Jan 31, 2025 02:21 UTC
  • Ijumaa tarehe 31 Januari 2025

Leo ni Ijumaa tarehe Mosi Shaaban 1446 Hijria sawa na 31 Januari 2025 Milaadia.

Mwezi wa Shaabani ulioanza leo ni mwezi wa ibada, kujipinda na kuomba maghufira.

Mtume Muhammad (saw) aliutukuza mno mwezi huu na kuuita kuwa ni mwezi wake. Mtume na maimamu watoharifu katika kizazi chake wamewausia mno Waislamu kufanya ibada hususan kufunga swaumu katika mwezi huu wa Shaabani kwa sababu ndio unaotayarisha uwanja mzuri wa kuingia kwenye mwezi wa ugeni wa Mwenyezi Mungu na wenye baraka tele wa Ramadhan. 

Katika mwezi huu wa Shaabani kumetukia mambo mengi muhimu kama kuzaliwa Imam Hussein bin Ali (as) mjukuu wa Bwana wetu Muhammad (saw) na pia tukio la kuzaliwa Imam wa Zama, Mahdi (as) Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake.

Siku kama ya leo miaka 753 iliyopita Ghiathuddin Abu Madhaffar Abdul Karim bin Ahmad anayefahamika kwa lakabu ya Ibn Taus, alifariki dunia huko Kadhimain, moja kati ya miji ya Iraq.

Ibn Taus alikuwa faqihi na mwandishi mashuhuri wa karne ya saba Hijria. Alihifadhi Qur'ani Tukufu akiwa na umri wa miaka 11. Baada ya hapo alijifunza fasihi ya lugha ya Kiarabu na kupata elimu kwa wanazuoni wakubwa kama Khajah Nasiruddin Tusi.

Ibn Taus ameandika vitabu kadhaa kwa lugha ya Kiarabu. 

Siku kama ya leo miaka 426 iliyopita, ilianzishwa kampuni ya kwanza ya British East India Company nchini India kwa amri ya Malkia Elizabeth wa Kwanza wa Uingereza.

Kampuni hiyo iliimarisha ukoloni wa Uingereza katika maeneo yenye utajiri huko kusini mwa Asia na baada ya hapo shughuli za ukoloni zikaimarika zaidi katika mataifa ya kusini mwa Asia kupitia kampuni hiyo. Baada ya kuasisiwa kampuni hiyo, nchi nyingine kama vile Uholanzi, Ureno na Ufaransa zilielekeza nguvu zao katika bara Hindi kwa lengo la kuhudumia ukoloni wao.

Baada ya karne 3 za kuanzishwa kampuni hiyo, ushawishi na kuimarika utawala wa Uingereza nchini India vilisababisha nchi hiyo kutangazwa kuwa sehemu ya Uingereza, na Malkia Viktoria akavikwa taji la kuwa mtawala wa India na Uingereza.   

Malkia Elizabeth wa Kwanza wa Uingereza

Tarehe Mosi Shaabani miaka 180 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Muhammad Hassan Najafi maarufu kwa lakabu ya Sahibul Jawahir.

Sahibul Jawahir alifanya uhakiki mkubwa wa masuala ya fiqhi na kusajili fikra zake katika taaluma hiyo kwa njia ya kuvutia na nyepesi. Kitabu kikubwa zaidi cha mwanazuoni huyo ni "Jawahirul Kalam" ambacho kina thamani na umuhimu mkubwa sana kati ya wataalamu wa taaluma hiyo.

Katika kitabu hicho Sheikh Muhammad Hassan Najafi ameandika masuala ya kifiqhi na sheria za Kiislamu kwa kutumia hoja madhubuti na umakini mkubwa.

Siku kama ya leo miaka 175 iliyopita, ilianzishwa harakati kubwa ya uasi ya wananchi wa China iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Taiping.

Harakati hiyo ilianzishwa kutokana na hali mbaya na umasikini uliokuwa ukiwasumbua wananchi wa nchi hiyo na hasa matabaka ya watu wa vijijini, iliyosababishwa na ukoloni wa kigeni na utawala wa familia isiyofaa ya Manchu.

Lengo kuu la harakati hiyo iliyoendelea kwa muda wa miaka 14 lilikuwa ni kuhakikisha kunakuwepo usawa katika kugawana ardhi kati ya wanawake na wanaume.   

Uasi wa Taiping

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita Imam Khomein (MA) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, alirejea nchini na kupokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi baada ya kuishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15.

Mapokezi hayo makubwa ya wananchi wa Iran kwa Imam Khomeini hayajawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia ya sasa ya dunia.

Baada ya kutoa hotuba fupi katika uwanja wa ndege wa Mehrabad, Imam Khomein alielekea moja kwa moja kwenye makaburi ya mashahidi waliouawa katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kutoa heshima kwa mashahidi hao ambako pia alitoa hotuba katika umati mkubwa wa wananchi. Kwa mara nyingine Imam aliitaja serikali ya Shapour Bakhtiar kuwa kibaraka wa Shah sanjari na kutangaza kuunda serikali mpya kwa msaada wa wananchi.

Siku kumi baada ya kurejea nchini Imam, Mapinduzi ya Kiislamu yalipata ushindi kamili na kipindi hicho cha siku kumi za baina ya kurejea Imam nchini hadi kupata ushindi kamili Mapinduzi ya Kiislamu, kinajulikana hapa nchini kama "Alfajiri Kumi".

Imam akiwasili nchini tarehe 12 Bahman