Mar 15, 2023 02:21 UTC
  • Jumatano, tarehe 15 Machi, 2023

Leo ni Jumatano tarehe 22 Shaabani 1443 Hijria sawa na Machi 15 mwaka 2023.

Katika siku kama ya leo miaka 856 iliyopita alifariki dunia mfasiri, faqihi, mpokezi wa Hadithi na alimu mkubwa wa Kiislamu Ibn Shahrashub. Alizaliwa mwaka 489 katika mji wa Mazandarani ulioko kaskazini mwa Iran na kuaanza kutafuta elimu na maarifa katika kipindi cha ototoni. Bin Shahrashub alikuwa amekwishahifadhi Qur'ani nzima akiwa na umri wa miaka 8. Alipata ruhusa ya kunukuu hadithi za Mtume (saw) kutoka maulamaa wakubwa wa zama hizo kama Zamakhshari, Muhammad Ghazali na Khatib Khorazmi na alikuwa hodari katika kutunga mashairi. Moja ya mashairi yake ya kuvutia ni lile alilotunga akitaja sifa na matukufu ya Mtume Muhammad (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu. Shairi hilo linapatikana katika kitabu cha Manaqib Al Abi Twalib. Mwanazuoni huyo mkubwa ameandika vitabu vingi katika elimu za hadithi na sayansi ya Qur'ani Tukufu.

Mahali lilipo kaburi la Ibn Shahrashub 

Siku kama ya leo miaka 671 iliyopita Ibn Hajar Asqalani, faqih, mwanahadithi, mwanahistoria na mshairi Mwislamu wa Misri alizaliwa mjini Cairo Misri. Alimpoteza baba yake mzazi alipokuwa na umri wa miaka mitano tu na katika umri huo akaanza kujifunza Qur'ani Tukufu pamoja na masomo mengine ya kidini. Kufikia miaka 10 alikuwa amehifadhi Qur'ani nzima na alisafiri katika nchi tofauti kwa lego la kupata masomo ya juu. Alionyesha kipawa na ujuzi mkubwa katika taaluma ya hadithi kiasi kwamba lifahamika kwa jina la Muhifadhi Mkubwa wa Hadithi. Ibn Hajar Asqalani anahesabiwa kuwa mmoja wa waandishi mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, kwa kadiri kwamba ameandika vitabu vinavyopata 150. Miongoni mwa vitabu hivyo ni Lisaan al-Mizaan, Fat'h al-Bari fii Sharh Hadith al-Bukhari na al-Ishara fii Tamyiz as-Swahaba. Ibn Hajar al-Asqalani aliaga dunia mwaka 852 Hijiria.

Siku kama ya leo miaka 169 iliyopita alizaliwa tabibu maarufu wa Kijerumani kwa jina la Emil Adolf von Behring. Behring aliendeleza utafiti wa Louis Pastor, mwanakemia wa Kifaransa wa zama hizo katika uwanja wa kutambua na kuzuia maradhi yanayoambukiza na kupata mafanikio makubwa katika suala hilo. Mwaka 1901 Emil Adolf von Behring alitunukiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fizikia. 

Emil Adolf von Behring

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita uchaguzi wa Majlisi ya kwanza ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la kwanza la Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulifanyika hapa nchini na hivyo kutimiza moja ya malengo ya mapinduzi hayo. Kwa sasa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ina wawakilishi 290 ambao huhudumu bungeni kwa kipindi cha miaka 4. Wafuasi wa dini za waliowachache nchini Iran kama Wakristo na Wayahudi pia kwa uchache huwa na mwakilishi mmoja katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu.

Miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo, vibaraka wa madola ya kigeni walilipua bomu katika hadhara kubwa ya waumini waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya ibada muhimu ya Sala ya Ijumaa  mjini Tehran na kuwaua shahidi waumini kadhaa pamoja na kuwajeruhi wengine wengi. Sambamba na kutekelezwa kwa kitendo hicho cha kigaidi dhidi ya raia wasio na hatia, ndege za kivita za Iraq ziliruka na kuingia katika anga ya mji mkuu Tehran kama tishio la kuonyesha kwamba, mji huu ulikuwa chini ya mashambulio.

Katika siku kama hii ya leo miaka 34 iliyopita ardhi ya Taba huko kaskazini mashariki mwa Misri ilikombolewa baada ya kukaliwa kwa mabavu kwa miaka kadhaa na utawala ghasibu wa Israel. Utawala wa Kizayuni ulilikalia kwa mabavu jangwa la Sinai katika vita vya mwaka 1967, ambalo upande wa mashariki mwake linapatikana eneo la Taba. Utawala wa Tel Aviv ulikubali kuirejeshea Misri jangwa la Sinai baada ya kusaini mkataba wa Camp David mwaka 1987. Israel iliendelea kulikalia kijeshi eneo muhimu la Taba huko kaskazini mwa Ghuba ya Aqaba, licha ya utawala huo wa Kizayuni kuondoka katika baadhi ya sehemu za jangwa hilo.