Jun 17, 2023 06:44 UTC
  • Hekaya za Aya (1)

Assalam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Hamjambo na karibuni kuwa nasi katika sehemu ya kwanza ya kipindi chetu kipya tulichokipa jina la Hekaya za Aya ambacho kwa hakika kinazungumzia sababu, kisa au tukio lililopelekea kuteremshwa Aya mbalimbali za Qur'ani Tukufu.

Qur'ani ni kitabu cha maisha ambacho kiritemshwa na Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake Muhammad (saw) taratibu na kwa muda mrefu ili kuwaongoza wanaadamu. Baadhi ya Aya za kitabu hicho ziliteremshwa kwa nyakati tofauti na kwa kuzingatia matukio yaliyojiri wakati wa uhai wa Mtume Mtukufu. Kwa kuwa ni vigumu na wakati mwingine ni muhali kuzifasiri Aya za Qur'ani bila kuzingatia kisa na sababu ya kuteremshwa kwake, tumetayarisha kipindi hiki cha “Hekaya za Aya” ili kuwa na ufahamu mzuri zaidi wa neno la Mwenyezi Mungu, yaani Qur'ani Tukufu. ****

Tunachagua kisa cha kwanza kutoka kwenye Sura ya "Al Insan". Sura hii imepewa jina la Insan kwa maana ya "mtu au binadamu" kwa sababu mhimili wake mkuu ni mwanaadamu, matendo yake, ikhlasi, kujitolea, na hatima ya kazi na amali zake Siku ya Kiyama. Sura hii pia inajulikana kwa majina ya "Hal Ataa" na "Dahr", ambayo yote yamechukuliwa kutoka kwenye Aya ya kwanza ya sura hii, kama ilivyo kwa jina la Insan. Aya hiyo inasema:

هَلْ أَتَى عَلَى الإِنسَانِ حِینٌ مِّنَ الدَّهْرِ لَمْ یَکُن شَیْئًا مَّذْکُورًا

Je, kilimpitia binadamu kipindi katika zama ambacho hakuwa kitu kinachotajwa? Na kwa kuwa Aya nyingi za Sura hii zinazungumzia sifa za watu wema, "Abrar", sura pia imepewa jina la Abrar.                           

Hassan na Hussein (as), wajukuu wapendwa wa Mtume Muhammad (saw), walikuwa bado wachanga na wakijishughulisha na michezo ya kipindi kitamu cha utotoni. Kila mara Mtume alipopita mbele ya nyumba ya Ali bin Abi Twalib (as) kwa ajili ya Swala, watoto wake wawili, Hassan na Hussein, walikuwa wakimkimbilia na kumkaribisha kwa hatua ndogo za kitoto, na Mtume (saw) alikuwa akiwakumbatia na kuwabusu, wote wawili. 

Siku moja watoto hao wawili walipatwa na maradhi, na mama yao, Fatima binti Muhammad (saw) akawa anawahudumia na kuwauguza. Mtume (saw) alikwenda nyumbani kwa binti yake, Fatima kuwatembelea na aliguswa sana kuona nyuso zenye homa za maua hayo mawili yenye harufu nzuri, yaani Hassan na Hussein. Alimwambia Ali (as) kwamba: “Ingekuwa vyema kama ungeweka nadhiri kwa ajili ya shifaa ya watoto wako”! Kutokana na pendekezo hili la Mtume, Ali bin Abi Twalib, alisema hapohapo kwamba: “Mola wangu! Watoto wangu wakipona na kupata shifaa, nitafunga Saumu siku tatu." Bibi Fatima (as) naye pia aliweka nadhiri kwa njia hiyo hiyo. Hassan na Hussein (as) pia walifuata nyayo za wazazi wao na kuweka nadhiri licha ya umri wao mdogo. Fedha, hadimu na mtumishi wao pia aliweka nadhiri ya kuomba shifaa ya Hassan na Hussein.

Muda si mrefu wajukuu wawili wa Mtume (saw) walipata shifaa na kuondokewa na homa; hivyo watu wa familia hiyo waliamua kuanza kutekeleza nadhiri yao. Ali (as) alitayarisha shayiri kwa ajili ya kufuturu katika siku tatu za kufunga Saumu ya nadhiri; akasaga shayiri hiyo na kutengeneza unga na kuugawa katika sehemu tatu. Sehemu moja aliikanda kwa ajili ya kuoka mkate wa siku ya kwanza ya funga, na akatayarisha mkate wa shayiri kwa idadi ya watu waliofunga.

Wakati wa futari ulipowadia, ilisikika sauti kutoka nyuma ya mlango wa nyumba hiyo ya Ali na Fatima. Mtu mmoja aliita kutoka nyuma ya mlango akisema: "Amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya familia ya Mtume. Mimi ni maskini nina njaa sana, naomba chakula. Mwenyezi Mungu akutunukuni chakula cha peponi."

Watu wote waliokuwa ndani ya nyumba hiyo walikuwa na njaa baada ya funga ya Saumu ya siku nzima. Hawakuwa na chochote isipokuwa futari ya tende na mkate kidogo. Hata hivyo watu wa familia hiyo ambao walikuwa maarufu kwa ukarimu na kimbilio la wenye haja na mafukara, walitoa chakula chao cha futari kwa masikini huyo. Usiku huo walilala na njaa bila ya kufuturu chochote.

Siku iliyofuata, wakati wa kufuturu, mlango wa nyumba uligongwa. Mtu mmoja aliwasalimia watu wa familia na kusema: "Mimi ni yatima, nina njaa sana, nisaidieni." Wakati huo, Ali bin Abi Twalib (as), ambaye ni mashuhuri kwa jina la "Baba wa Mayatima na Masikini", alinyoosha mkono na kuchukua sehemu yake kutoka kwenye meza ya Iftar, akampa yatima aliyeomba msaada. Wanafamilia wengine wa nyumba hiyo tukufu pia walitoa fungu lao kwa yatima huyo, kama alivyofanya baba wa familia.

Jioni ya siku ya tatu, ilitarajiwa kwamba wangeondokana na maumivu ya njaa kwa kula chakula kidogo wakati wa futari; mara wakasikia sauti iliyowasalimia watu wa nyumba hiyo. "Assalamu Alaykum. Mimi ni mateka, niko hoi. Ni mgeni katika mji huu, na sina mwenyeji. Nina njaa, nisaidieni!" Walichukua chakula chao cha mkate wa shayiri na kumpa mateka kwa upendo, heshima na taadhima. Kwa utaratibu huo wakawa wametimiza nadhiri yao ya kufunga Saumu siku tatu. ****       

Asubuhi ya siku iliyofuata, Mtume (saw) alipokwenda nyumbani kwa Ali bin Abi Twalib (as) alihuzunika sana kuziona nyuso zao zilizodhoofishwa na njaa. Wakati huo, Malaika Jibril aliteremka na kumpongeza Mtume (SAW) kwa niaba ya Mwenyezi Mungu kwa kuwa na familia yenye imani kubwa kama hiyo na kisha akamsomea Aya za Suratul Insan zinazosema: 

یُوفُونَ بِالنَّذْرِ وَیَخَافُونَ یَوْمًا کَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِیرًا. وَیُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَى حُبِّهِ مِسْکِینًا وَیَتِیمًا وَأَسِیرًا. إِنَّمَا نُطْعِمُکُمْ لِوَجْهِ اللَّهِ لا نُرِیدُ مِنکُمْ جَزَاء وَلا شُکُورًا

(Hakika watu wema) wanatimiza nadhiri, na wanaiogopa siku ambayo shari yake inaenea. Na huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini na yatima, na mateka. Hakika sisi tunakulisheni kwa wajihi wa Mwenyezi Mungu tu, hatutaki kwenu malipo wala shukrani. 

Tukio hili lilitokea tarehe 25 Dhul-Qaada mwaka wa 6 au 7 Hijiria. Imamu Hassan na Imamu Hussein (as) walikuwa watoto wadogo wakati huo. Hii inaonyesha kwamba, maimamu hawa wawili watukufu (as) licha ya kuwa maasumu, lakini pia walikuwa wamefikia ukomavu wa kidini na kiibada utotoni mwao. Kwa sababu hiyo, wazazi wao hawakuwakataza kuweka na kutekeleza nadhiri hiyo; kwa maana kwamba, watukufu hawa walikuwa tayari kiakili, kinafsi, kimwili na kimaarifa kukubali amri za Mwenyezi Mungu SW.  *****

Kwa mujibu wa Hadithi nyingi zinazopatikana katika vyanzo vya Hadithi vya Waislamu wa madhehebu zote mbili kubwa za Shia na Suni, Sura hii ya Insan iliteremshwa kuwaenzi Ahlul Bait (as) na kubakisha hai tukio hili. Mwanazuoni mtajika, Allamah Abdul Hussein Amini amewataja wanavyuoni 34 wa Kisuni katika kitabu chake cha Al-Ghadir, ambao wanasimulia kisa maarufu cha nadhiri ya watukufu hao na ukarimu wao mkubwa. Hekaya na kisa chetu cha leo pia kimethibitishwa na kusimuliwa na wanazuoni  wa madhehebu nyingi za Kiislamu. Muhammad bin Idris al Shafi' imamu wa madhehebu ya Shafi' ametunga mashairi yafuatayo akienzi tukio hili adhimu. Amesema: 

إلامَ إلامَ وحَتّى مَتى           اُعاتَبُ فی حُبِّ هذَا الفَتى ؟

وهَل زُوِّجَت فاطِمٌ غَیرَهُ      وفی غَیرِهِ هَل أتى  «هَلْ أَتَى»

"Ni kwa muda gani, kwa muda gani na hadi lini nitalaumiwa kwa kumpenda kijana huyu (Ali)?" Je, kuna yeyote aliyeozwa Fatimah isipokuwa yeye? Je, Sura ya Hal Ataa iliteremshwa kuhusu mtu mwingine asiye yeye?

"Abdul Baqi al Omari al Farooqi", mmoja wa washairi mashuhuri wa karne ya 13 na miongoni mwa waandishi wakubwa wa fasihi wa Iraq wakati wa utawala wa Kiothmani (Ottoman Empire), ameandika shairi akisema:

وسایل هل اتی نص بحق علی *** اجبته (هل اتی) نص بحق علیِ

فظننی اذغدا متی الجواب له *** عین السؤال صدی من صفحة الجبلٍ

ومادری لادری جدا و لاهزلاً *** انی بذاک اردت الجد با الهزل

"Muulizaji aliuliza: Je! Imeteremshwa Aya kwa heshima ya Ali?" * Nikajibu: "Hal Ataa ni maandishi ya Mungu juu ya wema wake."

Alipoona kwamba jibu langu, * * lilikuwa sawa na swali lake katika lafudhi, alidhani kwamba ulikua mwangwi wa suti ya mlima.

Hakujua kabisa kwamba sikuwa natania; * * Badala yake, nilisema ukweli katika jibu lake."

Vilevile mshairi Ibn Maatuq wa Misri anasema katika tungo zake za kuwasifu Ahubaiti wa Mtume Muhammad (saw) kwamba:

سل الحوامیم هل فی غیرهم نزلت ** و هل أتی، هل أتی الا بمدحهم؟

Uliza, je (sura zinazoanza na) Haamim ziliteremshwa kuhusu wasiokuwa Ahlul-Bait (as)? Na je, Sura ya Hal Ataa haikuteremshwa kuwasifu wao?

Mpenzi msoma, Sura "Hal Ataa" au baadhi ya Aya zake zilizoteremshwa kusifu na kupongeza kazi na amali adhimu na kubwa ya kujitolea Ahlul-Bait (as) ni miongoni mwa heshima na fadhila zao kuu. Naam, sifa zilizotajwa katika Aya hizo pia zinawahusu watu wote wema wanaosabilia kila walichonacho kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu SW. Imamu Sadiq (as) anaeleza adhama ya Sura ya "Hal Ataa" na ukweli kwamba iliteremshwa kuhusu kujitea kwa Imam Ali, Fatima, Fidha, Haasan na Hussein (a.s.) na kusema: "Aya hizi pia zinamhusu kila muumini anayefanya mema haya katika njia ya Mwenyezi Mungu." Kwa maneno mengine ni kwamba, mtu yeyote anayetimiza nadhiri na agano lake takatifu, na kuacha au kutoa kile anachokipenda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, anaweza kuwekwa kwenye safu za "Abrar" na watu wema. Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 92 ya Suratu Aal-Imran kwamba:

لَنْ تَنالُوا الْبِرَّ حَتَّى تُنْفِقُوا مِمَّا تُحِبُّونَ وَ ما تُنْفِقُوا مِنْ شَیْ‏ءٍ فَإِنَّ اللَّهَ بِهِ عَلیمٌ

"Hamtapata wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda. Na kitu chochote mnachokitoa basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua." Kwa hiyo, kilicho muhimu mbele ya Mwenyezi Mungu, ni ubora wa amali na matendo na si wingi na ukubwa wake.  VVV

Kama unavyojua, wakati mwingine watu hutoa walichonacho kwa sababu za huruma. Wakati mwingine hutoa kwa ajili ya kutekeleza wajibu na pengine kwa sababu ya kuogopa adhabu au kwa tamaa ya kuingia peponi. Wakati mwingine mwanaadamu hutoa alichonacho akitarajia shukrani au kusifiwa na upande mwingine. Yumkini pia mwanaadamu akatoa sadaka na mali yake wakati anapokuwa na utajiri mkubwa kiasi kwamba, kutoa huku hakupunguzi lolote katika mali na milki yake. Lakini wakati mwingine amali hiyo hufanyika wakati mtu anapokuwa katika shida na akiwa yeye mwenyewe ni mhitaji na fakiri, tena anafanya wema huo kwa watu ambao si marafiki na waumini wenzake pekee, bali wakati mwingine kwa maadui.

Wema na kilichotolewa na Ali bin Abi Twalib na familia yake hakikuwa kikubwa sana kwa vigezo, idadi na mizani ya kimaada. Lakini kwa kuwa amali hiyo ilifanyika kwa ajili ya Wajihi wa Mwenyezi Mungu na kupata radhi Zake, kama inavyosema Aya: إِنَّما نُطْعِمُکُمْ لِوَجْهِ اللّهِ لا نُرِیدُ مِنْکُمْ جَزاءً وَ لا شُکُوراً:

"Hakika tunakulisheni kwa ajili ya wajihi wa Mwenyezi Mungu, hatutaki malipo wala shukrani kutoka kwenu", hawakuwa na matarajio ya kushukuriwa au kusifiwa na watu. Na kwa upande mwingine pamoja na kuwa wao wenyewe walikihitajia chakula hicho, waliwatanguliza waliokuwa na haja na njaa licha ya kuwa hawakuwa hata Waislamuu. Kwa msingi huo Sura hii ya Hal Ataa iliteremshwa kubakisha hai tukio hili adhimu ili liwe kigezo na ruwaza njema ya kuigwa na wanaadamu wa mahali na zama zote.   

Tags