Januari 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1053 iliyopita, alifariki dunia mtaalamu wa mashairi wa Kiislamu kwa jina la Ibn Hajjaj. Ibn Hajjaj alizaliwa mjini Baghdad, Iraq na alijikita katika taaluma ya mashairi akiwa bado kijana na kutokea kuwa maarufu katika uwanja huo. Alitunga mashairi mengi yanayowaenzi na kuwasifu Ahlul bait wa Mtume (saw) na kuwashambulia wapiznani wa Uislamu na Mtume. Miongoni mwa athari za malenga huyo ni pamoja na diwani ya mashairi yenye juzuu kumi inayohifadhiwa katika maktaba mbalimbali duniani. ***

 

Miaka 228 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Aleksandr Griboyedov mwandishi na mwanasiasa asiye na ustahiki wa Urusi. Alikuwa na umahiri mkubwa katika uandishi wa drama na michezo ya kuchekesha. Aleksandr Griboyedov hakupata mafanikio ya uga wa siasa. Wakati wa kujiri vita vya pili vya Iran na Urusi alikuwa miongoni mwa maafisa wa Kirusi. Baada ya Iran kushindwa katika vita hivyo, Griboyedov alipewa amri na mtawala wa Tsar mwaka 1828 aje Tehran ili akawachukue mateka wa Kirusi waliokuwa wakishikiliwa Iran. Majigambo na kutokuwa na tajiriba pamoja na utumiaji mabavu wake wakati wa safari yake hii, ni mambo yaliyochochea hisia za wananchi wa Iran na kuanzisha uasi dhidi yake ambao ulipelekea kuuawa kwake mwaka 1829. ***

Aleksandr Griboyedov

 

Katika siku kama ya leo miaka 184 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 15 Januari 1839, nchi ya El Salvador ilijitangazia rasmi uhuru wake baada ya kusambaratika Muungano wa Amerika ya Kati, amma nchi hiyo haikupata amani na utulivu hata baada ya kupita karne moja. El Salvador ambayo ilikuwa ikikoloniwa na Uhispania kwa miaka kadhaa, ilijipatia uhuru wake mwaka 1821, na ulipofika mwaka 1824 ilijiunga na Muungano wa Amerika ya Kati, na hatimaye uliposambaratika muungano huo, nchi hiyo ilijitegemea kikamilifu. El Salvador ilikabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi mwaka 1931, baada ya kuporomoka bei ya kahawa katika soko la dunia, zao lililokuwa likitegemewa nchini humo. Hali mbaya ya kiuchumi iliwakasirisha wananchi wa nchi hiyo, na kupelekea kuanza kuibuka uasi wa wananchi na wanachuo dhidi ya dikteta Jenerali Maximiliano Hernandez Martinez wa El Salvador. ***

Bendera ya taifa la El Salvador

 

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita inayosadifiana na tarehe 25 Dey 1357 Hijria Shamsia, kulitokea mapigano makubwa baina ya jeshi la utawala wa Shah na wananchi wa Iran kufuatia maandamano ya mara kwa mara ya wananchi dhidi utawala huo wa kidikteta. Katika mapigano hayo baadhi ya wanajeshi waliotambua sababu za mapambano ya wananchi, waliamua kuzikimbia kambi zao za kijeshi na kujiunga katika safu za wananchi. Kujiunga wanajeshi na safu za wananchi ilikuwa bishara njema ya mabadiliko makubwa katika moyo na muundo wa jeshi la utawala wa Shah. Wakati huo huo Imam Khomeini ambaye alikuwa uhamishoni nchini Ufaransa, alikuwa akituma taarifa mara kwa mara akiwahimiza wanajeshi kujiunga na mapambano ya wananchi, kuuhami na kuutetea Uislamu na sheria zake na kuwafukuza wageni waliokuwa wakidhibiti kila kitu nchini Iran. ***

Maandamano dhidi ya Shah

 

Tarehe 15 Januari miaka 22 iliyopita ensaiklopidia ya Wikipedia ilianza kazi katika mtandao wa intaneti. Lengo la kuanzishwa ensaiklopidia hiyo limetajwa kuwa ni kupanua maarifa na uelewa wa watu kupitia njia ya kushirikishwa watu wote katika mradi huo. Insaiklopidia hiyo kubwa ya intaneti ina taarifa na makala kuhusu mamilioni ya vitu kwa lugha mbalimbali na ndiyo inayotembelewa zaidi na watu katika mtandao huo. Hata hivyo uwezekano wa kila mtu kuingia na kuandika atakavyo katika ensaiklopidia hiyo umeshusha chini hadhi na nafasi yake ya kielimu. Zaidi ni kwamba licha ya kuwa wasimamizi wa Wikipedia wanadai hawapendelei upande wowote lakini kwa kawaida makala zinazohusiana kwa njia moja au nyingine na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel huwa za upendeleo. Kituo kikuu cha Wikipedia kiko katika jimbo la Florida nchini Marekani na ensaiklopidia hiyo inafanya kazi kwa mujibu wa sheria za Marekani. ***