Kumbukumbu ya Siku za Fatimiyah
Assalaam alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa siku hizi za maombolezo ya binti ya Mtume (SAW), Bibi Fatima Zahra (AS) zinazojulikana kama ‘Siku za Fatimiya’.
Katika kipindi hiki cha leo tutatupia jicho baadhi ya visa na sira fupi ya bibi huyu Mtukufu aliyedhulumiwa na kukumbwa na masaibu mengi baada ya kuaga dunia baba yake. Kuuweni nami hadi mwisho wa kipindi.
Bibi Fatima al Zahra (as) ni binti ya Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na Bibi Khadija bint Khuwailid, mke kipenzi wa Mtume na mtoto wa nne wa kike wa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Baadhi ya lakabu zake ni al Zahra, Siddiqa, Twahira, Mubarakah, Zakiyyah, Raadhiyah, Mardhiyya, Muhaddathah na Batul.
Bibi Fatima al-Zahra alizaliwa na kulelewa katika nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ambako Malaika wa wahyi na ufunuo walikuwa wakiingia na kutoka wakileta ujumbe wa Mola Mlezi. Alikulia katika nyumba ambayo ndiyo pekee sauti ya Allahu Akbar (Mwenyezi Mungu ni Mkubwa) ilikuwa ikisikika katika zama za awali za Uislamu. Baada ya kuolewa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) alitambulika kuwa mwanamke kigezo bora cha kuigwa na watu wote katika maisha ya ndoa, ibada na mwenendo mzuri. Baada ya kazi za nyumbani, Bibi Fatima alikuwa akijipinda kwa ibada, dua na kumtaaradhia Mola Karima. Imam Ja'far Swadiq (as) ananukuu kutoka kwa babu yake Imam Hassan bin Ali, mwana wa Bibi Fatima (as) akisema kwamba: "Mama alikuwa akisimama katika mihrabu ya ibada katika usiku za kuamkia Ijumaa hadi asubuhi. Alikuwa akiwaombea dua waumini wa kike na kiume bila ya kusema lolote kuhusu yeye mwenyewe.
Siku moja nilimuuliza: "Mama! Kwa nini huiombea nafsi yako kama unavyowaombea dua watu wengine? Alisema: "Mwanangu mpenzi! Jirani kwanza kisha nyumbani." Tasbihi na dhikri ambazo ni maarufu kwa jina la Tasbihatu Zahra alizofundishwa na baba yake kipenzi yaani Mtume Muhammad (saw) ni maarufu katika vitabu vya wanazuoni wa Shia na Suni. Tokea awali Bibi Fatima alijifunza elimu na maarifa katika nyumba na ufunuo na wahyi. Elimu na mambo yote ya siri aliyokuwa akifunzwa na baba yake yalikuwa yakiandikwa na mume wake Ali bin Abi Twalib (as). Bibi Fatima alikusanya elimu na maarifa hayo aliyoambiwa na baba yake na kuandikwa na Imam Ali katika tabu kubwa lililokuwa maarufu kwa jina la 'Mas'hafu Fatima'. Bibi huyu mtakatifu alifanya jitihada kubwa za kuwafunza wanawake wa Kiislamu maarifa ya dini hiyo. Aliishika Qur'ani tukufu na kuanisika na kitabu hicho.
Imepokelewa kwamba hata mtumishi wake, Bibi Fidha, ambaye pia alikuwa mwanafunzi mkubwa wa mtukufu huyo, hakuwahi kuzungumza lolote au kujibu swali na maneno ya mtu yeyote bila ya kutumia aya za Qur'ani katika kipindi cha miaka 20. Bibi Fatima al Zahra (as) alikuwa akipitisha sehemu ya usiku kwa ibada na kumtaaradhia Mola Muumba. Swala zake za usiku zilikuwa ndefu kiasi kwamba miguu ya mtukufu huyo ilikuwa ikivimba kwa kusimama sana katika ibada hiyo. Hassan al-Basri aliyefariki dunia mwaka 110 Hijria anasema: "Hakuna mtu katika umma aliyekuwa akifanya ibada kwa wingi, kuipa mgongo dunia na kumcha Mungu zaidi ya Fatima bint Muhammad (as)."
Katika kipindi cha miaka 10 ya serikali ya Bwana Mtume (saw) mjini Madina, kulitokea vita 27 hadi 28 vilivyoongozwa na Mtume mwenyewe na mapigano 35 hadi 90 ambayo Mtume alituma jeshi la Kiislamu kukomboa au kukabiliana na hujuma za maadui katika maeneo mbalimbali. Baadhi ya mapigano hayo yalichukua muda wa miezi miwili hadi mitatu kutokana na kuwa mbali na mji wa Madina, makao makuu ya serikali ya Kiislamu. Katika kipindi kikubwa cha maisha yake ya ndoa na Bibi Fatima (as), Imam Ali bin Abi Twalib (as) alitumia wakati wake mwingi akiwa katika medani za vita na jihadi ya kulinda mipaka ya utawala mchanga wa Kiislamu. Wakati huo mke wake mwaminifu alichukua majukumu yote ya kuendesha nyumba na kulea watoto.
Si hayo tu, bali Bibi Fatima al-Zahra alifanya hima kubwa katika kusaidia pia familia za wapiganaji wengine wa Kiislamu au familia za mashahidi waliouawa katika vita vya jihadi na kupigania dini ya Uislamu. Alikuwa pia akiwahamasisha wanawake wa Kiislamu katika kutibu majeruhi wa vita vya jihadi wa familia na ndugu zao. Imepokelewa kwamba katika vita vya Uhud, Bibi Fatima akiwa pamoja na wanawake wengine, walielekea katika eneo hilo la vita lililoko umbali wa kilomita sita kutoka Madina. Katika vita hivyo Mtume Mtukufu alijeruhiwa vibaya huku Imam Ali bin Abi Twalib aliyekuwa akimhami Mtume wa Mwenyezi Mungu akipata pia majeraha. Bibi Fatima alifanya kazi ya kufuta damu katika kipaji kitukufu cha uso wa Mtume huku Imam Ali bin Abi Twalib akimimina maji kwa kutumia ngao yake ya vita. Baada ya kuona kwamba damu ilikuwa haikatiki na kusimama katika kipaji cha Bwana Mtume, Bibi Fatima alichoma kipande kidogo cha mkeka na akaweka majivu yake kwenye jeraha la Mtume ili kuzuia kuvuja damu kwa wingi.
Wakati wa vita vya Khandaq, Bibi Fatima (as) alimpelekea Mtume (saw) mkate. Mtume aliuliza: "Hiki ni kitu gani?" Bibi Fatima alisema: "Nimepika mkate, lakini moyo wangu haukutulia bila ya kukuletea wewe mkate huu." Mtume alimwambia: "Hiki ndicho chakula cha kwanza kinachoingia mdomoni mwangu tangu siku tatu zilizopita."
Bibi Fatima al Zahra (as) alikuwepo pia katika medani ya Fat'hu Makka, yaani wakati wa kukombolewa mji mtakatifu wa Makka. Bibi Fatima aliendelea kuhudumia Uislamu na Waislamu kwa njia mbalimbali katika kipindi cha uhai wa Mtume Muhammad (saw) na hata katika kipindi kifupi alichoishi baada ya kufariki dunia baba yake kipenzi. Alikuwa na Mtume Muhammad katika hali zote za mashaka, masaibu na hujuma za washirikina na hakusita kujitolea kwa ajili ya kumlinda Mtume wa Mwenyezi Mungu, na Uimamu baada yake hususan Imam Ali bin Abi Twalib. Aliendelea hivyo hadi katika kipindi cha mwishoni mwa uhai wa Mtukufu Mtume. Maradhi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu yalishadidi zaidi katika siku za mwishoni mwa umri wake uliojaa baraka. Bibi Fatima (as) alikuwa daima akiketi kando ya kitanda cha baba yake Mtukufu huku akiangalia sura yake iliyokuwa imejaa nuru ikitokwa na jasho kwa wingi kutokana na homa kali. Bibi Fatima alisikitishwa mno na hali hiyo na daima alikuwa katika hali ya kulia. Mtume Mtukufu pia alishindwa kustahamili kilio na mazonge ya binti yake kipenzi. Alimnong'oneza sikioni na ghafla Bibi Fatima alitulia na kutabasamu. Tabasamu hilo la Bibi Zahra hususan katika kipindi hicho cha kusikitisha liliwashangaza hadhirina. Walimuuliza: "Mtume wa Mwenyezi Mungu amekuambia siri gani?" Alijibu: "Sitatoa siri ya baba yangu maadamu yu hai.
Siri hiyo ilifichuliwa baada ya Mtume Mtukufu (saw) kuaga dunia. Bibi Fatima al Zahra (as) alisema: "Mtume aliniambia: "Utakuwa wa kwanza kati ya Ahli Baiti zangu atakayejiunga nami, na nilifurahi kwa sababu hiyo."
Baada ya kuaga dunia baba yake yaani Mtume Muhammad (saw), Bibi Fatima (as) na Ahlubaiti wa Mtume kwa ujumla walipatwa na masaibu makubwa mno. Hatimaye Bibi huyo mwema ambaye kwa mujibu wa hadithi sahihi ya Mtume Muhammad (saw) ni 'Mbora wa wanawake duniani' alikufa shahidi tarehe 13 Jamadil Awwal mwaka 11 Hijria kwa mujibu wa mapokezi ya baadhi ya wanahistoria akiwa na umri wa miaka 18 tu kwa mujibu wa nukuu mashuhuri zaidi. Aliswaliwa kwa siri na kundi dogo la maumini na kuzikwa usiku wa manane kwa mujibu wasia wake ambapo alitaka watu waliomdhulumu wasishuhudie jeneza na mazishi yake. Sala za salamu za Mwenyezi Mungu, Malaika, na Mitume wake zimshukie Bibi Fatima al Zahra.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.