Feb 26, 2023 02:25 UTC
  • Jumapili 26 Februari, 2023

Leo ni Jumapili 5 ya mwezi Shaaban 1444 Hijria mwafaka na 26 Februari 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1406 iliyopita alizaliwa Imam Ali bin Hussein (AS) maarufu kwa laqabu ya Zainul Abidin katika mji mtakatifu wa Madina. Mtukufu huyo ni mwana wa Imam Hussein bin Ali Bin Abi Twalib, mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alikuwa kinara wa elimu, uchamungu, wema ukarimu na upendo. Miongoni mwa sifa kuu za Imam Zainul Abidin ni kufanya ibada na kusali Swala za usiku. Alikuwa mwingi wa ibada na alipewa laqabu ya Sajjad kwa maana ya mwenye kusujudu sana na Zainul Abidin kwa maana ya 'Pambo la Wafanya Ibada' kutokana na sijda zake ndefu katika Swala. Imam Zainul Abidin alichukua jukumu la kuendeleza ujumbe wa mapambano ya Imam Hussein ya kupambana na ufisadi na dhulma ya watawala wa Bani Umayyah baada ya kuuawa baba yake katika medani ya Karbala. Aliishi miaka 35 baada ya tukio hilo chungu na aliuawa shahidi na mtawala wa Bani Ummayah Hisham bin Abdul Malik. Athari maarufu zaidi ya mtukufu huyo ni kitabu cha dua na miongozo ya Kiislamu cha al Sahifa as Sajjadiyya. ***

 

Miaka 1131 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia tabibu na mwanakemia mtajika wa ulimwengu wa Kiislamu na mvumbuzi wa alkoholi kwa jina la Muhammad bin Zakaria Razi. Tabibu Razi alizaliwa mwaka 251 Hijria katika mji wa Rei kusini mwa Tehran ya leo. Mwanakemia huyo mkubwa alianza kujishughulisha na kazi ya usonara na baadaye kemia. Tabibu na mkemia Muhammad bin Zakaria Razi alijifunza pia elimu nyingine kama vile tiba, mantiki na falsafa. Baadae Razi alifanikiwa kutengeneza asidi ya Sulfuriki kwa kustafidi na mada asilia. Msomi huyo wa Kiislamu Muirani alikuwa shakhsia wa kwanza kuvumbua alkoholi. ***

Muhammad bin Zakaria Razi

 

Tarehe 26 Februari miaka 221 iliyopita yaani mwaka 1802 alizaliwa mshairi na mwandishi mashuhuri Mfaransa, Victor Hugo. Alikuwa akitetea uhuru na usawa kwa ajili ya matabaka ya watu wote masikini. Hugo alikubaliwa kujiunga na chuo kikuu na wakati huo huo akawa mwanachama wa Baraza la Kutunga Sheria akiwa na umri wa miaka 25. Kutokana na upinzani wake dhidi ya utawala wa ukandamizaji wa Napoeleon wa Tatu alilazimika kuachana na masuala ya siasa na akaishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 20. Katika kipindi hicho Hugo aliandika vitabu muhimu na vya thamani. Miongoni mwa vitabu hivyo ni "Watu Masikini," "The Hunchback of Notre-Dame," " The Man Who Laughs" na "Toilers of the Sea". Victor Hugo alifariki mwaka 1885. ***

 

Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita, alifariki dunia, mvumbuzi wa Marekani kwa jina la Richard Jordan Gatling. Getling alizaliwa mwaka 1818 na katika umri wake alivumbua vitu kadhaa moja wapo ikiwa ni bunduki iliyopewa jina lake ya Getling. Bunduki ya Getling ina mabomba kadhaa ambayo baada ya ufyatuaji kila moja huzunguka na kuachia risasi kwa hatua, na kuipa uwezo wa kufyatua risasi nyingi kwa wakati mmoja. Mzunguko wa mabomba hayo ulitengenezwa na Richard Jordan Gatling mwenyewe. ***

Richard Jordan Gatling

 

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, yaani mwaka 1921 kulisainiwa mkataba wa kirafiki baina ya Iran na Urusi ya zamani. Katika mkataba huo ambao ulisainiwa baada ya miaka minne ya mapinduzi ya Muungano wa Sovieti ya zamani, Moscow ilitangaza kwamba, haingeendelea na siasa za kikoloni dhidi ya Iran zilizokuwa zikifuatwa na utawala wa Tzar nchini humo. Kwa mujibu wa kifungu hicho muungano huo wa zamani uliacha kutekeleza mikataba ya awali iliyokuwa inaidhuru Iran. Katika mkataba huo wa urafiki Moscow ilitangaza kwamba haingetambua tena mikataba yote iliyotiwa saini na utawala wa tatu wa Tzar dhidi ya Iran. Hata hivyo Urusi ya zamani haikuipatia Iran ardhi za Caucasia na Turkmenistan zilizopo kaskazini magharibi na mashariki mwa Iran. Aidha katika mkataba huo Iran iliahidi kutoruhusu nchi nyingine kutumia ardhi yake dhidi ya Urusi. Itakumbukwa kuwa, Urusi kipindi hicho ilikuwa inakabiliwa na vitisho vya nchi za Magharibi. ***

Miaka 67 iliyopita siku kama ya leo mwaka 1334 Hijiria Shamsia, alifariki dunia mtaalamu wa fasihi na malenga mkubwa wa Iran, Allamah Ali-Akbar Dehkhoda. Alizaliwa mjini Tehran mwaka 1258 Hijiria Shamsia na akawa miongoni mwa wanafunzi wa awali wa chuo cha zamani cha siasa mjini Tehran. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali Dehkhoda alikwenda Ulaya na kufanya utafiti kwa miaka 5. Alirudi Iran katika kipindi cha kuchipua fikra za kupigania uhuru, kipindi ambacho alikitumia kufanya kazi za kishairi dhidi ya utawala wa wakati huo. Kazi kubwa zaidi ya msomi huyo ni kamusi maarufu ya Dehkhoda. ***

Allamah Ali-Akbar Dehkhoda

 

Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita sawa na tarehe 7 Isfand 1377 Hijria Shamsia, duru ya kwanza ya uchaguzi wa Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji ulifanyika katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa muktadha huo kukawa kumefikiwa moja ya lengo jingine miongoni mwa malengo matukufu ya taifa la Kiislamu la Iran.  Kwa kufanyika uchaguzi huo kwa hamasa, asasi na ngome ya wananchi ya Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji katika uga wa kiutawala ikawa imepata dhihirisho la kivitendo. Kuundwa Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji zaidi ya 33,000 katika maeneo mbalimbali ya Iran, ikawa ni hatua moja mbele katika uga wa kuingia na kuweko ushiriki wa wazi wa wananchi wote katika uchukuaji maamuzi ya nchi. ***

Uchaguzi wa Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji