Jumatano, 12 Aprili, 2023
Leo ni Jumatano tarehe 21 Ramadhani 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 12 Aprili 2023.
Siku kama ya leo miaka 1404 iliyopita Ali bin Abi Talib AS wasii wa Mtume Muhammad (saw) na mmoja wa Ahlul Bait wa Mtume, aliuawa shahidi. Siku mbili kabla ya kifo chake, Imam Ali bin Abi Twalib alipigwa upanga kichwani na mmoja wa Khawarij wakati alipokuwa katika sijda akimwabudu Mwenyezi Mungu msikitini katika Swala ya Alfajiri. Siku kama ya leo Imam Ali (as) aliaga dunia kutokana na majeraha makubwa aliyopata na hivyo kufikia matarajio yake makubwa ambayo alikuwa akiyatamani daima, yaani kuuliwa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu SW. Kuuawa shahidi Imam Ali bin Abi Twalib (as) kulikuwa msiba mkubwa na usioweza kufidika kwa Uislamu na Waislamu.
Imam Ali (as) aliwausia wanawe na Waislamu akisema: "Nawausia kumcha Mungu na kuwa na taratibu nzuri katika mambo yenu. Wajalini yatima na muwafanyie mema majirani zenu, kwani nilimsikia Mtume wa Allah (saw) akiusia kuwafanyia mema jirani hadi nikadhani atawarithisha. Shikamaneni na Qur'ani na msiache watu wengine wawatangulie mbele katika kutekeleza mafundisho yake. Itukuzeni Swala kwani ndiyo nguzo ya dini yenu.." Sala na salamu za Allah jiwe juu ya Imam Ali bin Abi Twalib na Aali zake watoharifu.
Tarehe 21 Ramadhani miaka 340 iliyopita alifariki dunia faqihi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Sheikh Abu Jaafar Muhammad bin Hassan maarufu kwa jina la Sheikh Hurr al Aamili huko Jabal Amil nchini Lebanon. Alitokea kuwa miongoni mwa maulama na watafiti wakubwa wa Kiislamu. Sheikh Hurr al Amili ameandika vitabu vingi vya fiqhi na Hadithi na miongoni mwavyo ni kile cha Wasaailu Shia ambacho kina nafasi maalumu katika duru za elimu ya fiqhi.
Siku kama ya leo miaka 203 iliyopita sawa na tarehe 12 Aprili 1820, dawa ya kutibu ugonjwa wa malaria iligundulika kutoka kwenye magamba ya mti wa Cinchona. Asili ya mti huu wenye majani ya kijani kibichi ni maeneo ya Amerika ya Kusini lakini hii leo unapandwa katika ameneo mengine ya dunia. Utomvu wa mti huu hutumika kutengeneza dawa chungu sana ya Quinine. Tarehe 12 Aprili mwaka 1820 kwa mara ya kwanza kabisa madaktari Pierre Joseph Pelletier na Joseph Bienaimé Caventou wa Ufaransa walifanyia majaribio dawa hiyo ya malaria katika Maabara ya Paris na kukaanza jitihada za kuzalisha dawa ya Quinine.
Siku kama ya leo miaka 200 iliyopita, sawa na tarehe 12 Aprili 1823, alizaliwa Alexandr Ostrovsky mwandishi wa tamthilia wa nchini Russia. Alihitimu masomo ya sheria katika chuo kikuu ingawa aliamua kujiunga na tasnia ya uandishi wa tamthilia na uigizaji. Karibu kila mwaka Alexandr Ostrovsky alikuwa akifanya uigizaji wa kihistoria au kuandika vichekesho ambapo alikuwa akiakisi hali halisi ya jamii. Alikuwa na taathira kubwa katika senema ya Russia. Miongoni mwa athari za mwanasanaa huyo ni pamoja na 'Binti wa Barafu', 'Msitu' 'Tufani' na 'Muhanga Mwingine.' Mwandishi huyo alifariki dunia mwaka 1886.
Siku kama ya leo miaka 156 iliyopita, sawa na tarehe 12 Aprili 1867, Mutsuhito, mfalme maarufu na mwanamageuzi wa Japan aliingia madarakani nchini humo. Mfalme huyo aliingia madarakani wakati ambapo Japan ilikuwa inakabiliwa na changamoto nyingi za udhaifu katika nyuga tofauti. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Mutsuhito baada ya mwaka mmoja kuingia madarakani akabuni mapinduzi ya kijamii na kuanzisha mageuzi nchini Japan. Katika uwanja huo alihamisha mji mkuu kutoka Kyoto kwenya Tokyo sambamba na kubadili katiba ya nchi hiyo. Hata kama utawala wa Mutsuhito ulifikia tamati mwaka 1912, lakini Japan iliweza kupata maendeleo licha ya kuliibuka vita baina yake na China na Russia.
Katika siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, kwa mara ya kwanza mwanadamu alifika katika anga za mbali na kuizunguka dunia. Siku hiyo Yuri Gagarin mwanaanga wa Urusi ya zamani aliyekuwa na umri wa miaka 27 aliizunguka dunia kwa dakika 89 kwa kutumia chombo cha anga za mbali kwa jina la Vastok 1 na kwa msingi huo kukapatikana mafanikio makubwa katika sekta ya masuala ya anga. Gagarin alifariki dunia akiwa pamoja na mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa sekta ya masuala ya anga wa Urusi ya zamani katika ajali ya ndege hapo mwaka 1968.
Na siku kama hii ya leo miaka 31 iliyopita, Muhsin Saba mwalimu na mwandishi wa zama hizi wa Kiirani alifariki dunia. Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi katika shule ya Darul Funun alielekea nchini Ufaransa. Alirejea nchini Iran baada ya kupata shahada ya uzamivu (PhD) na kuanza kufundisha. Dakta Muhsin Saba aliasisi Kundi la Taifa la Utambuzi wa Vitabu. Aidha hakuwa nyuma pia katika kutunga na kuandika vitabu.