Jumatatu, 17 Julai, 2023
Leo ni Jumatatu tarehe 28 Mfunguo Tatu, Dhulhija 1444 Hijria, sawa na tarehe 17 Julai mwaka 2023 .
Siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita, sawa na tarehe 28 Dhulhija mwaka 63 Hijiria, yaani miaka miwili baada ya harakati na mapambano ya mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) yaani Imam Hussein bin Ali (AS) katika ardhi ya Karbala hapo mwaka 61 Hijria, kulijiri tukio la Harrah. Mwaka huo watu wa mji mtukufu wa Madina waliokuwa wamechoshwa na dhulma na ukatili wa mtawala Yazid bin Muawiya, walimfukuza gavana wake mjini humo Marwan bin al Hakam. Baada ya tukio hilo Yazid alituma jeshi likiongozwa na mtumishi wake mmwaga damu na mtenda dhulma Muslim bin Uqbah katika mji mtakatifu wa Madina na kuliamuru kufanya mauaji makubwa mjini humo na kupora mali. Mauaji kama hayo hayakuwahi kushuhudiwa katika historia ya zama za awali za Uislamu na wanahistoria wamesema kuwa Waislamu zaidi ya elfu kumi wakiwemo maswahaba wa Mtume, waliuawa katika shambulizi hilo. Vitabu vya historia pia vinasema utawala wa Yazid bin Muawiya ulihalalisha mji wa Madina kwa askari wake kwa muda wa siku tatu na kwamba wasichana na wanawake wa maswahaba walinajisiwa katika tukio hilo.

Siku kama ya leo miaka 155 iliyopita, alifariki dunia Mulla Hadi Sabzavari mmoja wa maulama na wanafalsafa wakubwa wa karne ya 13 Hijria.
Mulla Hadi Sabzavari alizaliwa mwaka 1212 Hijria na alitumiwa umri wake ulijaa baraka katika zuhdi na uchamungu. Athari za Mulla Hadi Sabzavari zinaonyesha kwamba, alimu huyo mkubwa wa Kiislamu mbali na kwamba alikuwa mmoja wa wanafalsafa wakubwa, pia alitabahari katika uwanja wa elimu ya sheria za Kiislamu (fiq'hi), tafsiri ya Qur'ani, mantiki, hisabati, fasihi na elimu ya tiba.
Aidha Mulla Hadi Sabzavari mbali na kufikia daraja za juu za kielimu, alikuwa pia malenga. Katika uwanja huo, alikuwa akitunga mashairi na tungo za elimu ya falsafa na irfani. Allamah Iqbal Lahore, malenga na mwanafalsafa mkubwa wa Pakistan, anasema kuhusiana na Mulla Hadi Sabzavari kuwa: "Mulla Hadi Sabzavari ni mmoja wa wanafikra wakubwa nchini Iran na falsafa yake imechanganyika sana na dini."
Miongoni mwa athari za mwazuoni huyo ni pamoja na 'Mandhumah' katika uwanja wa elimu ya mantiki, 'Asraarul-Hikam' na 'al-Jabru Wal-Ikhtiyaar.'

Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita Profesa Roger Garaudy, mwanafalsafa na mwanafikra wa Ufaransa alizaliwa huko katika mji wa Marseille. Garaudy alipata shahada ya udaktari katika taaluma tatu za masomo ya falsafa, fasihi na utamaduni. Roger Garaudy alifungwa jela katika kambi ya mateka wa kivita wa Ujerumani tangu mwaka 1940 hadi 1943 kutokana na mapambano yake dhidi ya ufashisti wa Adolph Hitler wakati Ufaransa ilipokaliwa kwa mabavu na Ujerumani. Profesa Garaudy alikuwa mwanachama wa chama cha Kikomonisti cha Ufaransa kwa miaka 36 na pia mwanachama wa kamati kuu ya chama hicho kwa miaka 25. Hata hivyo mitazamo ya kikomunisti na kiliberali haikuweza kukata kiu ya kutafuta ukweli ya msomi huyo wa Ufaransa na hatimaye alikubali dini ya tukufu ya Uislamu baada ya kufanya utafiti mkubwa. Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka 1979 ulikuwa na taathira kubwa katika mitazamo ya Profesa Roger Garaudy.

Katika siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, chama cha Baath cha Iraq kilichukua hatamu za uongozi kupitia mapinduzi yaliyoongozwa na Ahmad Hassan al-Bakr na kumpindua Rais Abdulrahman Aarif. Baada ya kuchukua madaraka chama cha Baath, Saddam Hussein ambaye alikuwa kiongozi nambari mbili wa chama hicho alianza kuwauwa wapinzani wake nchini Iraq na vikosi vya usalama na vya jeshi la nchi hiyo pia vikaanzisha hujuma kali dhidi ya wapinzani wa Kikurdi, wazalendo, wanaharakati wa Kiislamu na hata Wakomonisti.

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilianza rasmi kazi zake. Baraza hilo liliundwa kwa mujibu wa kipengee namba moja cha Katiba ya Iran kwa shabaha ya kulinda Sharia za Kiislamu na Katiba na kuhakikisha kwamba sheria zote zinazopasishwa hapa nchini hazipingani na viwili hivyo. Baraza hilo linaundwa na wataalamu 6 wa elimu ya fiqhi wanaoteuliwa na Kiongozi Mkuu wa Iran na wataalamu 6 wa sheria wanaoteuliwa na Idara ya Mahakama na kupasishwa na Bunge. Kazi kuu ya baraza hilo ni kuhakikisha kwamba, sheria zote zinazopasishwa na Bunge haziendi kinyume na Sheria za Uislamu.

Na miaka 36 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia uhusiano wa kisiasa wa Iran na Ufaransa ulivunjika wakati wa kujiri vita vya kichokozi vya dikteta Saddam dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Serikali ya wakati huo ya Ufaransa ilitoa himaya na uungaji mkono wa pande zote kwa Iraq wakati wa kuanza hujuma na mashambulio ya jeshi la dikteta Saddam dhidi ya Iran. Aidha wakati wote wa vita hivyo, himaya ya Ufaransa ilichukua wigo mpana zaidi. Hatimaye katika siku kama ya leo Ufaransa ilichukua hatua ya upande mmoja ya kukata uhusiano wake wa kisiasa na Tehran. ***