Apr 14, 2023 02:14 UTC
  • Ijumaa Aprili 14 mwaka 2023

Leo ni Ijumaa tarehe 23 Ramadhani 1444 Hijria sawa na Aprili 14 mwaka 2023.

Siku kama ya leo tarehe 14 Aprili miaka 897 iliyopita alizaliwa Ibn Rushd, mwanafalsafa na mwanafikra maarufu wa Kiislamu wa Andalusia (sehemu ya Uhispania ya sasa). Baba na babu wa Ibn Rushd, wote walikuwa makadhi huko Andalusia. Akiwa kijana alipata kusoma elimu mbalimbali za zama zake na kuutabahari zaidi katika elimu za hisabati, sayansi, nyota, mantiki, falsafa na udaktari. Kufuatia hali hiyo alipewa kipaumbele na watawala wa silsila ya Muwahhidun waliokuwa wakitawala Andalusia wakati huo, na kuteuliwa kuwa kadhi wa wa Córdoba, mji mkuu wa Andalusia. Hata hivyo mwishoni mwa umri wake alichukiwa na watawala na hatimaye akapelekwa uhamishoni. Mielekeo ya Ibn Rushd ilielemea sana kwenye fikra za Aristotle. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na ‘Tahaafut al-Tahafat’ ‘Kitabul-Kulliyyaat’ katika taaluma ya tiba na ‘Faslul-Maqaal.’ Ibn Rushd alifariki dunia Disemba 1198 sawa na mwezi Swafar 595 Hijiria.

Ibn Rushd

Siku kama ya leo miaka 190 iliyopita, ilikamilika kazi ya uandishi wa kitabu cha ‘Jawaahirul-Kalaam’ ambacho kimejumuisha masuala muhimu ya sheria za Mwenyezi Mungu juu ya halali na haramu na kadhalika sheria mbalimbali za dini ya Kiislamu. Ni vyema kuashiria kuwa, kitabu cha Jawaahirul-Kalaam kimebainisha kwa undani masuala mengi ya sheria kiasi kwamba hadi sasa hakuna msomi aliyeweza kuandika kitabu kama hicho. Kunukuu kauli za wasomi wakubwa wa sheria za Kiislamu na kuzitolea ushahidi kwa umakini wa hali ya juu, ni kati ya nukta zinazopatikana katika kitabu hicho. Ayatullah Muhammad Hassan Najafi, mtunzi wa kitabu hicho, alianza kazi ya uandishi wa kitabu cha Jawaahirul-Kalaam akiwa na umri wa miaka 25 na alitumia karibu muda wa miaka 30 katika uandishi wake na kupewqa lakabu ya ‘Sheikhul-Fuqahaa.’ Kipindi cha maisha yake kulitawaliwa na hujuma za fikra potofu za genge la Uwahabi na watu wa kundi la Ikhbariyyun suala ambalo lilimfanya Ayatullah Muhammad Hassan Najafi kuelezea umuhimu wa kuwa na kiongozi wa Umma wa Kiislamu. Ni baada ya hapo ndipo kukazaliwa fikra ya kuwepo waliyyu Faqihi ‘walii kiongozi anayesimamia masuala ya sheria za Kiislamu. 

Ayatullah Muhammad Hassan Najafi

Siku kama ya leo miaka 177 iliyopita alizaliwa Friedrich Carl Andreas, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) na Iran huko nchini Ujerumani. Baada ya kufahamiana na mtaalamu mmoja wa masuala ya mashariki wa nchini Denmark, alivutiwa sana na utamaduni wa Iran ambapo alianza kufanya utafiti kwa kipindi cha miaka minne katika uwanja huo. Katika kukamilisha masomo yake aliamua kutembelea nchi za Iran na India sambamba na kujifunza lugha ya Kifarsi. Kwa karibu kipindi cha miaka 30 alikuwa mwalimu wa lugha ya Kifarsi katika Chuo Kikuu cha Göttingen nchini Ujerumani ambapo wanafunzi wake walipata kufahamu tamaduni za thamani za Iran. Mtaalamu huyo wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Ujerumani alifariki dunia mwaka 1930.

Friedrich Carl Andreas

Siku kama hii ya leo miaka 133 iliyopita muungano wa Pan American ambao baadaye ulibadili jina na kujulikana kama Jumuiya ya Nchi za Amerika uliasisiwa. Nchi wanachama wa jumuiya hiyo zilikuwa zikishirikiana katika nyanja mbalimbali hadi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Hata hivyo baada ya vita hivyo kumalizika Jumuiya ya Nchi za Amerika iliundwa kutokana na kuweko haja ya kupanuliwa zaidi mashirikiano kati ya nchi hizo. Pamoja na hayo yote kitu kinachoitia wasiwasi jumuiya hiyo ni satwa na ushawishi mkubwa wa Marekani katika jumuiya hiyo na hatua yake ya kukitumia vibaya chombo hicho kwa maslahi yake ya kisiasa. Kwa sababu hiyo nchi wanachama zinafanya jitihada kubwa za kupunguza ushawishi wa Marekani katika jumuiya hiyo.

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita yaani tarehe 23 Ramadhani mwaka 1392 Hijria Qamaria, Allamah Muhammad Hussein Tabatabai mwanafalsafa, arifu na faqihi mkubwa wa Kiirani alikamilisha kazi ya uandishi wa tafsiri kubwa na ya aina yake ya Qur’ani ya al Mizan. Tafsiri hiyo ya Qur’ani ni moja kati ya tafsiri kubwa na makini sana za Qur’ani Tukufu na iliandikwa katika kipindi cha karibu miaka 20. Sifa kubwa zaidi ya tafsiri hiyo ni kwamba imefasiri aya za Qur’ani kwa msaada wa aya nyingine za kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Tafsiri hiyo kubwa na adhimu iliandikwa na Allamah Tabatabai kwa lugha ya Kiarabu na hadi sasa imetarjumiwa kwa lugha mbalimbali kama Kifarsi, Kiingereza na Kihispania. 

Allamah Muhammad Hussein Tabatabai

Tarehe 25 Farvardin miaka 35 iliyopita serikali ya wakati huo ya Iraq ilikiri kwamba ilitumia silaha za kemikali katika vita vyake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kipindi chote cha miaka minane ya vita hivyo Iran iliwasilisha mashtaka katika jumuiya za kimataifa kwamba Iraq inatumia silaha za kemikali dhidi ya wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu. Wakati huo Iraq haikukiri wala kukadhibisha habari hiyo. Hata hivyo katika siku kama hii ya leo wakati vita vilipokuwa vimepamba moto, serikali ya Baghdad ilikiri kwamba inatumia silaha za kemikali zikiwemo za gesi ya sumu na hatari ya haradali dhidi ya malengo ya kijeshi na kiraia ya Iran. 

 

Takwimu zimeonesha kwamba utawala wa Baath wa Iraq ulifanya mashambulizi 3,500  kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi chote cha vita hivyo. 

Miaka 21 iliyopita katika siku kama leo, Hugo Chavez rais wa zamani wa Venezuela alirejea nchini kwake na kushika hatamu za uongozi baada ya kufeli jaribio la mapinduzi ya kumuondoa madarakani. Chavez Aliingia madarakani mwaka 1999 na kufanya mabadiliko makubwa kwa maslahi ya tabaka la chini. Vilevile alichukua hatua za kusimamia mashirika ya mafuta ya Kimarekani yaliyokuwa yakichimba mafuta ya nchi hiyo. Siasa za kujitegemea za Chavez ziliikasirisha sana Washington. Ni kwa sababu hiyo, ndiyo maana Marekani ilipanga na kuratibu mapinduzi mnamo tarehe 12 Machi mwaka 2002. Licha ya mapinduzi hayo kupata mafanikio katika hatua za awali, lakini wananchi wa Venezuela waliokuwa wameridhishwa na mabadiliko ya Chavez, walipinga uingiliaji wa nchi za nje katika masuala ya ndani ya nchi yao. Hugo Chavez alifariki dunia Machi 5 mwaka 2013 kutokana na maradhi ya saratani akiwa na umri wa miaka 58.

Hugo Chavez