Kujilinda na kujihami katika mtazamo wa Qur'ani
Hamjambo na karibuni kuwa nami katika kipindi chetu cha leo cha Makala ya Wiki ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya Wiki ya Kujihami Kutakatifu nchini Iran.
Hii leo hakuna tena haja ya kueleza na kubainisha maovu na maafa ya vita. Utendaji wa watawala madhalimu, madikteta na waovu katika dunia ya sasa na mandhari za kutisha za mashambulizi ya mabomu dhidi ya miji na nchi mbalimbali, picha za kuuliwa watu, hususan wanawake na watoto wadogo, vyote hivyo vinaonesha waziwazi ubaya na uovu wa vita. Hata hivyo wakati taifa linaposimama kupambana na sera za kupenda kujipanua na kukataa kusalimu amri, vita hivyo hupata sura na rangi ya 'utakatifu' na kuwa vita baina ya haki na batili.
Wakati medani ya vita inapokuwa uwanja wa kudhihirishia irada, azma, imani na uwezo wa taifa mbele ya wachokozi, na wakati wananchi wanapojifunga kibwebwe na kuvaa vazi la Jihadi kwa ajili ya kulinda itikadi na utambulisho wao wa kitaifa na kuipa mgongo hali na mali zao kwa ajili ya kupata daraja ya juu ya kufa shahidi, basi vita kama hivi si jambo la kuchukiza tena, kwa sababu wakati huu hupewa rangi ya utukufu.
Kujilinda au kujihami kutakatifu kwa wananchi wa Iran mbele ya uchokozi na uvamizi wa jeshi la dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein, ambalo lilikuwa likiungwa mkono na kusaidiwa na nchi za Magharibi, ilikuwa hamasa kubwa iliyoendelea kwa kipindi cha miaka 8 baada ya kuanza tarehe 22 Septemba 1980.
Hapana shaka kuwa taifa lolote linalovamiwa na kuchokozwa linapaswa kusimama kwa ajili ya kutetea haki yake, na mapambano kama hayo ni jambo la lazima kwa mtazamo wa mantiki na akili, na ni miongoni mwa haki za kimsingi za kila mwanaadamu. Ni muhali kupata taifa lolote ambalo halisimami kukabiliana na adui anayehatarisha uhai wake, na inapolazimu taifa hilo hupambana hadi pumzi na tone la mwisho la damu yake. Kwa sababu hiyo jumuiya za kimataifa ambazo kawaida hukosoa vita na kuvikemea, zinahalalisha na kuhimiza mapambano ya kujitetea na kujihami.
Dini ya Uislamu pia ambayo kimsingi inahimiza amani, suluhu na kuishi pamoja kwa usalama wanaadamu wote, imeunga mkono suala la kujihami na kulaani vikali dhulma na hujuma dhidi ya mtu, jamii au taifa lolote. Qur'ani Tukufu inasema katika Aya ya 39 ya Suratul Haj kwamba: Wameruhusiwa kupigana wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa, na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia.
Waislamu wa Makka ambao walilazimika kuhamia Madina kutokana na maudhi na dhulma za washirikina, waliamrishwa na Mwenyezi Mungu kusimama na kukabiliana na adui baada ya kupata uwezo na nguvu ya kijeshi na kisiasa. Qur'ani Tukufu inawaahidi ushindi na msaada wa Mwenyezi Mungu watetezi hawa wa haki kwa kusema: Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamini. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila haini mwenye kukufuru sana. (al Haj: 38)
Hata hivyo katika mtazamo wa Qur'ani kujilinda kumeruhusiwa kwa sharti la kuzingatiwa na kuheshimiwa mipaka na masharti yake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu hawapendi wanaovuka mipaka na sheria. Miongoni mwa sifa za kujilinda kulikoruhusiwa na sheria ni kwamba japokuwa kutafanyika kwa ajili ya kulinda na kutetea nafsi au nchi yako lakini pia kunapaswa kufanyika kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kulinda sheria zake.
Tunapaswa kusisitiza tena kuwa kujilinda na kupambana na dhulma ni miongoni mwa masuala ya kimaumbile ya mwanaadamu na kila mtu anayechokozwa au kushambuliwa anapaswa kujilinda na kujitetea kwa mujibu wa hukumu ya akili na maumbile. Kwa upande wake Qur'ani Tukufu na Hadithi za Mtume na Ahlubaiti zake, mbali na kuthamini aina hii ya kujilinda na kujitetea, zimeweka pia masharti kadhaa ya mambo hayo ili watu wasije wakachupa mipaka wakati wa kujitetea. Kwanza ni kuwapo udharura wa kujitetea na kwamba suala hilo linapaswa kunasibiana na kiwango cha hatari inayomkabili mtu anayejitetea.
Mtazamo wa Qur'ani kuhusu vita umesimama juu ya nguzo kadhaa ambazo hapa tunaashiria baadhi yao. Kwanza ni kuwa Mwenyezi Mungu amemuumba mwanaadamu akiwa na uwezo wa kuchagua baina ya njia mbili na kujiamulia mambo yake mwenyewe. Hivyo basi kiumbe huyo ana uwezo wa kuchagua baina ya vita na amani. Sehemu ya aya ya 253 ya Suratul Baqara inasema: Na lau Mwenyezi Mungu angependa wasingepigana, lakini Mwenyezi Mungu hufanya ayatakayo. Kwa maana kwamba hufanya ayatakayo kwa hekima na hamlazimishi mtu kitu chochote.
Katika upande mwingine muqtadhaa wa hikima na rehma ya Mwenyezi Mungu ni kuwa ufisadi, ufuska na uovu unaofanywa na kundi la watu unapaswa kudhibitiwa ili dunia isitawaliwe na uovu na kizazi cha wanadamu kisiangamie. Aya ya 251 ya Suratul Baqara inasema: Na lau Mwenyezi Mungu asingewazuia baadhi ya watu kwa kutumia wengine ingeliharibika ardhi; lakini Mwenyezi Mungu ni mwenye ihsani na wema juu ya viumbe vyote.
Vilevile hikima ya Mwenyezi Mungu imeamua kwamba, kufru na ushirikina visienee dunia nzima na utajo wake Mola Muumba na masuala ya kiroho kutoweka kabisa. Kwa msingi huo Mwenyezi Mungu huwasaidia waumini na wale wamchao kwa ajili ya kulinda dini yake ili akumbukwe daima. Aya ya 40 ya Suratu Haj inasema: Na lau Mwenyezi Mungu asingewakinga watu kwa baadhi ya watu basi yangelivunjwa mahekalu na makanisa na sehemu za kuswalia na misikiti ambayo ndani yake hutajwa jina la Mwenyezi Mungu kwa wingi. Na hakika Mwenyezi Mungu humnusuru yule anayemnusuru Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye Nguvu, mwenye enzi.
Uwezo wa kulinda nafsi, heshima na mali mbele ya adui mchokozi na mvamizi ni katika hiba na neema za Mwenyezi Mungu kwa kimbe huyo kwa ajili ya kulinda heshima na hadhi ya mwanadamu. Hata hivyo kwa kuwa vita na kujitetea daima huambatana na hasara na maafa, siku zote limekuwa jambo lisilopendwa na wanadamu. Pamoja na hayo tunapaswa kukumbuka kuwa, kulinda vitu muhimu vya kimaada na kiroho vya mwanadamu kuna thamani ya kusimama na kustahamili misiba na mashaka kama hayo. Qur'ani Tukufu inasema katika aya ya 216 ya Suratul Baqara kwamba: Mumefaradhishiwa kupigana vita nalo ni jambo la kuchukiza kwenu. Na huwenda mkachukia kitu nacho kikawa kheri kwenu, na huwenda mkapenda kitu nacho kikawa shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua, nanyi hamjui.
Lengo kuu la vita vya jihadi ni kuondoa visiki na vizuizi vya ustawi na ukamilifu wa kiroho na kuwalea wanadamu kwa njia sahihi. Kwa sababu hiyo Qur'ani Tukufu inawahamasisha walinzi na wapiganaji wa jihadi kwa kutumia mbinu mbalimbali na kuwapa bishara ya kupata rehma na radhi za Mwenyezi Mungu. Katika aya ya 111 ya Suratu Tauba pia Qur'ani inaitambua jihadi kuwa ni sawa na kufanya biashara ya Mwenyezi Mungu.
Katika mtazamo wa Qur'ani wapiganaji wa jihadi wanaosimama kupambana na kuuawa katika njia ya Mwenyezi Mungu huitwa mashahidi walio hai, na kwamba wapo katika neema za Mwenyezi Mungu. (Baqara:154) Vilevile Qur'ani tukufu inawaahadi wapiganaji wa Jihadi msaada wa Mwenyezi Mungu kama inavyosisitiza Aya ya 11 ya Anfal na ile ya 151 na Suratul Aal Imran.
Vita havina uasili katika fikra za Kiislamu, bali dini hiyo daima inasisitiza juu ya amani, suluhu na utulivu baina ya wanaadamu wote. Hata hivyo kama mtu au nchi itafanya uchokozi na kuvamia nyingine basi Waislamu huwajibika kusimama kwa ajili ya kuondoa au kuzuia uvamizi na uchokozi huo. Ni kwa mujibu wa mtazamo huo, ndipo hayati Imam Ruhullah Khomeini akasema kuhusu vita vilivyoanzishwa na Saddam Hussein na waitifaki wake dhidi ya Iran hapo mwaka 1980 kwamba: "Sisi tunapinga vita kama unavyotuamuru Uislamu na tunapenda kuona amani na usalama vikitawala nchi zote. Hata hivyo iwapo tutalazimishwa vita basi taifa letu lote ni la wapiganaji."
Miongoni mwa mambo yaliyoshuhudiwa katika kipindi chote cha miaka 8 ya kujitetea kutakatifu kwa Jamhuri ya Kiislamu ni kulindwa sheria za dini ya Kiislamu na kanuni za kibinadamu. Rubani mmoja wa jeshi la Iran aliyetumwa katika operesheni ya kuvunja daraja la kijeshi nchini Iraq ameandika katika ripoti yake kwamba: Nilipotumwa kubomoa daraja hilo niliona gari la raia likipita juu yake. Nilisubiri kidogo katika anga ya eneo hilo hadi gari hilo ambalo halikuwa la kijeshi, lilipovuka na baada ya hapo nililenga daraja na kulivunja. Sikutaka mtu asiye katika vita na sisi apatwe na madhara yoyote."
Kuchelewesha mashambulizi kwa rubani huyo kungeweza kumtia hatarini yeye na ndege yake, na ni jambo ambalo halikubaliki katika vipimo vya kijeshi. Pamoja na hayo makamanda wa jeshi la Iran walimuunga mkono rubani huyo kwa kulinda sheria za Kiislamu vitani na kuheshimu kanuni za kibinadamu.
Hivi ndivyo walivyokuwa mashujaa wa Kiirani katika kipindi chote cha miaka 8 ya kujitetea kutakatifu chini ya uongozi wa Ayatullah Ruhullah Khomeini katika hamasa ya kulinda nchi na Mapinduzi ya Kiislamu itakayobakia na kukumbukwa siku zote.