Sura ya Al-Ah'qaaf, aya ya 15-18 (Darsa ya 924)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 924 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 46 ya al Ah'qaaf. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 15 ya sura hiyo ambayo inasema:
وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ إِحْسَانًا ۖ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ كُرْهًا وَوَضَعَتْهُ كُرْهًا ۖ وَحَمْلُهُ وَفِصَالُهُ ثَلَاثُونَ شَهْرًا ۚ حَتَّىٰ إِذَا بَلَغَ أَشُدَّهُ وَبَلَغَ أَرْبَعِينَ سَنَةً قَالَ رَبِّ أَوْزِعْنِي أَنْ أَشْكُرَ نِعْمَتَكَ الَّتِي أَنْعَمْتَ عَلَيَّ وَعَلَىٰ وَالِدَيَّ وَأَنْ أَعْمَلَ صَالِحًا تَرْضَاهُ وَأَصْلِحْ لِي فِي ذُرِّيَّتِي ۖ إِنِّي تُبْتُ إِلَيْكَ وَإِنِّي مِنَ الْمُسْلِمِينَ
Na tumemuusia mwanadamu awatendee wema wazazi wake wawili. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu. Na kuchukua mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini. Hata anapo fika utu uzima wake, na akafikilia miaka arubaini, husema: Mola wangu Mlezi! Niwezeshe nishukuru neema zako ulizo nineemesha mimi na wazazi wangu, na nitende mema unayo yaridhia. Na unitengenezee dhuriya zangu. Hakika mimi nimetubu kwako, na mimi ni miongoni mwa Waislamu.
Moja ya sifa muhimu zaidi ilizonazo dini tukufu ya Uislamu ni kuyapa uzito na umuhimu masuala ya familia. Na ndio maana kuna aya kadha wa kadha za Qur'ani, Hadithi na hukumu za dini zinazozungumzia na kutilia mkazo juu ya suala hilo. Kuusiwa watu kufunga ndoa na kuanzisha familia, kuwepo uhusiano wa kuhurumiana na uliotawaliwa na huba, mapenzi na kusameheana baina ya mke na mume ndani ya ndoa na familia yao, kuzaa watoto na kuwapa malezi mema na sahihi, kubainisha njia bora na mwafaka za kutatua tofauti zinazojitokeza ndani ya ndoa pamoja na utaratibu wa talaka na kuachana inapofikia hatua ya lazima kufanya hivyo, ni maudhui kuu ambazo zimejadiliwa na kuzungumziwa na aya mbalimbali za Qur'ani tukufu. Aya hii tuliyosoma, imeanza kwa kuashiria usia wa Mwenyezi Mungu kwa watu wote, wakiwemo waumini na wasio waumini. Katika sehemu moja ya aya hii zimegusiwa baadhi tu ya tabu na mateso, ambayo wazazi, na hasa akina mama, wanayahimili kuanzia katika ubebaji mimba hadi kwenye malezi na makuzi ya watoto wao, ili watu wawe na huruma na unyenyekevu kwa mama zao pamoja na kuwathamini na kuwa washukurivu kwao. Kwa masikitiko ni kwamba, katika dunia yetu ya leo, ambayo inashajiisha zaidi ubinafsi na watu kujali na kufikiria zaidi matakwa na matashi ya nafsi zao, takwimu za ufungaji ndoa na uanzishaji familia zinazidi kupungua. Na hata watu wanaoamua kuoana, huwa wanatosheka kuwa na watoto wachache tu. Kuendelea kwa mwenendo huu, kumepelekea kupungua idadi ya watu katika nchi zilizoendelea; na jamii za nchi hizo kuwa na idadi kubwa ya wazee. Katika utamaduni wa dini, mtu anayetimiza umri wa miaka arubaini huwa kwa hakika amefikia kilele cha ukomavu na ukamilifu wa kimwili na kiakili. Na kwa kawaida, mtu kama huyo, huwa tayari ana familia na watoto. Lakini kuwa na hayo, kusiwe sababu ya kumghafilisha na wazazi wake bali inampasa aendelee kuwatendea zaidi na zaidi wema na ihsani. Ni wazi kuwa wema, ni mpana zaidi ya utoaji kitu; na wala haukomei katika msaada wa kifedha tu. Kwani si hasha wakawepo wazazi ambao hawana shida yoyote ya fedha, lakini wakawa na kiu kubwa ya mapenzi, kujaliwa na kushughulikiwa na watoto wao. Au kutokana na kuzeeka, wakawa wanahitaji matunzo; na pale inapolazimu wakahitajia uuguzi na matibabu, ambayo yote hayo yanajumuishwa katika neno wema na ihsani. Pamoja na hayo, kuwashughulikia mtu wazazi wake kusimghafilishe na jukumu la kuwafikiria na kuwashughulikia pia mke na watoto wake. Na ndio maana sehemu inayofuatia ya aya inaashiria suala la kuwa wema watoto na kizazi cha mtu, ili iweze kufahamika kwamba, mbali na kuomba dua kwa Mwenyezi Mungu, zinahitajika pia bidii na juhudi za mtawalia za wazazi, za kuwapa malezi bora na mema zaidi watoto wao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, moja ya haki ambazo kila mzazi anayo kwa mtoto wake ni kutendewa wema katika uhai wake wote. Ihsani na wema ambao mtoto ana wajibu wa kuwatendea wazazi wake, unatakiwa uwe wa kudumu na endelevu, si wa nyakati maalumu au itokeapo shida na dharura tu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, suala la kuwatendea wema wazazi halishurutishwi na wao kuwa Waislamu. Uislamu unaliusia suala hilo kwa mtazamo wa kiutu, si wa kiimani. Aidha aya hii inatutaka tujue kwamba, japokuwa ni wajibu kuwatendea wema wazazi wote wawili, lakini kutokana na tabu na mateso ambayo mama anayapata katika kipindi cha ujauzito, kujifungua na unyonyeshaji, yeye ana haki maalumu kwa mtoto; na inapasa mapenzi na wema anaofanyiwa yeye uwe mkubwa zaidi. Halikadhalika aya hii inatuelimisha kuwa, kukumbuka tabu na mateso waliyopata akina mama, kuna taathira ya kuwafanya watoto wawe na hisia za huruma, upole na upendo kwao. Vilevile aya hii inatutaka tufahamu kwamba, kuwaombea dua na kuwatumikia wazazi, sambamba na kuwaombea dua watoto na kuwapa malezi mema ni miongoni mwa mambo ambayo Allah SWT amewausia wanadamu wote.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 16 ambayo inasema:
أُولَٰئِكَ الَّذِينَ نَتَقَبَّلُ عَنْهُمْ أَحْسَنَ مَا عَمِلُوا وَنَتَجَاوَزُ عَن سَيِّئَاتِهِمْ فِي أَصْحَابِ الْجَنَّةِ ۖ وَعْدَ الصِّدْقِ الَّذِي كَانُوا يُوعَدُونَ
Hao ndio tunaowatakabalia vitendo vyao bora walivyotenda, na tunayasamehe makosa yao. Watakuwa miongoni mwa watu wa Peponi. Miadi ya kweli hiyo waliyo ahidiwa.
Baada ya aya iliyotangulia kuzungumzia usia wa Mwenyezi Mungu kwa watu kuhusiana na wazazi wao pamoja na watoto wao, aya hii tuliyosoma inataja malipo watakayopata watu wanaoutekeleza usia huo muhimu wa Mwenyezi Mungu na kuufanya dira na mwongozo wa maisha yao, na kubainisha kwamba, Allah SWT ameahidi kuwaingiza peponi watu hao wema; na nani aliye mkweli zaidi ya Yeye Mola katika kutekeleza ahadi anazotoa? Bila shaka sharti la mtu kuingia peponi ni kusafika na kutu na uchafu wa madhambi, kwa hivyo Allah SWT atawasamehe waja wema makosa yao na kuzipokea kwa namna bora kabisa amali zao njema na za kheri walizofanya. Na hizo ni rehma na ukarimu mkubwa kabisa wa Mwenyezi Mungu kwa watendao mema, kwani atawalipa thawabu chungu nzima kwa kila jema moja walilofanya. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, thamani ya amali yoyote ni kutakabaliwa, si kutimiza wajibu wa kuifanya tu; hapana shaka yoyote, amali itakayokubaliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni ile iliyokidhi masharti na kufanywa kwa namna bora kabisa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kuwatendea wema na ihsani wazazi ni msingi wa mtu kutakabaliwa amali zake njema na kupata maghufira na msamaha wa Mola. Wa aidha aya hii inatuelimisha kwamba, mtu anayewatumikia wazazi wake, hasa mama, huwa kwa hakika amejifungulia njia ya kuingia peponi.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 17 na 18 za sura yetu ya al Ah'qaaf ambazo zinasema:
وَالَّذِي قَالَ لِوَالِدَيْهِ أُفٍّ لَّكُمَا أَتَعِدَانِنِي أَنْ أُخْرَجَ وَقَدْ خَلَتِ الْقُرُونُ مِن قَبْلِي وَهُمَا يَسْتَغِيثَانِ اللَّهَ وَيْلَكَ آمِنْ إِنَّ وَعْدَ اللَّهِ حَقٌّ فَيَقُولُ مَا هَٰذَا إِلَّا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ
Na ambaye amewaambia wazazi wake: Ah! Nanyi! Ati ndio mnanitisha kuwa nitafufuliwa, na hali vizazi vingi vimekwisha pita kabla yangu! Na hao wazazi humwomba msaada Mwenyezi Mungu (na humwambia mtoto wao): Ole wako! Amini! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kweli. Na yeye husema: Hayakuwa haya ila ni ngano za watu wa kale.
أُولَٰئِكَ الَّذِينَ حَقَّ عَلَيْهِمُ الْقَوْلُ فِي أُمَمٍ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِم مِّنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ ۖ إِنَّهُمْ كَانُوا خَاسِرِينَ
Hao ndio ambao imehakikikishwa hukumu juu yao kama mataifa yaliyo kwisha pita kabla yao miongoni mwa majini na watu. Hakika hao wamekuwa wenye kukhasirika.
Mkabala na watoto wema wanaowathamini na kuwatumikia wazazi wao, katika baadhi ya familia hukulia na kuinukia watoto wabaya na waovu, ambao huwataabisha na kuwadhikisha wazazi wao na kuzisononesha nyoyo zao kwa ujuba na maneno machafu wanayowatolea. Sio tu hawachungi haki za wazazi, lakini hawako tayari kufuata hata malezi ya kidini pia wanayopewa. Pale wazazi wao wanapowalingania kumwabudu Mwenyezi Mungu, watu hao huzifanyia shere na stihzai imani na itikadi za dini na kuthubutu hata kutamka kuwa, ahadi zilizotolewa na Mitume wa Mwenyezi Mungu ni uongo mtupu. Ni wazi kwamba hatima na mwisho wa watu kama hao walio watovu wa shukurani na wapigavita dini ni kuingia kwenye kundi la madhalimu na wafanya madhambi wa kaumu zilizopita. Hao watapatwa na ghadhabu na adhabu ya Mwenyezi Mungu; mwisho mbaya na mchungu unawangojea; na hawatakuwa na pa kukimbilia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, baadhi ya watoto hupotoka wakaikengeuka njia ya haki na uongofu. Lakini jukumu la wazazi kwao, si kuwaapiza na kuwatelekeza, bali ni kuwaombea dua na kuendelea kuwalingania njia ya haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wazazi wana wajibu na masuulia ya kuwafunza na kuwaelimisha watoto wao; na inapasa wafanye juhudi za kuwalea kidini na kuwajenga kiroho hata kama jitihada na bidii wanazofanya hazitakuwa na tija. Wa aidha aya hizi zinatuelimisha kwamba, mtu anayepuuza imani juu ya Mwenyezi Mungu na kufufuliwa, huwa hawajali wazazi wake, hudharau haki zao na hata yumkini akasimama dhidi yao. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 924 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe taufiki ya kupata radhi za wazazi wetu, na atupe mwisho mwema sisi na vizazi vyetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/