May 24, 2023 09:08 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 883 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 41 ya Fuss’ilat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 45 ya sura hiyo ambayo inasema:

‏ وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ فَاخْتُلِفَ فِيهِ ۗ وَلَوْلَا كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِن رَّبِّكَ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ ۚ وَإِنَّهُمْ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ مُرِيبٍ

Na hakika tulimpa Musa Kitabu, lakini kukahitilafiwa kwacho. Na lau kuwa halikwisha tangulia neno la Mola wako Mlezi wangeli hukumiwa. Na hakika wao wamo katika shaka yenye kuwatia wasiwasi.

Katika darsa iliyopita tulisoma aya iliyozungumzia visingizio walivyokuwa wakitoa washirikina wa Makka kwa kumwambia Bwana Mtume SAW ya kwamba: Kwa kuwa hii Qur’ani yako imeteremshwa kwa lugha ya Kiarabu, basi haiwezi kuwa muujiza; kama utaweza kutuletea kitabu kwa lugha nyingine, hapo ndio utakuwa umefanya muujiza! Aya hii tuliyosoma inamhutubu Bwana Mtume ya kwamba: Katika zama za Nabii Musa AS pia, kaumu ya Bani Israil nayo pia ilikuwa ikitoa visingizio kama hivi; na watu wake wakahitilafiana kuhusu ukweli wa Taurati. Lakini takdiri ya Mwenyezi Mungu si kuwaadhibu makafiri papo hapo, kwa sababu kuwaharakishia adhabu hakuendani na rehma zake, vyenginevyo adhabu yake Mola ingewashukia haraka makafiri papa hapa duniani. Ama kuhusu kuitilia shaka Qur’ani kunakofanywa na washirikina, utiaji shaka huo si wa hali ya kawaida ya maumbile ya kibinadamu, unaofanywa na watu kwa kutaka kuondoa shaka waliyonayo na kubaini ukweli kwa kulichunguza na kulihakiki jambo; shaka yao wao imechanganyika na mtazamo hasi na dhana mbaya. Wao kila siku wanatoa kauli tatanishi na kutoa kisingizio hiki na kile ili kuwafanya watu wengine wasisilimu na kuiamini haki. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, kutokana na rehma za Mwenyezi Mungu, makafiri na wafanyamadhambi wanapewa muhula kwa mantiki kwamba, huenda wakatubia na kuachana na mwenendo wa upotovu. Kama isingekuwa hivyo, kila mtu angeadhibiwa pale pale anapokufuru au kufanya dhambi, ukawa ndio mwisho wa maisha yake hapa duniani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, shaka ni daraja la kumvukisha mtu ili kuufikia ukweli na hakika ya jambo. Shaka inapasa iwe utangulizi wa suali wa kugundua na kubaini ukweli, na si wenzo wa kujengea dhana mbaya na kuukanusha ukweli huo!

Ifuatayo sasa ni aya ya 46 ambayo inasema:

مَّنْ عَمِلَ صَالِحًا فَلِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ أَسَاءَ فَعَلَيْهَا ۗ وَمَا رَبُّكَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ

Anaye tenda mema basi anajitendea mwenyewe nafsi yake, na mwenye kutenda uovu basi ni juu ya nafsi yake vile vile; wala Mola wako Mlezi si mwenye kuwadhulumu waja. 

Baada ya aya iliyotangulia kuzungumzia kaida na kanuni aliyoiweka Allah kuhusu makafiri, aya hii inaashiria kanuni nyingine ambayo kimsingi ndiyo kanuni na kaida kuu kuhusiana na amali za wanadamu; nayo ni kwamba, kila anayefanya amali njema, ni kwa manufaa ya nafsi yake, na kila mwenye kutenda mabaya, amehasirisha nafsi yake mwenyewe. Kwa maneno mengine ni kwamba, malipo ya thawabu na adhabu atakayopata kila mtu yatalingana na amali zake; na kila mtu atachuma matunda mazuri au mabaya yatakayotokana na mbegu za amali zake, kwa sababu Allah SWT katu hawadhulumu waja wake. Nukta nyingine ni kwamba, katika jamii za wanadamu, mfumo wa utoaji adhabu au malipo mazuri unafanywa kwa kuzingatia uwiyano kati ya kosa analofanya mtu na adhabu anayostahiki kupewa na huwa katika sura ya majimui ya kanuni maalumu zilizopangwa na watu wenyewe. Lakini mfumo wa hukumu za adhabu na thawabu wa Mwenyezi Mungu si wa namna hiyo ya upangaji kanuni bali umejengeka katika sura ya uhusiano wa amali na athari au radiamali yake, ambalo ni jambo linalothibiti katika dhahiri na uhalisia wa kimaumbile. Kwa kutoa mfano ni kwamba, ikiwa mtu ataamua kwa kujua kula chakula kibaya au kilichoharibika, ataumwa na kupata machungu na maumivu makali. Machungu na maumivu hayo ni adhabu ya chakula kibaya alichoamua kula na wala hawezi kumlaumu mtu yeyote kwa yaliyomsibu. Hapana shaka kuwa, ukafiri na ufanyaji madhambi una taathira na matokeo hasi kwa roho na akili ya mtu. Athari hizo hapa duniani hudhihiri kwa namna tofauti, ambazo kwa hakika ni adhabu za duniani za madhambi. Na huko akhera pia athari ya dhambi kwa roho na nafsi ya mtu itadhihirika kwa sura ya adhabu ya moto wa Jahanamu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, madamu tuna hiari, irada na haki ya kuchagua katika matendo tunayofanya, hatuwezi kumbebesha mtu yeyote dhima ya athari za matendo yetu hayo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, tusiihusishe na Mwenyezi Mungu misiba na masaibu yanayotupata maishani, kwa sababu kimsingi Allah SWT hamdhulumu yeyote katika waja wake. Masaibu mengi yatupatayo ni matokeo ya amali zetu wenyewe.

Tunaihitimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 47 na 48 ambazo zinasema:

إِلَيْهِ يُرَدُّ عِلْمُ السَّاعَةِ ۚ وَمَا تَخْرُجُ مِن ثَمَرَاتٍ مِّنْ أَكْمَامِهَا وَمَا تَحْمِلُ مِنْ أُنثَىٰ وَلَا تَضَعُ إِلَّا بِعِلْمِهِ ۚ وَيَوْمَ يُنَادِيهِمْ أَيْنَ شُرَكَائِي قَالُوا آذَنَّاكَ مَا مِنَّا مِن شَهِيدٍ

UJUZI wa kuijua Saa ya Kiyama unarudishwa kwake tu Mwenyezi Mungu. Na matunda hayatoki katika mafumba yake, wala mwanamke hachukui mimba, wala hazai, ila kwa kujua kwake. Na siku atakayo waita, akawaambia: Wako wapi washirika wangu? Hapo watasema: Tunakiri kwako ya kwamba hapana miongoni mwetu anaye shuhudia hayo. 

‏ وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَدْعُونَ مِن قَبْلُ ۖ وَظَنُّوا مَا لَهُم مِّن مَّحِيصٍ

Na wakawapotea wale walio kuwa wakiwaomba hapo kwanza, na wakawa na yakini kuwa hawana pa kukimbilia. 

Baada ya aya iliyotangulia kueleza kwamba, Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja wake katika kutoa malipo ya thawabu au adhabu, aya hizi tulizosoma zinasema, hakuna mtu yeyote ajuaye wakati wa kusimama Kiyama na yatakayojiri huko; na kwamba mjuzi wa hilo ni Yeye Mola Muumba. Hata kama Allah SWT amewaeleza watu baadhi ya habari zinazohusu Siku ya Kiyama kupitia Mitume wake, pamoja na hayo, siri za ulimwengu huo wa akhera zimefichikana katika elimu ya mwanadamu. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba, si siri za Kiyama pekee, lakini hata siri nyingi za ulimwengu huu pia ambazo nyinyi wanadamu hamzijui, ziko wazi kabisa kwa Yeye Allah SWT. Mfano wake ni kila tunda liotalo kwa kuchomoza na kuchanua kokwa na ganda lake na binadamu au mnyama jike abebaye mimba akafika hatua ya kujifungua, yote hayo yanajiri kwa ujuzi, utambuzi na hekima ya Mola Muumba. Kisha aya zinazungumzia washirikina wanaokanusha Kiyama na kueleza kwamba, watakaposimamishwa mbele ya mahakama ya siku hiyo, watu hao wataulizwa: viko wapi vitu na watu mliowadhania kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu, mkawa mnawategemea wao; waiteni leo basi waje wakuokoeni! Watu hao hawatokuwa na jibu la kutoa ghairi ya kusema, sisi hatuna ushahidi wowote wa kutetea kauli zetu na tuliyokuwa tukiyaamini. Leo tumefahamu kwamba, yale tuliyokuwa tukiyanena yalikuwa batili yasiyo na msingi wowote. Wakiwa katika hali hiyo, watu hao watashuhudia kwa macho yao kwamba waliokuwa wakiwaabudu na kuwadhania washirika wa Allah na wenye uwezo wa kuwasaidia wao katika wakati mgumu na wa masaibu, hakuna athari yao yoyote, bali wote wametoweka na kuangamia mbele ya macho yao. Itawadhihirikia wazi kuwa hakuna popote pa kupatia hifadhi wala pa kukimbilia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kutojua wakati wa Kiyama si hoja ya kukanusha kujiri kwake. Ni kama ulivyo wakati wa kujiri baadhi ya mambo mengine ambayo sisi hatuna ujuzi nao, lakini tuna hakika kuwa yatatokea tu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, elimu na ujuzi wa Allah hauhusiani na ulimwengu kwa ujumla wake tu, bali hata mambo madogo madogo kabisa ambayo wanadamu hawayajui au wameghafilika nayo, kwake Yeye Mola yanajulikana kwa uwazi kabisa. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, hapa duniani tusiwafuate watu ambao Siku ya Kiyama hawatakuwa na uwezo wowote wa kutusaidia. Siku hiyo washirikina wataungama na kutangaza kadamnasi kuwa, si wao wala maabudu wao waliokuwa wakiwatii na kuwafuata, wanao uwezo wa kufanya lolote. Vile vile aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa, katika mahakama ya Siku ya Kiyama, haki itadhihiri kwa namna ambayo, ubatilifu na kutokuwa na maana yoyote waabudiwa wote batili kutadhihirika na kubainika wazi. Wakati huo, waliomshirikisha Allah watatambua kwamba waliyaharibu maisha yao ya duniani na kuuvuruga mustakabali wao wa akhera. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 883 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atughufirie madhambi yetu, atukubalie dua zetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/