May 27, 2023 05:40 UTC
  • Sura ya Fat-h, aya ya 22-25 (Darsa ya 942)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 942 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 48 ya Al Fat-h. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 22 na 23 za sura hiyo ambazo zinasema:

وَلَوْ قَاتَلَكُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوَلَّوُا الْأَدْبَارَ ثُمَّ لَا يَجِدُونَ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا

Na lau makafiri wangeli pigana nanyi basi bila ya shaka wangeli geuza migongo (wakakimbia), kisha wasingeli pata mlinzi wala msaidizi.

سُنَّةَ اللَّهِ الَّتِي قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلُ ۖ وَلَن تَجِدَ لِسُنَّةِ اللَّهِ تَبْدِيلًا

Huo ndio utaratibu wa Mwenyezi Mungu uliokwishatangulia zamani, wala hutapata mabadiliko katika utaratibu wa Mwenyezi Mungu. 

Katika darsa kadhaa zilizopita tumesoma aya zilizozungumzia Sulhu ya Hudaibiya, eneo lililoko karibu na mji wa Makka, suluhu ambayo ilifikiwa kati ya Bwana Mtume Muhammad SAW na wakuu wa washirikina wa mji huo. Baadhi ya watu walikuwa wakitoa maneno ya dharau kumwambia Bwana Mtume na masahaba zake kwamba, nyinyi ni madhaifu na hamna uwezo wa kufanya lolote, ndio maana mmeridhia kufanya suluhu kama hii; na laiti kama vingetokea vita, basi mngeshindwa tu. Ndipo aya tulizosoma zikateremshwa kuwajibu watu hao na kuwapa moyo Waislamu; na vilevile kusisitiza kwamba, maneno hayo yasemwayo na watu hao si sahihi na hayana msingi wowote. Kimsingi ni kwamba, kila pale waumini wanapoingia kwenye medani ya mapambano ya Jihadi, wakawa wanafanya hivyo kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu tu huku wakitii na kufuata amri na maelekezo ya Mtume wake, na si kwa makusudio ya kupata manufaa ya vitu, wala wao wenyewe kuwa na tofauti na mifarakano, basi utaratibu na kanuni ya kudumu aliyoiweka Allah ni kuwapa auni na msaada wake waumini hao dhidi ya maadui zao. Na hilo lilithibitika kivitendo katika vita vya Badr na Ahzab, ambapo kwa msaada na nusura ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, kundi dogo la waumini liliweza kuyashinda majeshi makubwa mno ya washirikina na makafiri. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, mtu anayemkanusha Mwenyezi Mungu, huwa kwa hakika amejikosesha msaada na ulinzi wa Allah katika maisha yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuiwezesha haki kushinda dhidi ya batili na kuwasaidia waumini katika kukabiliana na makafiri ni miongoni mwa kanuni thabiti na za uhakika alizoweka Allah SWT. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, kanuni za Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kamilifu na zinavuka mipaka ya mahala na zama. Na ndio maana kupita muda hakuzifanyi zichakae wala zionekane zimepitwa na wakati na pia hakuzifanyi zipoteze ubora na ufanisi wake.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 24 na 25 za sura yetu ya al-Fat-h ambazo zinasema:

وَهُوَ الَّذِي كَفَّ أَيْدِيَهُمْ عَنكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ عَنْهُم بِبَطْنِ مَكَّةَ مِن بَعْدِ أَنْ أَظْفَرَكُمْ عَلَيْهِمْ ۚ وَكَانَ اللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرًا

Na Yeye ndiye aliyeizuia mikono yao kwenu, na mikono yenu kwao, katika bonde la Makka baada ya kukupeni Ushindi juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona myatendayo.

هُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوكُمْ عَنِ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَالْهَدْيَ مَعْكُوفًا أَن يَبْلُغَ مَحِلَّهُ ۚ وَلَوْلَا رِجَالٌ مُّؤْمِنُونَ وَنِسَاءٌ مُّؤْمِنَاتٌ لَّمْ تَعْلَمُوهُمْ أَن تَطَئُوهُمْ فَتُصِيبَكُم مِّنْهُم مَّعَرَّةٌ بِغَيْرِ عِلْمٍ ۖ لِّيُدْخِلَ اللَّهُ فِي رَحْمَتِهِ مَن يَشَاءُ ۚ لَوْ تَزَيَّلُوا لَعَذَّبْنَا الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا

Hao ndio walio kufuru na wakakuzuieni msiingie Msikiti Mtakatifu, na wakawazuilia dhabihu kufika mahala pao pa kuchinjwa. Na lau si wanaume Waumini na wanawake Waumini msio wajua mkawasaga na mkaingia makosani kutokana nao bila ya kujua ...Mwenyezi Mungu (amefanya haya) ili amuingize amtakaye katika rehema yake. Lau wangeli pambanuka bila ya shaka tungeli waadhibu walio kufuru kwa adhabu iumizayo. 

Aya hizi zinaendeleza maudhui iliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kwa kugusia nukta mbili muhimu kuhusiana na Suluhu ya Hudaibiya. Nukta ya kwanza ni kwamba, suluhu hiyo, hakika yake ilikuwa ushindi kwenu nyinyi dhidi ya washirikina; ushindi ambao ulipatikana bila vita na umwagaji damu. Sababu ni kwamba, nyinyi mlikuwa katika ardhi yao na kwa hivyo washirikina wangeliweza kukuangamizeni; lakini baada ya nyinyi kumpa baia' na mkono wa utiifu Mtume, woga na hofu vilitanda ndani ya nyoyo za makureishi mpaka wao wenyewe wakaamua kutoa pendekezo la kufanya suluhu. Ama nukta ya pili ni kuwa, huko Makka walikuwepo baadhi ya Waislamu waliokuwa wakiishi katika mji huo, ambao kwa sababu mbalimbali hawakuhajiri kuelekea Madina. Kama Mwenyezi Mungu angetoa amri ya kuushambulia mji wa Makka, maisha ya Waislamu hao pia yangekuwa hatarini, kwa sababu nyinyi mlikuwa hamuwajui na kwa hivyo mngepambana nao. Kwa kufanya hivyo mngejitia dola la majuto ya kudumu kwamba mliwashambulia au hata kuwaua Waislamu wenzenu katika mji wa Makka. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kwamba, baadhi ya wakati suluhu huwa ishara ya ushindi. Tab'an, hilo huweza kutambuliwa na viongozi weledi na waumini pale watakapohisi kwamba kufanya suluhu ni kwa maslaha ya jamii ya Kiislamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wakati wowote maadui wanapoamua kukomesha vita, huwa haifai sisi kuanzisha tena vita na mapigano dhidi yao. Wa aidha tunabainikiwa kutokana na aya hizi kwamba, Makka haiwahusu wakazi wa mji huo peke yao; na hakuna yeyote awezaye kuwazuia waumini wasiingie ndani ya mji huo kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Vilevile tunajielimisha kutokana na aya hizi kuwa, wakati wa vita na mapigano, tujitahidi kadiri iwezekanavyo kuepusha kuuawa watu wasio na hatia; na tujue kwamba, hatuna mamlaka na hiari ya kufanya mambo ndivyo sivyo au lolote lile tutakalo, kwa sababu tu ya kupata ushindi dhidi ya adui. Halikadhalika aya hizi zinatutaka tujichunge na kuchukua hadhari ya kutompa adui kisingizio. Kuna udharura wa kujiepusha na hatua yoyote ile itakayowatia doa Waislamu, kuwafanya wasemwe kwa ubaya na kuchafua sura na haiba yao ndani ya jamii. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 942 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe taufiki ya kuyatekeleza yote aliyotuamrisha na atuwezeshe kuyaepuka yote aliyotukataza. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/