Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Malaria
https://parstoday.ir/sw/radio/uncategorised-i28148-siku_ya_kimataifa_ya_kupambana_na_malaria
Tarehe 25 ya Jumanne ya wiki hii dunia iliadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Malaria ambayo ilitangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Siku hiyo ilikuwa fursa kwa walimwengu kutambua vyema zaidi ugonjwa huo na nchi mbalimbali kujifunza kutokana na tajiriba na uzoefu wa nchi mbalimbali juu ya namna ya kudhibiti ugonjwa huo unaoua mamilioni ya watu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 23, 2017 06:52 UTC
  • Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Malaria

Tarehe 25 ya Jumanne ya wiki hii dunia iliadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Malaria ambayo ilitangazwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Siku hiyo ilikuwa fursa kwa walimwengu kutambua vyema zaidi ugonjwa huo na nchi mbalimbali kujifunza kutokana na tajiriba na uzoefu wa nchi mbalimbali juu ya namna ya kudhibiti ugonjwa huo unaoua mamilioni ya watu.

Malaria ni miongoni mwa magonjwa yanayoenea kwa wingi katika baadhi ya nchi za dunia ambayo yanatatiza mipango ya ustawi ya nchi hizo. Ugonjwa huo husambazwa na vimelea vya "Plasmodium" vinavyoambukizwa na mbu wa kike Anopheles. Vimelea hivyo hubakia hai katika mwili wa mbu kwa kipindi cha karibu siku 9 hadi 12 na katika kipindi hicho huweza kuambukizwa kwa mwanadamu anayeng'atwa na mbu mwenye vimelea hivyo. Maambukizi hayo ya malaria kwa kawaida hufuatiwa na dalili kadhaa ikiwa ni pamoja na kuhisi baridi na kutetemeka kunakosababishwa na hali hiyo, homa kali, kutokwa na jasho kwa wingi, kukosa utulivu, maumivu ya kichwa, kutapika, kuharisha na kadhalika. Kwa ujumla dalili za malaria zinashabihiana sana na zile za homa ya mafua (influenza) au magonjwa mengine yanayotokana na virusi. Dalili nyingine za malaria ni pamoja na maumivu ya viungo vya mwili, mwili kuwa na rangi ya njano na macho kuwa meupe. Katika malaria kali zaidi dalili hizo huoenekana siku sita hadi 14 baada ya kupatwa na vimelea vya Plasmodium. Ugonjwa huo unaweza kumfanya mtu apoteze fahamu na hatimaye kuaga dunia. Watoto na wanawake waja wazito ndio wanaoathiriwa zaidi na ugonjwa huo.

Mbu wa Anopheles anayeeneza ugonjwa wa malaria

Japokuwa ugonjwa wa malaria umeangamizwa katika nchi zenye hali ya hewa ya wastani, lakini hadi sasa ungali unachukua roho za watu katika nchi zenye joto au zinazokaribia mstari wa Ikweta za Afrika, maeneo ya Asia, Mashariki ya Kati na America ya kati na kusini. Ripoti za hivi karibuni zinaonesha kuwa, kesi za maambukizi milioni 350 hadi milioni 500 za malaria huripotiwa kila mwaka duniani na watu kati ya milioni moja hadi tatu hufariki dunia kutokana na ugonjwa huo, aghlabu yao wakiwa  watoto wadogo na wanawake wajawazito.

Takwimu zinaonesha kuwa, kila sekunde 30 mtoto mmoja hufariki dunia kutokana na malaria na vifo vingi zaidi vya watoto hao hutokea katika nchi za Kiafrika. Katika nchi za bara hilo pia wanawake milioni 30 hupata mimba katika maeneo yenye maambukizi makubwa zaidi ya malaria, suala ambalo ni hatari kubwa kwa kina mama wajawazito wenyewe na watoto walio matumboni mwao. Kuavya mimba ghafla, kuzaliwa watoto waliofariki dunia, kuzaa kabla ya wakati na kuzaliwa watoto wenye uzito mdogo ni miongoni mwa mambo yanayowakabili wanawake wajawazito wanaopatwa na ugonjwa wa malaria. Uchunguzi umeonesha kuwa, zaidi ya kina mama wajawazito elfu kumi na watoto wachanga laki mbili hufariki dunia kila mwaka barani Afrika kutokana na ugonjwa wa malaria.

Mwaka 2015 Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa, nchi 33 duniani zimeripoti chini ya kesi elfu moja (1000) za ugonjwa wa malaria na kwamba kiwango cha vifo vinavyotokana na ugonjwa huo kimepungua kwa asilimia 60 tangu mwaka 2000. Hata hivyo uchunguzi unaonesha kuwa, hadi sasa watu bilioni 3.2 duniani wanakabiliwa na hatari ya kupatwa na malaria na kwamba idadi kubwa ya watu wanaokabiliwa na hatari ya kupatwa na malaria wako katika nchi za kusini mwa Afrika. Ripoti zinaonesha kuwa, katika mwaka 2015 asilimia 88 ya kesi za kupatwa na ugonjwa wa malaria na asilimia 90 vifo vilivyosababishwa na ugonjwa huo vilitokea katika maeneo hayo ya Afrika. Ugonjwa huo unaonekana kukomeshwa kabisa katika nchi za Ulaya na Marekani na kesi zinazoripotiwa huko aghlabu huwa za wasafiri au watalii waliokwenda katika nchi hizo kutoka kwenye maeneo yanayosumbuliwa na malaria kama Afrika na India.  

Malaria inatishia maisha ya maelfu ya watoto barani Afrika

Shirika la Afya Duniani lilipanga kupunguza kesi za ugonjwa wa malaria na kiwango cha vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo kote duniani kwa asilimia 90 hadi kufikia mwaka 2030. Hata hivyo upungufu wa bajeti uliojitokeza katika miaka ya hivi karibuni umekwamisha mpango huo. Moja kati ya sababu za kupungua bajeti ya kupambana na malaria ni kujitokeza maradhi mengine hatari duniani ambayo kuna udharura wa kukabiliana nayo. Kwa mfano kuenea kwa maradhi ya Ebola hapo mwaka 2014 na mgogoro wa virusi vya Zika vilizifanya nchi nyingi ziyatambue maradhi hayo kuwa ni hatari kubwa zaidi ya malaria na kuanza kutumia gharama kubwa kwa ajili ya kupambana na magonjwa hayo. 

Baada ya hapo kumeainishwa malengo ya miaka mitano ijayo ambayo ni pamoja na kupunguza vifo vinavyosababishwa na malaria hadi kufikia thuluthi moja ya kiwango cha sasa, (karibu vifo vya watu laki sita kwa mwaka) na kupunguza kesi za kupatwa na maradhi hayo kwa asilimia 40 katika nchi 19 za Afrika na kanda ya Mekong inayojumuisha nchi kadhaa za Asia. Kwa mujibu wa mpango huo wa WHO, iwapo malengo hayo ya muda mfupi yatafikiwa, kutakuwepo uwezekano wa kutokomezwa kabisa ugonjwa wa malaria hadi kufikia mwaka 2050. Hata hivyo sharti ya kutokomezwa kabisa ugonjwa huo ni kutekelezwa barabara mipango ya kinga ya malaria. Kwa msingi huo Shirika la Afya Duniani limetangaza kwamba, nara na kauli mbiu ya Siku ya Malaria Duniani mwaka huu wa 2017 ni "Jitihada za Kukinga" (A push for prevention) ili nchi zote duniani zishirikiane na kuchukua hatua za haraka za kung'oa kabisa ugonjwa huo.

Kauli mbiu ya Siku ya Malaria Duniani mwaka huu wa 2017 ni "Jitihada za Kukinga" (A push for prevention)

Japokuwa wasomi na wataalamu wa tiba wanafanya jitihada kubwa za kupata kinga madhubuti ya kuzuia ugonjwa wa malaria, lakini hadi sasa hakuna kinga iliyothibitishwa ya ugonjwa huo. Kwa sasa kuna njia tatu kuu za kupambana na ugonjwa huo duniani: Njia ya kwanza ni kuainisha haraka na kwa wakati mwafaka kesi za ugonjwa huo. Njia ya pili ambayo ni makhsusi kwa ajili ya meneo ambayo kiasili ni maeneo yenye kesi nyingi za ugonjwa huo, ni operesheni za mara kwa mara za kunyunyizia sumu na dawa za kuua vimelea vya malaria, kutumia vyandarua na kukausha maeneo yanayotumiwa na mbu kwa ajili ya kuzaliana. Njia ya tatu ni kutazamia hali mapema na haraka na kuweka taratibu za udhibiti wa kesi zinazotokea katika maeneo ambayo kiasili hupatwa na kesi za ugonjwa huo.   

Wataalamu wa masuala ya afya wamekuwa wakitilia mkazo masuala hayo na kuzitaka nchi mbalimbali kuimarisha mifumo yao ya huduma za afya. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Bi Margaret Chan anasisitiza kuwa, suala la kupambana na malaria linapaswa kupewa umuhimu mkubwa. Anasema nchi nyingi zinazosumbuliwa na malaria zingali na safari ndefu hadi kufikia viwango vya kimataifa vya kukinga ugonjwa huo na kwamba iwapo suala hilo halitapewa mazingatio ya kutosha vifo vinavyotokana na ugonjwa huo vitashika tena kasi ya kupanda juu.

Sambamba na hayo yote yaliyosemwa, inatupasa kuelewa kwamba, mapambano dhidi ya matataizo ya afya duniani ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya malaria yanahitaji ushirikiano wa kimataifa. Kuzishinda changamoto kubwa zinazomkabili mwanadamu katika sekta ya afya kunaziwajibisha nchi zote hususan zilizoendelea kutimiza wajibu na majukumu yao katika uwanja huo. Vilevile nchi za Magharibi zinazomiliki teknolojia ya kisiasa, mbinu na dawa bora zaidi za kukabiliana na ugonjwa huo zinapaswa kuacha tabia ya kujilimbikizia mambo hayo kwa ajili ya kupata faida zaidi za kiuchumi na kuweka mbele masuala ya kibinadamu.