Hikma za Nahjul Balagha (14)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 14 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi.
مَنْ ضَیَّعَهُ الاْقْرَبُ أُتِیحَ لَهُ الاْبْعَدُ
Aliyetelekezwa na jamaa zake, watu wa mbali hutumia fursa kumsaidia.
Sifa mojawapo ya familia zilizofanikiwa ni kwamba watu wote wa familia hiyo kamwe hawatupani. Wanajua kwamba tatizo lolote linalotokea kwa mmoja wao linahusiana na familia nzima. Kwa hivyo, huwa wanahakikisha wanamsaidia kikamilifu mwenzao huyo samamba na kuchunga mipaka yake binafsi. Lakini wakati mwingine katika familia, hutokea baadhi ya mambo yasiyofaa na kupelekea mtu kukataliwa, kutelekezwa na kufukuzwa kwenye familia.
Katika hikma hii ya 14 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anampa faraja na matumaini aliyetupwa na familia ambaye jamaa zake wa karibu hawampendi na wametelekeza kwa kumwambia asikate tamaa kwa sababu Mwenyezi Mungu yupo na atamfungulia njia nyingine. Imamu Ali AS hapa anasema: "Mwenye kutupwa na kutelekezwa na jamaa zake, ajue kuwa watu wa mbali wapo kwa ajili ya kumlinda na kumsaidia." Tab'an hapa Imam hakukusudia kuchochea watu wafanye maovu katika familia, mpaka watu wa familia washiindwe kumvumilia na walazimike kumfukuza.
Kwa hakika ni hikma na kanuni ya Mwenyezi Mungu kwamba watu wanapaswa kuungwa mkono na kusaidiwa na ndugu, marafiki na jamaa zao wa karibu. Lakini ikiwa watu hao hawatotekeleza majukumu yao, na kuipa mgongo rehema na wajibu wa kuunga udugu na urafiki, Mwenyezi Mungu anasema, atawakabidhi wengine jukumu hilo na kwamba hawezi kumwacha mja wake peke yake katika dhoruba za matukio mbalimbali ya kwenye maisha.
Kwa mfano, kabila la Kkiquraishi, ambalo lilichukuliwa kuwa ni jamaa wa karibu zaidi wa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW), walimvunjia heshima na kumfukuza mtukufu huyo. Walimfukuza Makkah na kumlazimisha kuishi kwenye bonde la Shib Abi Talib. Walimwekea vikwazo vikubwa mno vya kiuchumi na kupiga marukufu kuenezwa fikra na mafundisho yake kwa njia yoyote iwezekanayo. Lakini Menyezi Mungu aliyatia hima makabila ya mbali zaidi ya Aus na Khazraj kutoka mji wa Yathrib yaani Madina na wakamnusuru na kumlinda kwa udhati wa moyo wao.
Makabila hayo ya Aus na Khazraj yalimuunga mkono Mtume katika kila halii, wakaupigania Uislamu kikamifu na hatimaye wakamuwezesha Mtume Mtukufu wa Uislamu kurejea Makkah alikofukuzwa na kabila lake na kuukomboa mji huo mtukufu katika ushindi mkubwa uliojaa fakhari. Mtume alirejea Makkah, akavunja masanamu yote yaliyokuwemo kwenye Al Kaaba na kuutoharisha mji huo na washirikisha wa Kiquraish na akapeperusha juu bendera ya tawhid iliyoeneo katika kona zote za dunia hadi leo hii.