Feb 24, 2024 07:38 UTC
  • Imam Mahdi (atfs), Mwokozi Muahidiwa wa Ulimwengu

Assalaam alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Mahdi (atfs).

 

Sambamba na kutoa mkono wa kheri, baraka na fanaka kwa mnasaba huu adhimu ninakukaribisheni kkutegea sikio kipindi hikii maalumu.

 

Imam Mahdi (atfs) alizaliwa huko katika mji wa Samarra, Iraq ya leo, tarehe 15 Shaaban 255 Hijiria. Alipewa jina sawa na la Mtume (saw) yaani Muhammad na pia kunia yake ya Abul Qassim. Imam Mahdi (af) alichukua jukumu la ukhalifa wa kuongoza Umma wa Kiislamu mwaka 260 Hijiria kufuatia kuuawa shahidi baba yake mpendwa Imam Hassan Askary (as) na kwa mujibu wa Sunna ya moja kwa moja ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa msingi huo alichaguliwa kuhudumia nafasi hiyo muhimu na Mwenyezi Mungu mwenyewe, uongozi ambao bado unaendelea hadi leo hata baada ya kupita maelfu ya miaka. Imam Mahdi (as) ambaye hivi sasa yuko kwenye ghaiba yaani haonekani machoni pa walimwengu kwa amri ya Mwenyezi Mungu, atadhihiri tena na kuubadilisha kabisa ulimwengu kiuongozi.

Atafanya mabadiliko makubwa na kung'oa mizizi yote ya utawala duniani ambayo imesimama kwenye msingi wa dhulma na uonevu. Maadui wa dini ya Mwenyezi Mugu ambao daima huwa wanaimarisha kufri na kufanya njama za kuficha ukweli) mara hii pia na kama ilivyo kawaida yao, walipanga njama ya kutaka kumuua Imam na khalifa huyo wa Mwenyezi Mungu lakini Mungu akamuepusha na shari hiyo kwa kumfanya asionekane machoni pa watu, ili apate kubakia hai na wakati muwafaka utakapofika, atadhihiri tena na kuujaza ulimwengu uadilifu na usawa baada ya kujaa dhulma na uonevu. Imam Mahdi (af) anaona na kushuhudia moja kwa moja matendo na mambo yote wanayoyafanya waumini na wafuasi wake hadi wakati wa kudhihiri kwake utakapowadia.

Kudhihiri kwa Imam huyo wa mwisho, kunahitajia kupita wakati na kukomaa kwa akili, elimu na akhlaqi (maadili) ya watu na kuwa kwao tayari kwa ajili ya kushirikiana naye wakati muwafaka. Imam huyo wa mwisho wa Mwenyezi Mungu atawaongoza wanadamu wote kwenye njia nyoofu kuelekea kwa Muumba wao wakati ambao atapata fursa ya kuunda serikali itakayosimama juu ya misingi ya mafundisho ya Mwenyezi Mungu, kutekeleza uadilifu na kuheshimu sheria, na bila shaka jambo hilo litawezekana tu wakati wanadamu watakapokuwa tayari kukubali na kufuata miongozo ya mbinguni.

Katika maisha yake ya kijamii, mwanadamu anahitajia serikali na mtawala atakayelinda maisha yake na kumfanya apate maendeleo katika nyanja tofauti. Mwanadamu anapasa kuheshimu na kutii amri za watawala ili waweze kubuni jamii bora, salama, yenye utulivu na inayojitenga na kila aina ya dhulma na uonevu. Lakini kwa bahati mbaya hilo halijaweza kuthibiti bali tunayoshuhudia ni kuwa jamii ya mwanadamu inaendelea kukabiliwa kila siku na ongezeko la dhulma na uonevu. Hivyo katika mazingira ya hivi sasa ambapo jamii imetumbukia kwenye lindi la matatizo ya kisiasa na kiusalama, fitina kuenea kila sehemu, magonjwa sugu na yasiyo na tiba kuikumba jamii na utovu wa nidhamu na maadili kuenea kila upande, mwanadamu kwa dhati yake anahisi na kutarajia kuwadia siku ambayo itatawaliwa na mtawala anayefuata thamani na miongozo ya Mwenyezi Mungu, ambaye ataweza kutekeleza na kueneza uadilifu katika jamii. Mfano wa wazi ni vita vya sasa vya Gaza na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala haramu wa Israel. Madola ya kibeberu yakiongozwa na Marekani yameendelea kuunga mkono utawala dhalimu wa Israel liicha ya utawala huo kufanya dhulma, mauaji na ukandamizaji wa wazi dhidi ya Wapalestina. Matarajio au kusubiri huko ndiyo mazingira yanayofaa kwa ajili ya kukubalika utawala wa ulimwengu wa Imam Mahdi (af), ambayo yanapasa kuwa katika kila jamii ya mwanadamu. Ni wazi kuwa tunapasa kuzingatia nukta hii kwamba, kusubiri huku hakupasi kuchukuliwa kuwa na maana ya kupuuza mambo na kukaa kimya. Mwanadamu hapasi kuketi pembeni na kutochukua hatua yoyote ya kurekebisha hali ya mambo katika jamii, bali kusubiri kuna maana ya matumaini na matarajio. Roho na msingi wa matarajio hayo ni kuwa na mtazamo mzuri kuhusiana na mustakbali wake ambao Mwenyezi Mungu amembashiria moja kwa moja kupitia Aya na Riwaya nyingi. Serikali ya Imam Mahdi (af) inatambulishwa katika mtazamo mpya wa jamii iliyo bora zaidi kiuadilifu na kimaadili ambayo hadi leo haijawahi kushuhudiwa na mwanadamu yoyote.

Kwa kudhihiri Imam Mahdi (af) tawala zote mbovu, dhalimu na fasidi zitafutwa kwenye mgongo wa ardhi na kuwa simulizi za historia. Ni wazi kuwa kufuta tawala kama hizo zinazotawaliwa na watawala fasidi, kunahitajia mapambano dhidi yao. Kuhusiana a suala hilo tunapasa kuzingatia nukta hii kwamba ili kufanikiwa katika lengo hilo, kunahitajika kuwepo serikali yenye nguvu na jeshi lililojizatiti vyema kwa silaha, serikali ambayo bila shaka itakuwa na maafisa na wafuasi walio na sifa maalum. Ni wazi kuwa maafisa na wafuasi kama hao wanapasa kuwa na uwezo mkubwa wa kuvumilia matatizo na machungu mengi yanayopatikana katika medani ya vita na kuongoza jamii katika mazingira magumu ya kudhihiri Imam Mahdi (as). Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu hajamlazimisha Imam wa Zama, Imam Mahdi (af) kubeba ujumbe huo peke yake na kwa msaada Wake wa mbinguni, bali jeshi kubwa la watu linapasa kushiriki katika tukio hilo muhimu la kihistoria ili nao wenyewe wapate kujibadilisha na kuwa na nafsi muhimu katika kuainisha mustakbali wao wa kihistoria.

Katika kipindi cha kabla ya kudhihiri Imam (af), wanaomsubiri mtukufu huyo wana jukumu kubwa na zito la kuwalea watu na jamii inayofaa ambayo itaweza kumsaidia Imam Mahdi katika mapambano yake ya kurudisha uadilivu na usawa duniani. Jukumu la kwanza la wanaomsubiri Imam ni kuwa wanapasa kupata elimu na maarifa ya kutosha kuhusiana na Imam wao huyo wa Zama. Jambo hilo lina umuhimu mkubwa kadiri kwamba Mtume Mtukufu (saw) amenukuliwa akisema katika Riwaya kwamba Mtu anayeaga dunia hali ya kuwa hamjui Imam wa zama zake huwa amekufa kifo cha kijahili. Jukumu jingine ni kuwa, wanapasa kujitenga na sifa zote mbaya na kujipamba kwa sifa bora na za kuvutia kidini. Imam Swadiq (as) anasema: 'Kila mtu anayependa kuwa miongoni mwa wafuasi wa Mahdi Muahidiwa (af), anapasa kusubiri, kujitenga na maovu na kuwa na akhlaqi nzuri katika hali hiyo. Hivyo iwapo ataaga dunia katika hali hiyo.... atakuwa na malipo sawa na ya yule mtu aliyemdiriki (kumwona/kauishi katika zama za kudhihiri kwake) mtukufu huyo. Hivyo fanyeni juhudi na muendelee kusubiri.'

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kilichokujieni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Mahdi (atfs) umefikia tamati. Ni matumini yangu kuwa mmenufaika na hiki kichache kilichokkuandalieni kwa mnasaba huu. Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.