Feb 25, 2023 02:44 UTC
  • Jumamosi, 25 Februari, 2023

Leo ni Jumamosi tarehe 4 ya Shaaban 1444 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 25 Februari 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1418 iliyopita, yaani tarehe 4 Shaaban mwaka 26 Hijria, alizaliwa Hadhrat Abbas Bin Ali Bin Abi Talib, mashuhuri kwa lakabu ya Abul Fadhl. Mama yake ni Ummul-Banina, ambaye aliolewa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) baada ya kufariki dunia Bibi Fatima Zahra (as). Abul Fadh al-Abbas alikulia katika familia ya watu adhimu kama vile baba yake, Imam Ali (as), kaka zake Imam Hassan na Hussein na dada yake mtukufu Zaynab (as). Alimpenda sana kaka yake, Hussein Bwana wa Mashahidi kiasi kwamba alisabilia kila kitu katika ardhi ya Karbala kwa lengo la kumtetea yeye na risala yake kwa nguvu zake zote. Abbas alifahamika mno kutokana na elimu, ukweli na uchajimungu wake. Kutabahari kwake katika elimu kuliwafanya watu wengi warejee kwake kwa ajili ya kutatua masiala mbalimbali ya kielimu. Siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Abul Fadhl Abbas inajulikana hapa nchini Iran kama Siku ya Vilema wa Vita. Aidha katika siku ya kuzaliwa mtukufu huyo, watu wa Iran huwa wanawakumbuka na kuwaenzi mashujaa waliosimama imara katika vita vya kulazimishwa vya utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Iran. Kwa mnasaba huu, Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa baraka kwa Waislamu na wapigania uhuru kote duniani. ***

 

Siku kama ya leo miaka 1004 iliyopita, sawa na tarehe 4 Shaban 440 Hijiria, alifariki dunia Abu Said Abul-Khayr, mtaalamu wa elimu ya Kumjua Mwenyezi Mungu (irfan) na malenga wa Iran akiwa na umri wa miaka 83. Abu Said alizaliwa mwaka 357 Hijiria na kujifunza elimu ya hisabati na historia ya wafalme. Aidha alitabahari katika elimu za tafsiri ya Qur’ani, Hadithi na fiqhi (sheria za Kiislamu), huku akipata elimu ya irfani kutoka kwa wanazuoni mashuhuri wa elimu hiyo wa karne ya nne na ya tano Hijiria. Kitabu cha ‘Asraarut-Tawhid’ ni moja ya turathi za Abu Said Abul-Khayr. Aidha alipendelea sana kusoma mashairi. ***

Mahali lilipo kaburi la Abu Said Abul-Khayr 

 

Katika siku kama hii ya leo miaka 39 iliyopita ndege za kivita za utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein zilishambulia miji ya Saqz, Pol-e Dokhtar na Mahabad. Utawala wa Saddam Hussein uliamua kushambulia makazi ya raia katika miji mbalimbali ya Iran sambamba na ushindi mkubwa wa wapiganaji wa Kiislamu hususan katika operesheni ya jeshi la Iran iliyopewa jina la Khaibar na kipigo cha jeshi la Iraq katika visiwa vya Majnun. Makumi ya raia waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi hayo. ***

 

Tarehe 25 Februari miaka 37 iliyopita dikteta wa zamani wa Ufilipino aliyekuwa amejitangaza rais wa maisha, Ferdinand Marcos, alikimbia nchi hiyo akiwa pamoja na familia yake. Marcos alichukua hatamu za uongozi mwaka 1965. Alidumisha utawala wake wa kidikteta na ukandamizaji nchini Ufilipino kwa himaya na uungaji mkono wa nchi za Magharibi hususan Marekani. Mwaka 1973 Ferdinand Marcos alijitangaza kuwa rais wa maisha wa Ufilipino. Wakati huo wananchi katika maeneo mbalimbali walikuwa tayari wameanzisha harakati za mapambano ya kisiasa na kijeshi dhidi ya dikteta huyo. Mapambano hayo yalishika kasi zaidi katikati ya mwongo wa 1980, na Februari 25 1986 Marcos alilazimika kukimbia Ufilipino.  ***

Ferdinand Marcos

 

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita Mzayuni mmoja aliyekuwa na misimamo ya kufurutu ada aliwashambulia na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala katika Msikiti wa Haram ya Nabii Ibrahim mjini al Khalil, Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuua shahidi 29 miongoni mwao. Mauaji hayo yalitokea wakati Waislamu hao walipokuwa katika ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Waislamu wengine wengi walijeruhiwa katika shambulizi hilo la kikatili. Mauaji hayo ambayo yalidhihirisha tena uhasama na chuki za Wazayuni wa Israel dhidi ya Waislamu, yalilaaniwa na Waislamu kote duniani. Ukatili huo ulizusha wimbi kubwa la machafuko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ambapo wananchi walizidisha mapambano dhidi ya maghasibu wa Tel Aviv. Israel ilimshika kwa muda na kumuachia huru mhalifu huyo katili kwa kisingizio kwamba alikuwa punguani! ***

Mji wa al-Khalil