Kwa mnasaba wa kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa Imam Ali AS
Bismillahir Rahmanir Rahim. Karibuni wasikilizaji wapenzi katika kipindi hiki maalumu ambacho tumekuandalieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Ali bin Abi Talib AS. Siku hii kwa hapa nchini Iran inajulikana pia kwa jina la Siku ya Baba.
Ilikuwa ni miaka 23 kabla ya Hijra ya Bwana Mtume Muhammad (rehema za Allah ziwe juu yake na Aal zake) kutoka Makka kwenda Madina na ilikuwa ni mwaka wa thelathini tangu mwaka wa ndovu, anga ya ardhi ya Makka katika usiku wa siku hiyo iling'ara kwa nyota zilizotandawaa mbinguni. Nuru ya mbalamwezi iliifanya Nyumba Tukufu ya Allah ya al Kaaba iwe na sura na mandhari ya aina yake. Lahadha yoyote ile baada ya wakati huo alitarajiwa kuwasili mgeni wa Mwenyezi Mungu na hujja Wake katika ardhi. Maumbo yote ya mbinguni na angani yaliweka ahadi kuwa yataifanya kesho ya siku hiyo kuwa siku adhimu katika kumbukumbu ya historia. Jua lilipochomoza, siku ya Ijumaa ya tarehe 13 Rajab, ambayo ndiyo siku iliyoahidiwa, iliwadia.Watu wote walimwona Fatima bint Asad wakati alipoizuru Nyumba ya Allah ya al Kaaba jinsi alivyokuwa akinong'ona na Mola wake kwa kusema: " Ee Mola wangu, mimi nimekuamini Wewe, na nimeyaamini yale yaliyokuja kutoka kwako, kupitia Mitume wako na Vitabu vyako; na ninasadikisha maneno ya babu yangu Ibrahim, na ni yeye ndiye aliyeijenga nyumba hii ya kale. Ninakuomba kwa jaha ya yule aliyeijenga nyumba hii, na kwa jaha ya kizazi hiki kilichomo tumboni mwangu, uniwezeshe kujifungua kwa wepesi."
Kufumba na kufumbua na kwa namna ya kimuujiza, Fatima bint Asad aliingia ndani ya al Kaaba; watu wote walishangaa na kupigwa na butwaa. Na naam, katika lahadha hiyo alifumbua jicho na kuja duniani Ali bin Abi Talib, mzaliwa wa fakhari na adhama wa al Kaaba, chemchemu ya haki na uadilifu na johari na mfunguzi wa silsili ya Maimam thenashara walioahidiwa. Kwa niaba ya Radio Tehran, tunakupeni mkono wa kheri na baraka wasikilizaji wapenzi kwa mnasaba huu wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa mlinganiaji na mnadi wa uadilifu, Bwana wa wampwekeshao Allah na ruwaza ya wachamungu, Imam Ali bin Talib AS.****Wakati Imam Ali AS alipozaliwa, umri wa Bwana Mtume (rehema za Allah ziwe juu yake na Aal zake) haukuwa umepindukia zaidi ya miaka thelathini. Miaka michache baadaye, Mtukufu huyo alitoa shauri kwa Ami yake Abu Talib la kumsaidia ulezi wa Ali kutokana na aila na familia kubwa aliyokuwa nayo ami yake huyo ili kumpunguzia mzigo mzito wa gharama za kukidhi mahitaji ya familia yake. Abu Talib aliafiki ushauri huo, na kuanzia kipindi cha utotoni mwake, Ali AS akawa pamoja na Bwana Mtume katika kipindi chote cha umri wake. Ali alikuwa mtu wa kwanza kumwamini Bwana Mtume. Alikuwa mpwekeshaji wa Allah tangu udogoni mwake na hakuwahi hata mara moja kuabudu masanamu kama walivyokuwa watu wengi wa zama hizo.Baada ya Mtume Muhammad SAW kubaathiwa na kupewa Utume, kwa muda wa miaka mitatu alikuwa akiwatangazia watu dini kwa siri, na hakuwa akifanya hivyo ila kwa wale ambao alihisi kuna uwezekano wa wao kuukubali mwito wa Uislamu. Alifanya hivyo kwa amri ya Mwenyezi Mungu aliposema: "Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe." Baada ya kupita miaka mitatu, Malaika wa Wahyi Jibril AS alishuka, na kwa amri ya Mola akamfikishia Bwana Mtume ujumbe wa kumtaka aitangaze dini hadharani na kuanzia kwa jamaa na watu wake wa karibu. Bwana Mtume SAW alitekeleza amri hiyo ya Allah kwa kuwaalika shakhsia na watu wakubwa wakubwa wa ukoo wake wa Bani Hashim na akaanza kwa kuwaambia: "Hakuna mtu yeyote duniani aliyewaletea watu wake kitu bora kama kile nilichokuleteeni mimi. Mimi nimekuleteeni kheri yenu ya dunia na Akhera. Mola wangu ameniamuru nikulinganieni Tauhidi na kukufikishieni wito wake wa kumwabudu Yeye Mola Mpweke. Nani kati yenu atakayenisaidia katika jambo hili ili awe ndugu yangu, wasii wangu na mwakilishi wangu kwenu?"Katika lahadha hiyo kimya kizito kilitanda katika anga ya majlisi hiyo na watu wote wakawa wameinamisha vichwa vyao chini wakiwa wamezama kwenye mawazo na tafakuri. Ghafla Ali AS alivunja kimya hicho, akainuka na kumuelekea Bwana Mtume na kumwambia:" Yaa Rasulallah, mimi nitakusaidia katika jambo hili". Hapo Bwana Mtume akamtaka Ali akae kitako, na kwa mara nyengine akarudia tena maneno yake.
Alifanya hivyo mara tatu pasina kupata jibu lolote kutoka kwa watu, na hivyo mara ya mwisho aliuweka mkono wake juu ya mkono wa Ali na kusema:" Enyi watu wangu na jamaa zangu! Ali ni ndugu, wasii na khalifa wangu kwenu". Na kwa njia hiyo wasii wa kwanza wa Bwana Mtume akaainishwa na kutangazwa na yeye mwenyewe Mtume wa mwisho wa Allah.Katika siku hiyo moja Bwana Mtume SAW aliutangaza Utume wake na Uimamu wa Ali AS. Na kwa njia hiyo akawa amewatambulisha watu wote kuwa daraja mbili hizo hazitenganiki, na Uimamu, ni mkamilishaji wa risala ya Utume.*******Katika mwaka wa 13 tangu alipobaathiwa Nabii Muhammad SAW, wakati watu wa Yathrib yaani Madina walipombai Mtukufu huyo na kuahidi kumlinda na kumhami, wakubwa wa Makureishi walihisi hatari inawakabili, hivyo wakaamua kukutana na kufikiria la kufanya. Baada ya majadiliano marefu waliafikiana katika kikao chao hicho kuwa wamuue Bwana Mtume. Lakini kumuua Bwana Mtume halikuwa jambo rahisi, kwani kufanya hivyo kungezusha vita na kuwafanya Bani Hashim watake kulipiza kisasi cha damu ya mtu wao. Kwa sababu hiyo wakaamua kwamba kila kabila la Kikureishi litoe kijana mmoja, kisha vijana hao kwa pamoja waende nyumbani kwa Bwana Mtume wakati wa usiku na kumshambulia kitandani alipolala kwa kumkatakata kwa panga zao. Kwa kufanya hivyo Bani Hashim hawatokuwa na uwezo wa kukabiliana na makabila yote, na kwa hivyo watalazimika kukubali fidia tu ya damu ya mtu wao iliyomwagwa, na suala litaishia hapo.Lakini Makureishi waliyapanga hayo bila kuwa na habari kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu alishampa Mtume wake habari ya njama yao hiyo ovu na kumuamuru ahame Makka na kuhajiri Madina. Pamoja na hayo ili kuizima njama hiyo ya Makureishi kwa kuwababaisha wasiweze kung'amua habari ya Hijra ya Bwana Mtume, alihitajika mtu wa kujitolea mhanga nafsi yake, ambaye angelala kwenye kitanda cha Mtukufu huyo katika usiku huo, ili pale kundi la vijana wa Kikureishi litakapotaka kuivamia nyumba ya Bwana Mtume lidhani kwamba yeye bado hajaondoka nyumbani kwake na kwa njia hiyo Hijra ya Mtukufu huyo kuelekea Madina ifanyike bila kizuizi. Mtu huyo wa kuwa tayari kujitolea mhanga roho yake hakuwa mwengine ghairi ya Ali AS.Wakati kundi la vijana wa Kikureishi liliposhikilia panga mikononi mwao na kuvamia nyumba ya Mtume wa Allah, baina ya Ali na mauti ya kuuawa shahidi, yalikuwa ni masafa ya pua na mdomo tu, lakini ghafla wauaji hao wakatanabahi kuwa ni Ali ndiye aliyekuwa amelala kitandani pa Mtume. Qur'ani Tukufu imekuzungumzia kujitolea mhanga huko kwa Ali AS katika aya ya 207 ya Suratul Baqaraha kwa kusema: Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.
Maisha ya Ali bin Abi Talib AS tokea kipindi cha Hijra ya Bwana Mtume SAW hadi kuaga dunia mtukufu huyo yalitawaliwa na matukio mengi mno hususan yale yaliyoakisi moyo mkubwa wa kujitolea kwake mhanga katika medani za vita vya Jihadi. Baada ya ushindi wa Waislamu katika vita vya Badr, Makureishi walikuwa wameemewa na kufadhaika mno kutokana na taathira ya kushindwa katika vita hivyo, na kwa hivyo waliamua kujiandaa kwa jeshi kubwa na kujizatiti kwa zana na silaha chungu nzima katika vita vilivyofuatia vya Uhud, ili kulipiza kisasi cha kushindwa vibaya katika vita vya Badr na kisasi cha watu wao waliouawa katika vita hivyo. Awali, hata katika vita hivyo vya Uhud pia Makureishi walikuwa wameshashindwa, lakini wakati Waislamu walipokuwa wameshughulika kukusanya ngawira, wapiganaji wa Kiislamu waliopewa jukumu la kulinda ngome katika sehemu ya juu ya mlima Uhud na ambao walisisitizwa mno na Bwana Mtume wasije wakaondoka mahala hapo katika hali yoyote ile kwa kuona wenzao wameshinda au wanashindwa, walighafilika na agizo hilo la Mtume na badala yake wakakimbilia kwenye ngawira.Wakati huo, Khalid ibn Walid mmoja wa makamanda wa jeshi la makafiri wa Kikureish aliyekuwa akivizia na kungojea fursa kama hiyo aliliongoza jeshi la wapanda farasi kupitia kwenye ngome iliyoachwa tupu na wapiganaji wa jeshi la Waislamu na kuanza kuwashambulia Waislamu kutokea nyuma. Katika hali hiyo ya tafrani na hamkani maadui wakaeneza uvumi pia kwamba Bwana Mtume ameuawa. Waislamu wengi walirudi nyuma, wakatawanyika na kusambaratika ukiachia wachache walioendelea kubaki pamoja na Mtume wa Allah. Ni katika lahadha hiyo ndipo ilipoonekana kwa uwazi kabisa nafasi na mchango mkubwa wa Ali AS.Kwa ushujaa usio na mfano Ali alipambana kwa upanga wake bega kwa bega na Bwana Mtume huku akimlinda Mtukufu huyo kutokea kila upande mbele ya mashambalio ya mtawalia ya washirikina. Ibn Athir, mwanahistoria, mwanafasihi na mpokezi maarufu wa hadithi, ameandika katika kitabu chake kiitwacho 'al Kaamil fit Taarikh' kwamba: "Mtume SAW aliliona kundi la washirikina waliokuwa wameazimia kufanya shambulio; akamuamuru Ali awashambulie. Kwa amri ya Mtume, Ali aliwashambulia washirikina hao, na kutokana na kuwaua kadhaa miongoni mwao walitawanyika na kusambaratika. Kisha mara Mtume akaliona kundi jengine, na hapo akamuamuru Ali alishambulie, na Ali akalishambulia na kuwaua na kuwasambaratisha. Katika lahadha hiyo Malaika wa Wahyi alimuelekea Bwana Mtume na kumwambia: "Huu ulioonyeshwa na Ali, ni upeo wa juu kabisa wa kujitolea mhanga". Naye Bwana Mtume akajibu kwa kusema:" Yeye anatokana na mimi, na mimi ninatokana na yeye". Katika lahadha hiyo ikasikika sauti kutoka mbinguni ikinadi:
لا فَتى اِلاّ عَلِىّ، لا سَیفَ اِلاّ ذُو الفَقار
"Hakuna shababi mithili ya Ali, wala hakuna upanga mithili ya dhulfiqar"
Mbali na ushujaa huo mkubwa wa Imam Ali AS katika vita vya Uhud, ushujaa wake ulionekana pia katika vita vyote alivyoshiriki mtukufu huyo. Imam Ali alikuwa anajulikana pia kwa jina la 'Faatihu Khaybar', yaani mtu aliyewezesha kupatikana ushindi na kukombolewa ngome ya Khaybar na kisa cha kukombolewa ngome hiyo ya Khaybar ni maarufu.
******
Wapenzi wasikilizaji bila ya shaka kuna mengi mno ya kueleza na kusimulia kuhusiana na jinsi Imam Ali AS alivyokuwa pamoja na bega kwa bega na Bwana Mtume, katika kipindi chote cha maisha ya mtukufu huyo na mengi aliyoyafanya kujitolea kwa ajili ya Uislamu, lakini tumelazimika kuzungumzia haya machache tu kutokana na muda uliotengewa Makala yetu ya leo. Kwa mara nyengine tena tunaitumia fursa hii kukukupeni mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba huu adhimu wa kukumbuka siku ya kuzaliwa mzaliwa wa ndani ya Alkaaba, Imam wa Mashariki na Magharibi, Simba wa Mwenyezi Mungu mwenye kushinda, Imam Ali AS. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.