Jumapili, Februari 5, 2023
Leo ni Jumapili, mwezi 14 Rajab, 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 5 Februari 2023 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1442 iliyopita yaani tarehe 14 Rajab mwaka wa pili Hijiria, kulijiri vita vya kwanza baina ya Waislamu na washirikiana wa Makka mwanzoni kabisa mwa kudhihiri dini Tukufu ya Kiislamu. Mapigano hayo ya kwanza ya Waislamu baada ya kusimamisha dola mjini Madina, yaliongozwa na Abdullah bin Jahsh Asadi, huku upande wa pili ukiongozwa na Omar bin al Hadhrami ambaye alikuwa kiongozi wa msafara wa Maquraish. Katika mapigano hayo Omar bin al Hadhrami aliuawa. Mapigano hayo yanajulikana katika historia ya Kiislamu kwa jina la Sariyyatu Abdullah bin Jahsh.
Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia na kufuatia amri ya Imam Khomeini MA ya kutangaza kuundwa serikali ya muda ya Mapinduzi nchini Iran, mamilioni ya wananchi Waislamu na Wanamapinduzi wa Iran waliandamana katika miji mbalimbali nchini ili kuuunga mkono na kuidhinisha uamuzi huo wa Imamu Khomeini (M.A). Katika siku hiyo wananchi Waislamu wa Iran walimiminika kwenye mitaa mbalimbali na kwa sauti moja wakitaka kuondoka madarakani serikali kibaraka ya Bakhtiyar. Siku hiyo hiyo pia Jenerali Huyser (inasomwa Haizer) Mjumbe Maalumu wa Marekani ambaye alitumwa Tehran ili kusaidia kuubakisha madarakani utawala wa Pahlavi na kutangaza uungaji mkono wa Marekani kwa makamanda wa jeshi la Shah na kuandaa uwanja wa kujiri mapinduzi dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu hatimaye alirejea nchini kwake mwezi mmoja baada ya kufeli jitihada zake hizo katika uwanja huo.
Katika siku kama ya leo miaka 142 iliyopita alifariki dunia mwanahistoria, mwanafalsafa na mtaalamu mashuhuri wa masuala ya mashariki wa Scotland, Thomas Carlyle. Mwanafalsafa huyo alizaliwa mwaka 1795 katika familia ya watu wa kijijini na mbali na lugha ya Kijerumani, alijifunza pia lugha ya Kiarabu na baadaye alianza kufunza lugha hiyo katika Chuo Kikuu cha Cambridge,London. Katika safari zake nyingi katika nchi za Kiislamu, mwanahistoria huyo alijifunza utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu na kuathirika mno na dini hiyo. Thomas Carlyle anasema kuhusu Qur'ani kwamba: "Qur'ani ni sauti isiyokuwa na wasita kutoka kwenye roho ya ulimwengu, na wanadamu wanapaswa kuisikiliza, la sivyo hawapaswi kusikiliza maneno mengineyo." Mwanafalsafa huyo wa Scotland anasema kuhusu Mtume Muhammad (SAW) kwamba: Mwenyezi Mungu amemfunza hikima na elimu shakhsia huyu adhimu. Alijiepusha na kupenda jaha na ni miongoni mwa watu waliotakaswa na kupendwa mno na Mola Muweza.
Katika siku kama ya leo miaka 44 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, Shirika la Kijasusi la Marekani CIA lilikiri kushindwa kutabiri masuala ya Mapinduzi ya Kiislamu. Maafisa wa CIA walikiri kuwa shirika hhilo limeshindwa kutabiri matukio ya Iran. Walisema, kitu ambacho hatukukitabiri kabisa ni mtu mmoja mzee wa miaka 78 ambaye alibaidishwa nje ya nchi kwa muda wa miaka 14, kuweza kuwaunganisha kiasi chote hiki wananchi wa Iran.
Miaka 25 iliyopita katika siku hii, yaani tarehe 16 Bahman 1376 Hijiria Shamsia, alifariki dunia mtumishi wa Mwenyezi Mungu, Hujjatul Islam "Jalil Honrovar Khoei." Jalil Honravar Khoei alizaliwa mwaka 1305 Hijria Shamsia yaani mwaka 1345 Hijria Qamaria katika mji wa Khoei wa mkoa wa Azarbaijan Magharibi nchini Iran. Alianza mapema kusoma masomo ya dini. Katika miaka kumi na minne ya umri wake, alijifunza fasihi na usul na kutabahari katika fani hizo. Kuanzia mwaka 1337 Hijria Shamsia, alichukua jukumu la kusimamia chuo muhimu cha kidini cha mji huo kwa muda wa miaka 20. Katika kipindi hiki na hadi mwisho wa maisha yake, alifundisha sayansi ya dini na kufunza makumi ya masheikh na walimu mahiri waliondeleza juhudi zake baada yake. Alikuwa akitumia siku nzima kuanzia asubuhi hadi jioni kufundisha mafundisho ya Ahlul-Bayt AS. Alikuwa akitumia muda wake mwingine kutatua masuala ya watu, kuhudumia Waislamu, kutatua hitilafu zao, kujibu maswali yao ya kidini, kusimamia misikiti na shule, na alikuwa akisoma vitabu mbalimbali katika wakati wake wa faragha. Alikuwa na umahiri mkubwa wa Tafsir ya Qur’ani, tarikhi, hadithi na fasihi ya Kiarabu na Kiajemi na ameirithisha vizazi vya baada yake turathi yenye thamani kubwa. Miongoni mwa athari za thamani za Hojjatul Islam Jalil Honravar Khoei, ni kitabu cha "Ufafanuzi wa Majina" ambacho kimehifadhi maelezo ya majina ya Mitume na Manabii, Maimamu, wanazuoni wa Kishia na Kisunni, pamoja na wasifu wa mmoja wa wanazuoni wakubwa.