Mar 11, 2023 02:24 UTC
  • Jumamosi, 11 Machi, 2023

Leo ni Jumamosi tarehe 18 ya mwezi Shaaban 1444 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 11 Machi 2023.

Siku kama ya leo miaka 1119 iliyopita kisiwa cha Malta maarufu kama "Herini ya Mediterania" kilitwaliwa na Waislamu na kuunganishwa na mamlaka ya nchi za Kiislamu. Utawala wa Waislamu wa kisiwa cha Malta uliendelea hadi mwaka 1091 yaani hadi zama za udhibiti wa kaumu ya Norman kisiwani humo.Malta ambayo inaundwa na visiwa vingi vidogo na vikubwa ina ukubwa wa kilomita mraba 316 na jamii ya watu karibu nusu milioni. ***

 

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita, mgogoro mkubwa katika ngazi za uongozi wa Urusi ya zamani ulifikia kikomo kufuatia kutangazwa kifo cha Konstantin Chernenko na badala yake Mikhail Gorbachev ambaye wakati huo alikuwa mwanachama kijana zaidi katika Idara ya Siasa ya Chama cha Kikomunisti akatangazwa kuchukua nafasi ya Chernenko. Hatua ya kuchaguliwa Gorbachev kuongoza chama hicho cha Kikomunisti ilikwenda sambamba na kujiri mabadiliko makubwa, ambayo hatimaye yalipelekea kusambaratika Umoja wa Kisovieti. ***

Mikhail Gorbachev

 

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Haj Agha Hussein Khadimi, faqihi, alimu na mujtahidi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Ayatullah Haj Hussein Khadimi alizaliwa mjini Isfahani, Iran mwaka 1280 Hijiria Shamsia. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi na ya kati alielekea mjini Najaf, Iraq na kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Ayatullah Mirza Naini, Sayyid Abul-Hassan Isfahani na Sheikh Muhammad Jawad Balaghi. Akiwa na umri wa miaka 26 alifikia daraja ya ijtihadi ambapo baada ya kurejea mjini Isfahani alijikita na shughuli ya ufundishaji sheria za Kiislamu (fiqhi) na usulu fiqhi ambapo alikuwa na wanafunzi wengi. Katika tukio la amri ya mtawala wa wakati huo wa Iran ya kuwataka wanawake kutovaa hijabu Ayatullah Haj Agha Hussein Khadimi alitoa hotuba kali ya kupambana na utawala wa Reza Shah Pahlavi kama ambavyo pia alishiriki katika harakati mbalimbali za kupambana na njama za mkoloni Mwingereza kwa ajili ya kupora raslimali za Iran. ***

Ayatullah Haj Agha Hussein Khadimi,

 

Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita yaani mwaka 2004, watu karibu 200 waliuliwa na wengine 1000 kujeruhiwa kufuatia miripuko 5 ya mabomu iliyotokea kwenye vituo kadhaa vya treni ya chini ya ardhi (Metro) mjini Madrid, Uhispania. Miripuko hiyo inahesabiwa kuwa ni miongoni mwa vitendo vikubwa vya kigaidi kuwahi kutokea Uhispania na Ulaya tangu mwishoni mwa vita vya Pili vya Dunia. Baada ya kutokea miripuko hiyo serikali ya wakati huo nchini humo iliituhumu kundi la Eta Basque ambalo linadai kujitenga na utawala wa nchi hiyo, kwamba ndilo lililohusika na miripuko, hata hivyo kundi la Al Qaida lilitangaza kuhusika katika miripuko hiyo. Miripuko hiyo ya Machi 11 ilitokea wakati chama cha Socialist kikiwa kimeshinda katika uchaguzi wa Bunge nchini humo na kuondoka vikosi vya Uhispania nchini Iraq.

 

Na miaka 11 iliopita katika siku kama ya leo yaani Machi 11 mwaka 2011, tetemeko la ardhi lililokuwa na ukubwa daraja 9 kwa kipimo cha Rishta lililikumba eneo la Tohoku lililopo mkoa wa Miyagi Mashariki mwa Japan. Tetemeko hilo lilipelekea kuuawa kwa watu elfu 12 na malaki kadhaa ya wengine kubakia bila makazi kufuatia tetemeko hilo ambalo halijawahi kutokea mfano wake tangu makumi ya miaka yaliyopita nchini humo. Tetemeko hilo lilibomoa miundombinu, makazi ya raia na taasisi mbalimbali na kuiletea hasara ya mabilioni ya pesa nchi hiyo, kiasi kwamba kwa muda kadhaa Japan ilikuwa katika hali mbaya ya kiuchumi. Tetemeko hilo lilizua mawimbi ya Tsunami yaliyokuwa na mwinuko wa mita 15, huku mawimbi mengine madogo madogo yakizikumba nchi nyingine za jirani kufuatia tetemeko hilo. ***

Tetemeko la ardhi