Mar 03, 2023 02:38 UTC
  • Ijumaa, tarehe tarehe 3 Machi, 2023

Leo ni Ijumaa tarehe 10 Sha'aban 1444 Hijiria, sawa na tarehe 3 Aprili 2023.

Siku kama ya leo miaka 1022 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Iraq Abu Abdillah Abdul-Baqi, mmoja wa malenga mashuhuri wa karne ya tano Hijiria.

Mbali na kusoma kwa maulama wakubwa wa fasihi, pia alipata fursa ya kushiriki masomo ya kidini kwa maulama wakubwa wa mji huo na kuweza kustafidi  na elimu tofauti, hususan elimu ya hadithi na kadhalika.

Mashairi ya Abu Abdillah Abdul-Baqi yalikuwa ya kipekee kiusomaji mashairi na ameacha athari nyingi katika uwanja huo.

Siku kama ya leo miaka 690 iliyopita, alifariki dunia Majdud-Din Abul-Fawaaris, mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu.

Alizaliwa nchini Iraq na baada ya kuhitimu elimu ya msingi, alianza kusoma kwa maulama wakubwa na kufanikiwa kufikia daraja ya juu kielimu na kutokea kuwa mwalimu. Majdud-Din Abul-Fawaaris, alitabahari sana katika elimu za fiqhi, usulu fiqhi, hadithi, theolojia, tafsiri ya Qur'ani na fasihi ya lugha ya Kiarabu.

Kuna athari nyingi kutoka kwa msomi huyo mkubwa wa Kiislamu na mojawapo ni kitabu kinachoitwa 'Kanzul-Fawaaidi.'

Miaka 320 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Robert Hooke, mwanasayansi wa Uiingereza. Hooke alizaliwa mwaka 1635 huko kusini mwa nchi hiyo. Alifanya utafiti mbalimbali katika sayansi ya fizikia, na kutoa mchango mkubwa katika mapinduzi ya sayansi kupitia kazi zake za majaribio na nadharia.

Hooke kwa mara ya kwanza aliweza kutumia darubini yake na kutazama chembe ndogo kabisa ya kiumbe hai na kuipa jina la seli. 

Mwanasayansi huyo wa Uingereza pia alivumbua vifaa kadhaa katika taaluma ya hali ya hewa. 

Robert Hooke

Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita, utawala wa Othmaniya na Russia zilisaini mkataba katika eneo lilopewa jina la mkataba huo yaani San Stefano.

Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya utawala wa Othmaniya kushindwa na Urusi katika vita. Urusi iliuvamia utawala huo kutokana na uchu wake wa kutaka kuzidhibiti ardhi zilizokuwa chini ya himaya ya Othmaniya katika eneo la Balkan.

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopiita Kufuatia kushindwa mara kwa mara kwa vikosi vya Saddam Hussein kwenye uwanja wa vita, utawala wa Baath wa Iraq ulianza kushambulia ya mabomu dhidi ya miji mbalimbali ya iran na kulenga meli za mafuta ili kubadilisha mlinganyo wa vita kwa maslahi yake. Novemba 1984 Iraq ilitangaza rasmi kwamba italenga maeneo ya raia wa Irani. Mashambulizi hayo, mbali na kuwa na lengo la kuzidisha mashinikizo dhidi ya Iran na hivyo kupanua wigo wa vita, yaliakisi pia kushindwa stratijia ya kijeshi ya Iraq ya kuivamia Jamhuri ya Kiislamu.

Miaka 31 iliyopita katika siku kama ya leo ilifanyika kura ya maoni kwa ajili ya uhuru na kujitawala Jamhuri ya Bosnia Herzegovina. Kura hiyo ya maoni iliungwa mkono na karibu asilimia 100 ya wananchi walioshiriki katika zoezi hilo na kupelekea nchi hiyo kujitenga na Yugoslavia, baada ya Slovenia na Croatia kufanya hivyo. Jamhuri ya Bosnia Herzegovina ina ukubwa na kilomita mraba karibu 51,129 na inapakana na Croatia kwa upande wa kaskazini na magharibi, Serbia upande wa mashariki na Jamhuri ya Montenegro upande wa kusini mashariki. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka 1991, asilimia 44 ya jamii ya nchi hiyo ilikuwa ni Waislamu, jamii ambayo inaunda kundi kubwa zaidi la kidini katika jamhuri hiyo ya eneo la Balkan.

Siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, Wahindu wenye misimamo mikali walifanya mauaji makubwa dhidi ya Waislamu katika jimbo la Gujarat nchini India. Serikali ya India ilitangaza kuwa, Waislamu 790 waliuawa kwa umati katika mauaji hayo, lakini vyombo vingine huru vilisema kuwa, idadi ya Waislamu waliouawa ilikuwa ni zaidi ya 2000. Kisingizio kilichotumiwa na Wahindu kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waislamu wa Gujarat hususan katika mji wa Ahmadabad ni moto uliotokea katika gari moshi lililokuwa limebeba Wahindu lakini baadaye ilibainika kuwa, Waislamu hawakuhusika kwa njia yoyote na tukio hilo. Polisi na maafisa wa jimbo la Gujarat walishirikiana na Wahindu katika mauaji hayo dhidi ya Waislamu.