Kwa mnasaba wa kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa Imam Jawad AS
Siku ya Kumi ya Mwezi wa Rajab inasadifiana na siku ya kuzaliwa Imam Jawad AS. Mwaka 195 Hijria Qamaria katika siku kama hii Imam Mohammad Taqi AS ambaye ni mashuhuri kwa lakabu ya Jawad kwa maana ya mkarimu, alizaliwa katika mji wa Madina. Ni Imamu wa Tisa katika kizazi cha Maimamu 12 kutoka katika Nyumba ya Mtume SAW .
Imam Jawad AS alikuwa mwana wa pekee wa Imam Ridha AS na alichukua jukumu la uimamu kwa muda wa miaka 17 baada ya kuuawa shahidi baba yake. Zama za Uimamu wake zilisadifiana na ukhalifa wa makhalifa wawili madhalimu wa Bani Abbas waliojulikana kama Ma'amun na Mu'tasim.Mtukufu huyo akiwa na umri wa miaka 25 alipewa sumu kwa amri ya Mu'tasim Abbasi na kufa shahidi mjini Baghdad. Katika muda mfupi wa umri wake, kwa vitendo na maneno yake, aliweza kuarifisha mafundisho ya Ahlul Bayt Alaihuma Salam katika ulimwengu na hivyo kuacha kumbukumbu yenye thamani. Sisi hapa kwenye Idhaa tunatoa salamu za kheri na fanaka kwa mnasaba wa siku hii ya maadhimisho ya kuzaliwa Imamu huyu mtukufu na kuwakaribisha kusikiliza maneno machache kuhusu sira na maisha ya mtukufu huyu.
Harakati za kiutamaduni za Imam Jawad ASKila mmoja kati ya Ahul Bayt wa Mtume SAW, katika zama zake, kwa kuzingatia hali ya zama hizo, alijishughulisha na harakati za kiutamaduni na kisiasa na kuwalea wanafunzi. Kwa mfano katika zama za Imam Baqir AS na Imam Sadeq AS kutokana na kuwa walikuwa na mazingira ambayo yalikuwa mazuri kidogo, waliweza kuwa na maelefu ya wanafunzi pamoja na walionukulu hadithi. Lakini katika zama za Imam Jawad AS hadi wakati wa Imam Hassan Askari AS, kipindi kilichodumu kwa muda wa takribani miaka 50, kutokana na mashinikizo ya kisiasa na udhibiti mkali, idadi ya walionukulu hadithi na wanafunzi wao ilikuwa ndogo sana. Kwa hivyo tusishangae iwapo tutasoma historia na kuona kuwa wanukulu hadithi na masahaba zake Imam Jawad AS walikuwa karibu watu 110 na kwa jumla hadithi 250 zimenukuliwa kutoka kwa mtukufu huyo.Hii ni kwa sababu kwa upande mmoja mtukufu huyo alikuwa chini ya mashinikizo makali na udhibiti wa kisiasa na kwa upande wa pili haikupita muda mrefu kabla hajauawa shahidi.Pamoja na hayo, kwa kuzingatia kuwa miongoni mwa idadi ndogo ya masahaba na walionukulu hadithi za mtukufu huyo, kuna shakhsia wakubwa ambao kila mmoja wao alikuwa na nafasi kubwa katika masuala ya kielimu na kifiqhi na wengine wao wameandika vitabu vingi.Tab'an walionukulu hadithi za Imam Jawad AS hawakuwa tu Mashia, bali muhadithina na wanazuoni Masunni pia wamenukulu maarifa na ukweli wa Uislamu kutoka kwa mtukufu huyu.
Midahalo ya Imam Jawad ASImam Jawad AS katika kutekeleza majukumu yake mbele ya Mwenyezi Mungu na kueneza risala, alitumia mbinu mbali mbali.Moja ya mbinu hizo ni kufanya midahalo na wanafikra na hilo lilianza katika siku za kwanza za Uimamu wake.Midahalo hiyo ilikuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha nafasi ya Uimamu wake. Mtukufu huyo alikubali kuingia katika medani ya midahalo ya kielimu kwa sababu mbili.Kwanza ni kuwa, watu wengi hasa wafuasi wa Ahul Bayt AS, kutokana na umri mdogo wa mtukufu huyo, walitaka kupata uhakika kuhusu nafasi yake ya kielimu na kimaanawi. Midahalo hii iliweka wazi nafasi ya juu ya kielimu na kifiqhi ya Imam Jawad AS.Kwa utaratibu huu Ma'amun na Mu'tasim walikumbwa na kashfa baada ya kushindwa njama zao za kumharibia jina Imam. Makhalifa hao wa kiimla waliandaa vikao vya midahalo kati ya Imam na baadhi ya wasomi wakubwa wa zama hizo ili pengine, kwa dhana yao potofu, Imam ashindwe kujibu maswali na nafasi yake ya kielimu na kiroho itiliwe shaka.Sababu nyingine ya Imam Jawad AS kushiriki katika midahalo ilikuwa ni kuwaweka wazi na kuwafichua wasemao uongo. Katika midahalo hiyo, Imam aliweza kuwabainishia Waislamu fadhila bandia za makhalifa wa Kiabbasi.Kuwalea na kuwasomesha wanazuoni ilikuwa moja kati ya mipango ya miongozo na tablighi ya Imam Jawad AS.Mtukufu huyo, sambamba na kulinda chuo kikuu cha kidini (hauza) kilichokuwa kimeanzishwa na Imam Ja'far Sadeq AS, aliweza pia kuwasomesha wanafunzi 270 na kati yao walikuwemo pia wanafunzi wa Imam Reza AS.
Imam Jawad AS alieneza satwa yake maeneo ya mbaliKatika kusambaratisha propaganda chafu za Bani Abbas na kuwasilisha Uislamu wa kweli kwa ummah, Imam Jawad AS aliwatuma wajumbe wake katika maeneo mbali mbali.Wawakilishi hawa walitumwa katika miji muhimu kama vile Ahwaz, Hamedan, Sistan, Rey, Basra, Baghdad, Kufa na Qum kwa lengo la kuwaunganisha wafuasi wa Ahul Bayt na kuweka uhusiano baina yao na Imam.Aidha Imam Jawad AS aliwapa idhini wafuasi wake kupenyeza ushawishi wao ndani ya vyombo vya dola na kuchukua nafasi muhimu.Wale waliotumia fursa ya idhini hiyo vizuri ni pamoja na Mohammad bin Ismail bin Bazi na Ahmad bin Hamzah Qumi ambapo waliweza kupata nafasi muhimu katika serikali kwa lengo la kuhudumia Uislamu na Ahul Bayt AS.Hussein bin Abdullah Nishaburi mtawala wa Sistan na Alya al-Asadi mtawala wa Bahrain walikuwa kati ya masahaba zake Imam Jawad AS na walikuwa wakimtumia Imam Khums za pato lao.
Nasaha za Imam Jawad AS kuhusu urafiki na marafikiImam Jawad AS, sawa na Maimamu wengine, alikuwa na elimu na maarifa halisi ya Tauhid na katika maisha yake, aliweza kuweka wazi sehemu ya bahari yake kubwa ya elimu. Maneno ya mtukufu huyo kuhusu urafiki na muamala na wengine ni moja kati ya kumbukumbu zake zilizojaa thamani.Mwanaadamu ni kiumbe wa kijamii na ili kudhamini mahitaji yake ya kimwili, kiroho na kihisia, daima anahitaji kuwa na uhusiano na wenzake.Wanaadamu wote hutaka kuwa na mtu ambaye akiwa pembeni yao hupata hisia ya utulivu, faraja na furaha. Urafiki na uhusiano na watu wema na wenye elimu ni moja ya sababu za saada na mafanikio ya mwanaadamu. Kuwa na marafiki wema na wanaofaa kunaweza kumfanya mwanaadamu apite vizuri katika vipindi vigumu vya maisha na afikie malengo yake. Mafundisho ya kidini na kisaikolojia yanaonyesha kuwa mwanaadamu ambaye hana neema ya kuwa na urafiki na uhusiano na wenzake huwa mpweke. Mtu kama huyu hukumbwa na huzuni na hata yamkini akakosa ustawi wa kiakili.Imam Jawad AS anasema hivi kuhusu taathira ya kiroho na kisaikolojia ya urafiki: 'Kutembelea na kuwa na uhusiano na marafiki hupelekea kuwepo furaha na huzidisha akili hata kama muda wa kuonana utakuwa mfupi.' (Muntaha al-Amal Juz.2 Uk. 229.)
Kwa mtazamo wa Imam Jawad AS, watu huhesabiwa kuwa marafiki wa kweli wakati wanapohifadhi siri na kumsaidia mtu anapokuwa na masaibu na mushkili katika maisha na kuwasaidia wengine katika kufuata njia ya dini na kuinua kiwango cha maarifa yao. Kwa hivyo watu wanapaswa kuwa waangalifu kuhusu wanaowachagua kuwa marafiki zao na kuhakikisha kuwa marafiki ni wale tu wanaostahiki baraka za Mwenyezi Mungu na wasiwe wamefanya jambo linalomkasirisha Mwenyezi Mungu. Kwa hakika kuwa rafiki na mja mwema ni sawa na kuelekea katika rehma ya Mwenyezi Mungu.Mkabala wa hilo, urafiki na mwanaadamu aliyechafuka kimaadili na kupotea ni jambo ambalo humuweka mtu mbali na watu wema na kumuweka katika safu ya watu waovu. Mtu kama huyu huwa hasikii tena nasaha za watu wema na hata huwa na dhana mbaya kuhusu watu hao wema. Ni kwa sababu hii ndio Imam Jawad AS akasema: 'Kukaa na watu wabaya humfanya mtu kuwa na mtazamo mbaya kuhusu watu wema.' Amal Uk 531.Urafiki na maingiliano na wengine kwa sababu ya Mwenyezi Mungu pasina na kuwa na matamanio ya kidunia huwa jambo la kudumu kwani msingi wake ni kumridhisha na kumfurahisha Mwenyezi Mungu. Aina hii ya urafiki huandaa mazingira ya kustawi na kuinuka hadhi ya watu katika jamii.Imam Jawad AS anasema hivi kuhusu urafiki unaofaa: 'Kila mtu ambaye atapata rafiki kwa njia ya Mwenyezi Mungu, atapata nyumba peponi.' (Mawsuat al Imam al Jawad Juz. 2 Uk. 352.) Kuchagua rafiki mzuri ni moja ya nukta za kimsingi kabisa katika mafanikio ya mwanaadamu katika nyuga mbali mbali za maisha. Kupuuza na kutolipa uzito suala hili yamkini kukamletea mtu matatizo na maangamizi.Mwislamu anapaswa kuimarisha uhusiano wake wa kijamii na kutembeleana na marafiki na ndugu wa kidini kwani kujitenga na watu huwa na athari mbaya. Kukutana na kuamiliana vizuri na wanaadamu wengine ni kama mvua ya machipuo ambayo huleta mazingira mapya na ya kijani kibichi. Katika sehemu nyingine ya nasaha zake kuhusu suala la urafiki, Imam Jawad AS anasema: 'Mahaba ya marafiki huvutiwa kwa sababu tatu: 'Insafu katika muamala na mkutano, kushikamana nao wakati wa shida na furaha na kuwa na moyo msafi.' Biharul Anwar Juz. 75 Uk. 82.