Alkhamisi tarehe 6 Aprili 2023
Leo ni Alkhamisi tarehe 15 Ramadhani 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 6 Aprili 2023.
Siku kama ya leo miaka 1441 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alizaliwa Imam Hassan al-Mujtaba (as), mmoja wa Ahlul-Bait wa Mtukufu Mtume (saw). Imam Hassan (as) alikulia chini ya malezi na usimamizi wa Mtume, Bibi Fatma Zahra, binti wa Mtume, na Imam Ali bin Abi Twalib (as). Baada ya kuuawa shahidi baba yake yaani Imam Ali hapo mwaka wa 40 Hijria, mtukufu huyo alifanya kazi kubwa ya kusimamia na kuwaongoza Waislamu. Mwanzoni Waislamu wengi walimbai na kumpa mkono wa utiifu Imam Hassan, lakini mfumo wa utawala wa Bani Umayyah uliokuwa ukiongozwa na Muawiya mwana wa Abu Sufiyan ambao wakati huo ulikuwa na nguvu kubwa, ulianzisha uadui na chuki dhidi ya Imam huyo. Hatimaye Imam Hassan (as) alijiandaa kukabiliana na utawala dhalimu wa Bani Umayyah, lakini viongozi wengi wa jeshi lake walidanganyika na ahadi za uongo za maadui na kumuacha peke yake, hali iliyomlazimu mtukufu huyo kufanya suluhu na mtawala huyo wa Bani Umayyah kwa lengo la kuhifadhi dini tukufu ya Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 443 iliyopita, ardhi ya Ureno, moja kati ya nchi zilizokuwa na nguvu barani Ulaya katika karne za 15 na 16 iliunganishwa na Uhispania. Ureno ilikuwa mpinzani wa kisiasa na kikoloni wa Uhispania huko Asia, Afrika na Marekani. Hata hivyo kutokana na raia wa nchi hiyo kuhamia kwa wingi katika nchi makoloni ya Ureno na vile vile hali mbaya ya kiuchumi taratibu Ureno ilianza kupoteza satwa na nguvu yake ya kisasa. Udhaifu na kutokuwa na nguvu Ureno uliipelekea Uhispania kuivamia nchi hiyo. Pamoja na hayo yote hatimaye mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Ureno ya mwaka 1640 yalipelekea kukombolewa tena nchi hiyo.

Miaka 106 iliyopita katika siku kama ya leo, serikali ya Marekani ilitangaza vita dhidi ya Ujerumani na ikaingia katika Vita vya Kwanza vya Dunia kwa maslahi ya Waitifaki. Tab'an kabla ya hatua hiyo, Marekani ilikuwa imekata uhusiano wake wa kisiasa na Ujerumani na ilikuwa ikizisaidia nchi Waitifaki.

Miaka 38 iliyopita katika siku kama hii ya leo Ja'far Nimeiry, Rais wa zamani wa Sudan alipinduliwa na Jenerali Abdulrahman Swarul Dhahab aliyekuwa Waziri wa Ulinzi ambaye alichukua madaraka ya kuiongoza Sudan. Ni vyema kuashiria hapa kuwa Nimeiry pia aliingia madarakani kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea Sudan mwaka 1969. Nimeiry aliongoza Sudan kimabavu kwa miaka 16 na kuanzisha uhusiano mkubwa kati ya nchi hiyo na Marekani.
Katika siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, Wahutu wenye misimamo mikali wa Rwanda walianzisha mauaji makubwa dhidi ya Watutsi. Katika mauaji hayo Wahutu wenye misimamo mikali waliwauwa raia wa Kitutsi na Wahutu wenye misimamo ya wastani karibu milioni moja na kuwafanya mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Wahutu wanaunda asilimia 84 ya jamii ya Rwanda na kabila hilo lilikuwa madarakani hadi mwaka 1994.
