Mar 10, 2023 02:22 UTC
  • Ijumaa, tarehe 10 Machi, 2023

Leo ni ijumaa tarehe 17 Shaaban 1444 Hijria sawa na Machi 10 mwaka 2023.

Siku kama ya leo miaka 147 iliyopita mvumbuzi wa Kimarekani, Alexander Graham Bell alivumbua simu na siku hiyo hiyo akafanya mazungumzo ya kwanza ya majaribio ya simu na msaidizi wake, Thomas Watson. Uvumbuzi huo wa simu ulileta mabadiliko makubwa katika vyombo vya mawasiliano.

Bell alifaidika na uzoefu na majaribio ya wahakiki na wavumbizi wengine katika kutengeneza chombo hicho cha mawasiliano ya haraka. Baada ya hapo chombo cha simu kiliboreshwa na kufikia kiwango cha sasa kwa kukamilishwa kazi iliyofanywa na Alexander Graham Bell.

Alexander Graham Bell

Tarehe 10 Machi siku kama ya leo miaka 127 iliyopita jeshi la Italia lilishindwa vibaya katika jaribio lake la kutaka kuivamia na kuikalia kwa amabavu Uhabeshi au Ethiopia ya sasa. Lengo kuu la shambulizi hilo la Italia lilikuwa kuiungunisha Ethiopia na makoloni mengine mawili ya nchi hiyo, yaani Somalia na Eritrea. Katika vita hivyo jeshi la Italia lilipata kipigo na hasara kubwa ya hali na mali licha ya kuwa na silaha za kisasa na kulazimika kurudi nyuma.

Katika siku kama ya leo miaka 83 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Sheikh Hassanali Isfahani, arif, msomi na mwanazuoni aliyekuwa amebobea katika taaluma ya fiqhi. Alizaliwa mwaka 1279 Hijria huko Isfahan katikati mwa Iran na akaanza mapema mno kusoma elimu mbalimbali kama fiqhi, usul, mantiki na falsafa. Ayatullah Isfahani akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu, alielekea Najaf nchini Iraq na baadaye Mash’had, Iran na kubakia huko hadi mwisho wa umri wake. Ayatullah Isfahani alibobea pia katika elimu za hisabati, nujumu na tiba. Hata hivyo alikuwa mashuhuri zaidi katika baadhi ya elimu kama irfan na akhlaq. Umashuhuri mkubwa zaidi wa msomi huyo unatokana na uchamungu wake mkubwa na karama zake ambazo ni matokeo ya kujipinda katika ibada, kuitakasa nafsi na uchamungu mkubwa. Baadhi ya karama za Ayatullah Isfahani zimenukuliwa mwanaye katika kitabu alichokipa jina la "Alama za Wasio na Alama".

Sheikh Hassanali Isfahani

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ndege za kivita za Marekani zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya mji mkuu wa Japan, Tokyo. Mashambulizi hayo makubwa yalishirikisha mamia ya ndege kubwa za kurusha mabomu za Marekani zilizomimina mabomu kwa mara kadhaa katika mji mkuu wa Japan. Karibu raia laki moja wa nchi hiyo waliuawa katika mashambulizi hayo. Hata hivyo Japan haikusalimu amri hadi Mwezi Agosti mwaka huo huo wa 1945 wakati Marekani iliposhambulia kwa mabomu ya nyuklia miji ya Hiroshima na Nagasaki na kuua maelfu ya raia wasio na hatia.

Bomu la nyuklia

Katika siku kama ya leo miaka 38 iliyopita alifariki dunia Konstantin Ustinovich Chernenko, kiongozi wa zamani wa Urusi ya Zamani. Alizaliwa tarehe 24 Septemba mwaka 1911 Miladia katika familia ya kawaida na ya kijijini maeneo ya Siberia ambapo baada ya kuhitimu masomo yake na akiwa na umri wa miaka 18 alijiunga na idara ya vijana ya chama cha Ukomonisti, huku akiwa mwanachama rasmi miaka miwili baadaye. Kwa kipindi cha miaka 20 alikuwa mjumbe wa ngazi ya juu wa ofisi ya kisiasa wa chama cha Ukomonisti wa Urusi ya zamani na baada ya hapo akateuliwa kuwa katibu Mkuu. Aidha katika kipindi chote cha utawala wa Leonid Ilyich Brezhnev alikuwa akiandamana na Konstantin Ustinovich Chernenko na ni kwa ajili hiyo ndipo Wamagharibi wakamwita Chernenko kuwa ni kivuli cha Brezhnev. Baadaye alichaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo na kufanikiwa kuongoza kwa kipindi cha miezi 13 na kufariki dunia katika siku kama ya leo mwaka 1985 akiwa na umri wa miaka 74. Ni baada ya kufariki dunia ndipo akachaguliwa Mikhail Sergeyevich Gorbachev, kiongozi wa mwisho wa Urusi ya zamani.

Konstantin Ustinovich Chernenko

Katika siku kama ya leo miaka 10 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Mujtaba Musavi Lari ambaye alikuwa miongoni mwa maulama wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1314 Hijria Shamsia katika eneo la Lar nchini Iran na kupata elimu ya msingi katika eneo hilo. Mwaka 1332 alielekea Qum kwa ajili ya elimu ya juu ya Kiislamu. Huko Qum, Ayatullah Musavi Lari aliasisi Kituo cha Kueneza Maarifa ya Kiislamu Duniani ambacho kilikuwa kikisambaza vitabu vyake vilivyotarjumiwa kwa lugha hai za dunia. Mwaka 1372 Hijria Shamsia Academia ya Sayansi ya Jamhuri ya Azarbaijan ilimtunuku shahada ya uzamivu kutokana na taathira kubwa ya vitabu vyake vilivyotarjumiwa kwa lugha ya Kirusi. Ayatullah Mujtaba Lari aliaga dunia siku kama ya leo tarehe 19 Esfand katika Hospitali ya Imam Ridha (as) baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa kipindi kirefu.

Ayatullah Sayyid Mujtaba Musavi Lari