Maadili ya Hussein bin Ali (as)
(last modified Tue, 16 Jul 2024 16:54:11 GMT )
Jul 16, 2024 16:54 UTC
  • Maadili ya Hussein bin Ali (as)

Tumo katika siku za mwezi wa Muharram ambao unakumbusha msiba adhimu na mkubwa kwa Umma wa Kiislamu.

Mwezi ambamo ndani yake mjukuu kipenzi wa Mtume wetu Muhammad (saw), Imam Hussein aliuawa kwa sura ya kutisha. Katika kipindi chetu cha leo tunakunukulieni simulizi inayoakisi tabia, murua na maadili ya Hussein aliyorithi kutoka kwa babu na baba yake watoharifu.

Imepokelewa kwamba mtu mmoja kutoka Sham, makao makuu ya watawala wa Bani Umayyah waliobadilisha mafundisho ya dini ya Kiislamu hususan Yazid laana za Mwenyezi mungu zimshukie, alifika Madina akiwa katika safari ya kelekea Makka kwa ajili ya hija au sehemu nyingine. Alimuona mtu mmoja mwenye haiba akiwa ameketi chini. Alivutiwa mno na mandhari yake na kudadisi kwa kuuliza: Bwana yule ni nani? Aliambuiwa ni Hussein bin Ali bin Abi Twalib. Mwarabu kutoka Sham ambaye alikuwa ameathiriwa mno na propaganda chafu za Bani Umayyah za kuwachafulia jina Ahlulbait (as) na Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) alianza kummiminia matusi na kumvunjia heshima kadamnas, Imam Hussein (as). Alitoa kila alilokuwa nalo moyoni na kumwaga nje vinyongo na bughudha zote alizokuwa nazo rohoni dhidi ya Ahlulbait wa Mtume, kama alivyokuwa amefunzwa na Bani Umayyah. Baada ya kumaliza kumtusi Imam, bwana huyo kutoka Sham alishangazwa na utulivu wa Imam Husseun ambaye hakukasirika, kuhamaki wala kudhihirisha chuki mbele ya bwana huyo. Alimuangalia kwa jicho la huruma na upendo, na baada ya kumkumbusha Aya za Qur'ani Tukufu zinazohimiza kuwa na tabia njema na mwenendo mzuri na watu, Imam Hussein alimuza: “Unatokea wapi, je wewe ni mtu wa Sham? Alisema: Ndio. Kisha alimwambia wewe ni mgeni katika mji huu; kama una haja ya jambo lolote tuko tayari kukukidha. Vilevile karibu nyumbani kwangu. Kama huna masurufu tutakusaidia, na kama unahitaji mavazi na fedha tutakutayarishia.”

Mwarabu wa Sham ambaye alidhani kuwa atakabiliwa na jibu kali kutoka kwa Imam Hussein kutokana na matusi na jinsi alivyomvunjia heshima hadharani, aliathiriwa mno na mwenendo wa mtukufu huyo na kusema, nilitamani lau ardhi ingepasuka na mimi nikazama ndani yake kutokana na kuoa soni na aibu. Bwana huyo wa Sham anasimulia kwamba: ‘Hadi wakati ninazungumza na Hussein (sa) hakuna mtu aliyekuwa mbaya zaidi kwangu kuliko Hussein na baba yake, lakini sasa hakuna mtu bora zaidi kuliko watukufu hao wawili.

Kama nilivyotangulia kusema, tumo katika maombolezo ya kukumbuka tukio chungu la kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein (as). Kwa mnasaba huo ni bora katika sehemu hii ya kipindi chetu cha leo tuashirie walau kwa muhtasari, baadhi ya simulizi zilizonukuliwa na maulamaa wa Kiislamu kuhusu matukio ya siku ya Ashuraa na katika medani ya mapambano ya Imam Hussein, huko Karbala. 

Mwanazuoni mashuhuri wa madhehebu ya Kishafi, Sheikh Muumin bin Hassan al Shablanji al Shafii, anasimulia kisa kifuatacho kuhusu Imam Hussein (as). Mwanazuoni huyo aliandika kitabu mashuhuri cha Nurul Abswar (kwa maana ya Nuru ya Macho) na anaeleza siri ya kuandika kitabu hicho akisema: “Nilipatwa na maradhi hatari ya macho nikawa siwezi kuona, nikaamua kwenda kwenye ziara na kaburi la mjukuu wa Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib, Sayyida Nafisa katika viunga vya Cairo huko Misri, kwa lengo la kutawasali na kupata baraka za walii huyo wa Mwenyezi Mungu, na mababu zake watoharifu. Niliweka nadhiri kwamba iwapo nitapata shifaa na kupona nitaandika kitabu kinachosimulia matukufu ya Mtume (saw) na Aali zake. al Shablanji al Shafii anaendelea kusimulia kwamba, Mwenyezi Mungu alimponya maradhi hayo ya macho na akaamua kuandika kitabu hicho cha Nurul Abswar mwaka 1290 Hijria. Katika kitabu hicho al Shablanji al Shafii anasimulia hadithi iliyopokewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saw) kuhusu jinsi mjukuu wake, Imam Hussein, atakavyouawa katika ardhi ya Karbala.  Ananukuu Hadithi iliyopokewa kutoka kwa Ummul Fadhli, mke wa ami wa Mtume, Abbas bin Abdul Muttalib akisema: “Siku moja niliingia nyumbani kwa Mtume wa Mwneyezi Mungu kisha nikamwambia: Ya Rasulallah, jana usiku niliona ndoto mbaya!

Mtume aliuliza: Ni ipi ndoto hiyo? Nilisema: Nimeota kana kwamba kipande cha mwili wako kimekatwa na kuwekwa mapajani mwangu! Mtume aliniambia: Umeona kheri. Mwanafatima atajifungua mtoto atakayeitwa Hussein. Ummul Fadhl anaendelea kusimulia kwamba, baada ya Fatima, binti ya Mtume, kujifungua Hussein, nilimuweka kwenye mapaja yangu kama alivyotabiri Mtume. Nilimwendea Rasurullah kisha nikamuweka mtoto huyo mchanga mapajani kwake. Nilipogeuka kumuangalia Mtume usoni niliona macho yake yakibubujikwa na machozi! Nilisema: "Baba na mama yangu wawe wahanga wako ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Kitu gani kinakuliza? Mtume alisema: “Malaika Jibrail amenijia na kunipasha habari kwamba, umma wangu utamuua mwanangu huyu, na amenipa udongo huu wenye rangi nyekundu."   

Mwanazuoni huyo wa Kishafi Sheikh Shablanji anaendelea kusimulia katika kitabu cha Nurul Abswar kwamba Ibnu Nabata amesema: "Wakati tulipopita na Imam Ali bin Abi Twalib (karramallahu wajhahu) katika ardhi ya Karbala miaka kadhaa kabla ya tukio la Ashura (mwezi Muharram mwaka 61 Hhijria) alisema: Hapa ndipo watakaposhukia, hapa ndipo msafara wao utakapofikia, hapa ndipo damu zao zitakapomwagwa. Hawa ni kundi katika umma wa Muhammad (saw) ambao watauawa katika medani hii, na zitawalilia mbingu na ardhi." Mwisho wa kunukuu. 

Imepokelewa katika vitabu vingi vya maulamaa na wazuoni wa Kiislamu kwamba baada ya Imam Hussein kuuawa katika jangwa la Karbala akiwa pamoja na ahli yake, watoto na wajukuu wa Mtume wakachukuliwa mateka kama watumwa kutoka Karbala, Iraq hadi Damascus huko Syria kwa mtawala Yazid bin Muawiyah, huku vichwa vya mashahidi waliouawa katika medani ya Karbala vikiwa mbele yao juu ya mikuki, mtawala huyo alisimama akiangalia mateka hao kwa kiburi na majivuno. Alisikia sauti ya kunguru kisha akasema:

"Kunguru kalia, nikamwambia: Sema au usiseme, hakika nimechukuwa deni langu kutoka kwa Mtume". Wanahistoria na wafasiri wa Qur'ani, akiwemo al Alusi katika tafsir ya Ruhul Maani juzuu ya 26:73, wanasema Yazid bin Muawiya alikuwa akiashiria jamaa zake waliouawa na Mtume Muhammad (saw) katika vita vya Badr, kama vile babu yake Utba, mjomba wake na wewengine kadhaa. Pia historia inasema kuwa, mal'uni huyo baada ya kupelekewa kichwa kitoharifu cha Bwana wa Vijana wa Poponi Imam Hussein (as), alikichokonoa kwa fimbo, huku akisoma mashairi yanayosema: "Laiti babu zangu waliouawa Badri wangeshuhudia tuliyoyafanya Karbala, basi wangepiga vigelegele na kushangilia kwa furaha, huku wakisema: heko ewe Yazid. "

Vilevile wanahistoria wamenukuu kwamba, wakati mateka kutoka Nyumba ya Mtume (saw) na kichwa cha mjukuu wake, Imam Hussein (as) kilipowekwa kwenye sinia mbele ya mtawala Yazid, mlaanifu huyu alisoma mashairi kadhaa likiwemo lile linalosema:

“Bani Hashim wamechezea ufalme, hakuna habari iliyokuja wana hakuna ufunuo ulioteremshwa kutoka mbinguni.”

Kwa kuzingatia hayo yote na mengine mengi, maulamaa kadhaa wakubwa wa Ahlusunna Waljama, kama Jalaluddin Suyuti, Ibnul Jauzi, Qadhi Abu Yaala, Taftazani na Alusi, wamesisitiza kwamba Yazid bin Muawiya alikuwa kafiri, na kwamba inajuzu kumlaani.

Kwa mnasaba wa tukio chungu la kuuawa shahidi mjukuu kipenzi wa Mtume wetu Muhammad (saw), Bwana wa Vijana wa Popeni na kinara wa mashahidi, Abu Abdillah al Hussein, amani na Myenyezi Mungu iwe juu yake, ahli na masahaba zake waaminifu, Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani na pia wapigania uhuru, haki na uadilifu popote pale walipo. Tunamuomba Allah atufufue pamoja na Hussein, babu na baba yake watukufu. Amiin ya Rabbal alamiin. Wassalam alaykum warahmatullah wabarakatuh.