Mar 18, 2023 04:06 UTC
  • Jumamosi, 18 Machi 2023

Leo ni Jumamosi 25 ya mwezi Shaaban 1444 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 18 Machi 2023 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1307 iliyopita, aliuawa kamanda wa Kiiran, Abu Muslim Khorasani, kwa amri ya Mansur, aliyekuwa mtawala wa wakati huo wa Bani Abbasi. Abu Muslim Khorasani alikuwa kiongozi wa harakati liyopewa jina la 'Siah Jamegan' huko Khorasan ambayo ilianzisha uasi dhidi ya mtawala dhalimu wa Bani Umayyah. Katika kipindi kifupi watu wengi wa vijiji na miji mingi ya Khorasan walijiunga na kundi hilo. Baada ya vita vingi Abu Muslim na wafuasi wake walifanikiwa kuwashinda watawala hao wa Bani Umayyah. Kwa utaratibu huo kuliandaliwa uwanja wa kuhitimisha kabisa utawala wa Bani Umayyah na kuingia madarakani watawala wa Bani Abbas. Katika kipindi hicho Abu Muslim Khorasani alikuwa na nafasi kubwa kiasi cha kumfanya Mansur, mtawala wa ukoo wa Bani Abbas kujawa na hofu kubwa. Kwa sababu hiyo alipanga njama ya kumuua. Baada ya mauaji hayo wafuasi wa Abu Muslim Khurasani walianzisha mapambano na kulipiza kisasi cha damu yake na mapimbano hayo yaliendelea kwa muda mrefu. ***

Abu Muslim Khorasani

 

Siku kama ya lao miaka 210 iliyopita, alizaliwa Christian Friedrich Hebbel mwanafasihi na mkosoaji mkubwa wa Ujerumani. Akiwa kijana mdogo na kutokana na kufariki dunia baba yake, alilazimika kufanya kazi katika kiwanda cha kuchapisha magazeti kwa lengo la kujidhaminia mahitaji yake. Hata hivyo baada ya kufanya tafiti kadhaa na kujiongezea maarifa, alianza kazi ya uandishi. Akiwa na umri wa miaka 20 Christian Hebbel alianza kusambaza Makala zake kwa ajili ya kuchapishwa katika magazeti ya fasihi ya mjini Hamburg, Ujerumani. Baada ya hapo alijiendeleza zaidi kielimu ambapo sambamba na kuendelea na masomo pia alikuwa akijihusisha na kazi za fasihi na kuandika michezo ya sinema mbalimbali ambapo pia katika uwanja huo ameacha athari katika uga wa fasihi na nadharia za ukosoaji. Hebbel alifariki dunia mwaka 1863 Miladia akiwa na umri wa miaka 50. ***

Christian Friedrich Hebbel

 

Miaka 165 iliyopita katika siku kama leo, alizaliwa mvumbuzi mashuhuri wa Kijerumani, Rudolf Diesel, ambaye alibuni injini ya diseli. Diesel alifanya utafiti na uhakiki mkubwa kuhusu injini za mitambo mbalimbali na akafanikiwa kuvumbua chombo ambacho kinaweza kuzalisha nishati kubwa zaidi bila ya kuhitaji umeme lakini kwa kutumia nishati ya kawaida na rahisi zaidi. Chombo hicho ambacho kilipewa jina lake mwenyewe la Diesel kilileta mabadiliko makubwa katika sekta ya viwanda na usafirishaji kwa kadiri kwamba licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia lakini injini za diseli zingalia zinatumika kwa kuwa ni zenye nguvu kubwa na zinazotumia nishati ndogo. Rudolf Diesel alifariki dunia mwaka 1913. ***

Rudolf Diesel

 

Miaka 58 iliyopita katika siku kama ya leo, mfalme Farouk wa Misri aliyekuwa ameondolewa madarakani aliaga dunia.  Mfalme Farouk alizaliwa 1920 Miladia. Alizaliwa katika kipindi ambacho baba yake yaani Ahmad Fuad alikuwa akitawala nchini Misri kwa anuani ya Fuad wa Kwanza. Farouk alichukua madaraka akiwa na umri wa miaka 16 baada ya kuaga dunia baba yakke. Hata hivyo kutokana na kutotimiza umri wa kisheria, uongozi na usimamizi wa nchi ulikabidhiwa kwa Baraza la Niaba la Ufalme. *** 

Mfalme Farouk