Feb 06, 2023 02:41 UTC
  • Jumatatu, tarehe 6 Februari, 2023

Leo ni Jumatatu tarehe 15 Rajab 1444 Hijria, sawa na Februari 6 mwaka 2023.

Tarehe 15 Rajab miaka 1449 iliyopita kundi la kwanza la Waislamu lilianza safari ya kuondoka Makka na kuhamia Uhabeshi barani Afrika. Hijra hiyo iliyokuwa na taathira kubwa katika harakati za Uislamu, ilifanyika miaka 8 kabla ya Mtume (saw) kuhamia Madina.

Baada ya kushadidi mashaka ya Waislamu waliokuwa wakiteswa na kusumbuliwa na washirikina wa Makka, Mtume Muhammad (saw) aliwaamuru baadhi ya maswahaba zake waelekee katika ardhi ya Uhabeshi barani Afrika kwa ajili ya kujilinda na adha na mateso ya washirikina. Kundi hilo la Waislamu lililojumuisha wanaume 11 na wanawake 4 likiongozwa na Uthman bin Madh'un, lilihamia Uhabeshi na kutayarisha uwanja na mazingira mazuri ya Hijra ya pili ya Waislamu kuelekea katika ardhi hiyo ya Afrika. Kundi hilo la pili liliongozwa na binamu wa Mtume wetu Muhammad (saw), Ja'far bin Abi Twalib. Hijra hizo mbili zilikuwa na mchango mkubwa wa kueneza zaidi dini ya Uislamu barani Afrika.

Miaka 1442 iliyopita katika siku kama ya leo, mnamo tarehe 15 Rajab mwaka wa Pili Hijria, Kibla cha Waislamu kilibadilishwa kutoka Baitul Muqaddas na kuelekea Makka kwa amri ya Mwenyezi Mungu.

Mayahudi daima walikuwa wakiwakebehi Waislamu kwa vile walikuwa nao wakielekea kwenye kibla hicho hicho cha Baitul Muqaddas. Hali hiyo iliwatia unyonge Waislamu na hasa Mtume Mtukufu SAW, na kwa minajili hiyo, katika siku kama ya leo Mwenyezi Mungu aliteremsha wahyi kwa Mtume SAW kupitia Malaika Jibrail AS akimtaka aelekee Makka wakati wa ibada ya Swala, badala ya Baitul Muqaddas. 

Msikiti wa Dhulqiblatain

Siku kama ya leo miaka 1384 iliyopita mwafaka na tarehe 15 Rajab mwaka 60 Hijria, alifariki dunia Muawiyah bin Abu Sufiyan, adui mkubwa wa Ahlibaiti wa Mtume Muhammad (saw) na mwasisi wa utawala muovu wa Bani Umayyah.

Muawiyah alizaliwa miaka 15 kabla ya kuhama Mtume SAW kutoka Makka na kuelekea Madina, na alisilimu wakati jeshi la Kiislamu lilipoukomboa mji wa Makka mwaka wa 8 Hijria.

Muawiyah alishika ugavana wa Sham wakati wa Ukhalifa wa Omar bin Khattab. Wakati wa uongozi wa Imam Ali bin Abi Twalib (A.S) alianzisha vita vya Siffin kwa kisingizio cha kulipiza kisasi cha kuuawa Othman bin A'ffan. Alibadilisha uongozi wa Kiislamu ni kuufanya sawa na usultani na ufalme wa Warumi. Mbali na kufanya mauaji ya mjuu mkubwa wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hassan bin Ali (as), Muawiyah bin Abi Sufiani pia alimrithisha utawala mwanaye fasiki, mlevi na katili Yazid, ambaye pia alimuua kikatili mjukuu wa pili wa Mtume (saw), Imam Hussein bin Ali (as).

Siku kama ya leo miaka 1382 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alifariki dunia Bibi Zaynab (as) mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw) baada ya kuvumilia mateso na machungu mengi.

Bibi Zaynab (as) alizaliwa mwaka wa 6 Hijria na alipata malezi bora kutoka kwa baba yake, Imam Ali na mama yake, Bibi Fatimat Zahra (as).

Mwaka 61 Hijria, Bibi Zaynab (as) alishiriki katika mapambano ya Karbala pamoja na kaka yake, Imam Hussein (as) na watu wengine wa familia ya Mtume (saw). Baada ya kuuawa shahidi Imam Hussein (as) na wafuasi wake, Bibi Zaynab alikuwa mfikisha ujumbe wa hamasa ya kudumu ya Imam Hussein na wafuasi wake. 

Siku kama ya leo miaka 406 iliyopita alifariki dunia daktari na mtaalamu wa mimea wa Italia, Prospero Alpini.

Alizaliwa mwaka 1553 na baada ya kuhitimu masomo ya tiba alitunukiwa shahada ya udaktari. Katika uchunguzi na utafiti wake, Prospero Alpini aligundua kwamba, mimea kama walivyo wanyama, ina jinsia mbili za kike na kiume japokuwa hakuweza kujua kama kanuni hiyo inahusu kila kitu.

Miongoni mwa hatua nyingine muhimu za Prospero Alpini ni kuarifisha kahawa na ndizi kwa watu wa Ulaya. Biashara ya kahawa ya Mocha au al Mukha ambalo ni jina la bandari iliyoko kusini mwa Yemen, ilikuwa mikononi mwa Waislamu tangu karne ya 15, na mtaalamu huyo wa mimea wa Italia ndiye aliwajulisha watu wa Ulaya aina hiyo ya kahawa (Arabica) iliyokuwa ikioteshwa katika maeneo ya milimani nchini Yemen.

Prospero Alpini

Siku kama ya leo miaka 101 iliyopita mkutano wa kimataifa wa kuzuia matumizi ya silaha za sumu ulimaliza kazi zake mjini Washington, Marekani kwa kutiwa saini mkataba uliopewa jina la mkataba wa pande tano kati ya nchi zilizoshiriki mkutano huo.

Nchi zilizotia saini mkataba huo ni Marekani, Ufaransa, Uingereza, Italia na Japan. Mkataba huo ulipiga marufuku utumiaji wa aina yoyote ya gesi za sumu na za kemikali katika vita. Miaka kadhaa baadaye nchi nyingine zilijiunga na mkataba huo wa kuzuia utumiaji wa gesi za sumu vitani. 

Miaka 87 iliyopita mwafaka na tarehe 6 mwezi Februari mwaka 1936 eneo lenye baridi zaidi duniani lilitambuliwa na jopo moja la kielimu baada ya kufanya juhudi za miaka minne na hatimaye kugundua eneo hilo. Kundi hilo la wataalamu hatimaye liligundua kuwa, mji wa Verkhoyansk huko Siberia, kaskazini mwa Russia, ndiyo eneo lenye baridi zaidi duniani baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu. Mji wa Verkhoyansk ulikuwa ukitumika kama makazi ya uhamishoni ya wahalifu wa kisiasa wa Russia kabla ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti. Mji huo una jamii ndogo ya watu ambao kazi yao kuu ni biashara ya ngozi na kuchimba madini. Kiwango cha joto la eneo hilo majira ya baridi hufikia daraja 70 chini ya sifuri.  *

Tarehe 6 Februari miaka 60 iliyopita aliaga dunia mwanaharakati mashuhuri na mpigania uhuru wa Morocco, Abd-el Karim Al-Khattabi. Alianzisha harakati za kupambana na wakoloni wa Kihispania na Kifaransa akiwa bado kijana na kuunda kundi la mapambano katika maeneo ya milimani nchini humo. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia Uhispania ilifanya mauaji mengi ya halaiki huko Morocco kwa ajili ya kupanua mamlaka na ushawishi wake. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na wakati wa kupamba moto mapambano ya wanamapinduzi wa Morocco, Ufaransa nayo ilifanya mauaji dhidi ya maelfu ya wananchi wa nchi hiyo.   

Abd-el Karim Al-Khattabi

Na siku kama hii ya leo miaka 44 iliyopita mamilioni ya wananchi Waislamu na wanamapinduzi wa Iran waliandamana katika miji mbalimbali hapa nchini baada ya kutangazwa serikali ya muda ya Mapinduzi.

Wananchi Waislamu wa Iran walifanya maandamano ili kuunga mkono uamuzi huo uliotolewa na Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu.

Katika siku hiyo pia wananchi wa Iran na kwa sauti moja walitaka kuondoka madarakani serikali ya Bakhtiyar ambayo ilikuwa kibaraka wa madola ya kibeberu.

Siku hiyo pia Jenerali Robert Ernest Huyser, mjumbe maalumu wa Marekani aliyekuwa Tehran kwa ajili ya kusaidia juhudi za kuubakisha madarakani utawala wa Shah Pahlavi na kutangaza uungaji mkono wa Washington kwa makamanda wa jeshi la Shah, alifunga virago na kurejea Marekani baada ya kushindwa kusitisha wimbi la Mapinduzi ya Kiislamu.   

Jenerali Robert Ernest Huyser