Kwa mnasaba wa siku ya kuuawa shahidi Imam Hadi AS
Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Hamjambo wasikilizaji wapenzi na karibuni kuwa nasi katika kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kukumbuka tukio chungu la kuuawa shahidi Imam Ali al Hadi ambaye alikuwa miongoni mwa wajukuu wa Mtume wetu Muhammad (SAW).
Kuuawa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu ni pambo la mawalii wake Allah SW na alama ya uja kamili, uhuru na kutosalimu amri mbele ya watawala madhalimu na anasa za dunia. Kuuawa shahidi ni daraja kubwa kabisa ya ukamilifu wa mwanadamu anayejitolea na kusabilia nafasi yake kwa ajili ya malengo aali na matukufu.
Imam Ali al Hadi (as) ni mfano na kielelezo aali kabisa cha mawalii wa Mwenyezi Mungu SW. Mtukufu huyo aliuawa shahidi katika njia ya kueneza dini sahihi ya Allah mwaka 254 Hijria kwa kupewa sumu kwa amri ya mtawala Muutaz aliyekuwa khalifa wa 11 wa utawala wa Bani Abbas baada ya kustahamili vifungo jela, mateso na mashaka mengi ya kiroho na kimwili. Tarehe tatu Rajab inakumbusha tukio hilo chungu la kuuawa shahidi Imam na mjukuu wa Mtume wetu Mumammad (saw) na kwa mnasaba huu Redio Tehran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote hususan wafuasi na wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume mtukufu.
Imam Ali Annaqi aliyepewa lakabu ya al Hadi, alizaliwa katika nusu ya mwezi wa Dhil Hijja mwaka 212 Hijria karibu na mji mtakatifu wa Madina. Baba yake ni Imam Muhammad al Jawad (as) na mama yake alijulikana kwa jina la Sumata al Maghribiyya na alikuwa mwanamke mwema na mcha Mungu. Kipindi cha Uimamu wake kilidumu kwa miaka 33 na kilikuwa na sifa zake za kipekee kutokana na kuenea fikra na teolojia mpya na maswali mengi ya kifalsafa. Makundi tofauti ya kifikra yalikuwa katika hali ya kueneza na kuhubiri fikra na mitazamo yao. Utawala wa Bani Abbas pia ulitumia mazingira hayo ya mkanganyiko wa kifikra na kielimu kwa ajili ya kutimiza malengo yake ya kisaisa.
Katika kipindi hicho Imam al Hadi (as) daima alikuwa akitahadharisha kuhusu opotofu wa kiitikadi na kifikra uliokuwepo wakati huo. Hata hivyo utawala dhalimu wa Bani Abbas ulizidisha mzingiro na udhibiti wa nyumba ya Imam kwa lengo la kumtenga na kumuweka mbali na jamii, suala ambalo lilizidisha matatizo ya Umma wa Kiislamu. Imam naye kwa upande wake alikuwa akifanya jitihada za kujaribu kuzima njama hizo chafu. alianzisha chuo cha elimu na maarifa na kulea wanafunzi hodari kwa kutoa maarifa sahihi ya Kiislamu na mfano wa wanafunzi hao alikuwa ni Sayyid Abdul Adhim al Hassani, Hussein Said al Ahwazi na wengine wengi. Aliandika risala nyingi kwa ajili ya wanafunzi wake ikiwemo risasi ya kuthibitisha uadilifu wa Allah, risala ya majibu ya maswali ya Yahya bin Aktham aliyekuwa miongoni mwa maulamaa wa utawala wa Bani Abbas, risala ya sheria za dini na kadhalika. Harakati hizo za kielimu za Imam al Hadi sambamba na mapambano yake makubwa dhidi ya makundi yaliyokuwa yamepotea kifikra na kiitikadi mbali na kutoa mwongozo kwa umma na jamii, ziliwaamsha na kuwazindua Waislamu.
Moja ya harakati kubwa zaidi za Imam Al Hadi (as) ilikuwa ile ya mapambano yake ya kifikra na ya kiutamaduni dhidi ya makundi yenye fikra na itikadi potofu. Makundi hayo kwa hakika yalikuwa matunda na matokeo ya anga chafu na iliyojaa sumu iliyotengenezwa na utawala wa Bani Abbas. Miongoni mwa makundi hayo yaliyokuwa na fikra na itikadi potofu ni lile la Ghulat. Kundi hili lilikuwa na wafuasi wenye misimamo mikali, iliyochupa mipaka ya dini na isiyo na mantiki kuhusu Uimamu. Wafuasi wa kundi hili walivuka mipaka ya dini na kumtukuza Imam kiasi cha kumwabudu na kumuoina kama Mungu. Kwa kutumia fikra hizo potofu, kundi hilo liliharamisha baadhi ya sheria za wajibu za Kiislamu na kuhalalisha makosa na dhambi kubwa. Kundi hili lilizusha bidaa nyingi katika dini kwa shabaha ya kuhalalisha na kuyapa sura ya sheria na dini matakwa na matamanio yao. Imam Ali Al Hadi alipambana vikali na wafuasi wa kundi hili na kutangaza waziwazi msimamo wake wa kujitenga na kuwa mbali kabisa na kundi hilo. Ili kudhihirisha sura na hakika ya kundi hilo, Imam al Hadi (as) alimjibu mtu aliyeuliza swali kuhusu itikadi potofu za wafuasi wa kundi hilo akisema: Naapa kwa jina la Allah kwamba Mwenyezi Mungu SW alimtuma Muhammad (saw) na mitume wa kabla yake kwa ajili ya kulingania watu dini ya Tauhidi na Mungu Mmoja na kuwaamuru kutoa zaka, kufanya ibada ya hija. Mtume Muhammad (saw) pia aliwalingania watu dini ya Tauhidi na Mungu Mmoja na sisi ni makhalifa wake na waja wa Mwenyezi Mungu na hatumshirikishi na chochote. Iwapo tutamtii Mwenyezi Mungu ataturehemu, na kama tutaasi amri zake tutakumbwa na adhabu yake kali.... Ninajitenga kikamilifu na mtu yeyote anayotoa maneno ya kuwatukuza Maimamu katika kizazi cha mtume kupitia kiasi na najikinga kwa Mwenyezi Mungu na maneo yao...
Miongoni mwa makundi potofu yaliyozusha tashwishi katika jamii ya wakati huo ya Waislamu lilikuwa lile la masufi. Wafuasi wa kundi hilo waliwapoteza watu kutokana na dhahiri yao ya zuhudi na kuipa mgongo dunia, uchamungu na kutupilia mbali anasa. Kundi hili la masufi, kama lilivyokuwa lile la ghulati, lilitumia vibaya itikadi za kidini za watu kwa ajili ya kutimiza malengo yake. Wafuasi wa kundi hili walikuwa wakikusanyika katika maeneo matakatifu kama Msikiti wa Mtume mjini Madina na kuwavutia watu wa kawaida kwa harakati na hali makhsusi kama za kusoma uradi na dhikri kiasi kwamba watu alikuwa wakiwaona kuwa ndio wachamungu na wasafi zaidi. Baadhi ya watu walikuwa wakiathirika na kuhadaika kwa mandhari kama hizo.
Imam Ali al Hadi (as) alichukua jukumu kubwa la kufichua na kuanika wazi bidaa na uzushi uliokuwa ukifanywa na wafuasi wa makundi hayo na historia imenukuu mengi kuhusu harakati za Imam katika uwanja huo. Wanahistoria wameandika kuwa, siku moja wakati Imam alipokuwa ameketi na masahaba zake katika Msikiti wa Mtume mjini Madina, lilingia kundi la masufi na kuketi katika kona moja ya msikiti huo. Kundi hilo lilianza dhikri na uradi makhsusi. Imam Ali Al Hadi ambaye aliona hali hiyo na vitendo vya hadaa vya wafuasi wa kundi hilo, aliwaambia masahaba zake kwamba: Hebu tazameni kundi hilo la watu wenye hila na malaghai. Hawa ni masahiba wa shetani na wavunjaji wa nguzo imara za dini. Watu hawa wamejivika vazi la zuhudi na kujipa sura ya kuipa dunia mgongo kwa shabaha ya kufikia malengo yao machafu na wanakesha usiku kwa lengo la kuwatumbukiza maamuma katika mitego yao. Wanasema: Laa ilaha illallah kwa ajili ya kuwahadai watu na taratibu wanaelekea katika shimo walilojimbia wao wenyewe...
Imam Ali Annaqi al Hadi (as) pia alikabiliana vilivyo na makundi ya mijadala ya kiteolojia yaliyomfananisha Mwenyezi Mungu na mwanadamu, kuzusha itikadi zisizo sahihi kwamba wanadamu wanatezwa nguvu katika amali na matendo yao na kadhalika.
Maimamu katika kizazi cha Mtume Muhammad na Ahlul Bait (asa) ambao ni taa za uongofu na nuru walikuwa chemchemi ya elimu na hazina kubwa ya maarifa. Daima waliwamulikia watu katika vipindi mbalimbali vya giza la ujinga na ujahili na kuwaonesha njia nyoofu na maarifa asili ya Uislamu. Katika upande huo Imam al Hadi alikuwa mstari wa mbele na moja na jitihada zake ilikuwa kuandika risala ya teolojia akijibu mishkeli na maswali ya kifikra na kiitikadi yaliyokuwa yakigubika fikra na nyoyo za watu wa zama hizo. Katika risala hiyo aliweka wazi masiala yanayohusiana na madai ya kutenzwa nguvu mwandamu katika amali na matendo yake tena kwa kutumia hoja za kimantiki na lugha nyepesi na sahali. XXX
Wapenzi wasikilizaji muda uliotengwa kwa ajili ya kupindi hiki maalumu umefikia mwisho. Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani hususan wafuasi wa watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (saw) kwa mnasaha wa siku ya kukumbuka tukio chungu la kuuawa shahidi mtukufu huyo. Tunakabilisha kipindi hiki kwa semi kadhaa za hekima za Imam al Hadi ambaye amesema: "Bora zaidi kuliko wema ni mtendaji wema, na bora zaidi kuliko maneno mazuri ni msemaji wake. Kitu bora zaidi kuliko elimu ni mwenye ilimu na kibaya zaidi kuliko ubaya na uovu ni mtenda maovu."
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.