May 28, 2018 12:14 UTC
  • Mwaliko wa Ramadhani

Waashiki wa Qur'ani Tukufu hukikaribia zaidi kitabu hiki cha mbinguni katika mwezi huu mtukufu na kuzipa nyoyo zao msisimuko na uhai mpya kwa kusoma, kujifunza na kudiriki maarifa yake.

Kati ya misimu yote ya mwaka, msimu wa machipuo ndio msimu unaovutia zaidi kutokana na kudhihiri mandhari ya kuvutia kimaumbile na hasa uhai mpya unaojitokeza kwenye mimea iliyopukutika majani katika msimu wa kabla ya hapo, ambayo hugeuka na kuwa ya kijani kibichi katika msimu huu. Msimu huu hubeba ujumbe wa upendo, ustawi na uhai mpya na ndio maana unapowadia, nyoyo husisimka na kupata maarifa zaidi. Katika mazingira ya kuvutia ya msimu wa machipuo, wanadamu huhisi kwa karibu na kukumbuka zaidi rehema na upendo wa Mwenyezi Mungu kwao kuliko wakati mwingine wowote. Wanazuoni na wajuzi wa masuala ya kimaanawi pia wanasema kuwa hakuna hakika inayodhihirisha rehema, upendo na huruma ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake kama kitabu kitakatifu cha Qur'ani. Wanasema hakuna kitu kingine chochote kinachosisimua, kuliwaza, kufariji na kulainisha nyoyo kama kusikiliza na kusoma ujumbe wa Qur'ani Tukufu. Kama ambavyo jua huangaza na kutoa uhai mpya kwa viumbe walioko duniani kupitia joto na mwangaza wake baada ya kupita usiku wenye giza kubwa, Qur'ani pia huchangamsha na kutoa uhai mpya kwa nyoyo zilizochoka, kupooza na kufa. Hivyo Qur'ani ni msimo wa machipuo kwa ajili ya nyoyo nao mwezi wa Ramadhani ni msimu wa machipuo kwa ajili ya Qur'ani. Imam Swadiq (as) anasema: 'Kila kitu kina msimu wake wa machipuo na msimu wa machipuo wa Qur'ani ni mwezi wa Ramadhani.' Ni kwa kutilia maaanani ukweli kwamba sote tumealikwa kuwa wageni wa Mwenyezi Mungu katika mwezi huu mtukufu, ndipo tunaweza kudiriki vyema mvuto, hakika na thamani za aina yake za mwezi huu mtukufu.

Kama ambavyo msimu wa machipuo ni msimu wa mazingira kupata uhai mpya, pia usomaji na uazingatia wa Qur'ani Tukufu katika mwezi wa Ramadhani ni wakati wa kupulizwa pumzi na uhai mpya katika nyoyo za wanadamu. Hii ni kwa sababu maumbile ya mwanadamu yanaenda sambamba na  Qur'ani pamoja na Aya zake tukufu. Ni wazi kuwa Aya hizo hutayarisha, kushawishi na kuwavutia wanadamu kuelekea utiifu wa Muumba wa mbingu na ardhi. Qur'ani yenyewe inazungumzia mvuto huo maalumu wa kimaanawi kwa kusema katika sehemu ya Aya ya 23 ya Surat az-Zumar: Mwenyezi Mungu ameteremsha hadithi nzuri kabisa, Kitabu chenye kufanana na kukaririwa; husisimka kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola Mlezi. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu.


Ni kutokana na ukweli huo ndipo Hadithi zikaitaja Qur'ani kuwa ni msimu wa machipuo ya nyoyo.

Qur'ani Tukufu ni muujiza wa Mwenyezi Mungu na waraka wa kudumu milele wa Uislamu. Licha ya kuwepo njama mbalimbali za maadui dhidi ya dini hii tukufu, lakini kitabu hiki cha mbinguni kimesalimika na njama zote hizo na kuendelea kuongoza na kuwalinda wanadamu dhidi ya upotovu. Sifa maalumu ya Qur'ani ni kuongoza jamii ya mwanadamu. Tokea ilipoteremshwa, Qur'ani imeweza kuziongoza nyoyo safi na kulea jamii zenye maadili bora kutokana na jamii za watu waliokuwa wamepotea njia na kuwa na tabia za kinyama. Kwa kuteremsha kitabu hiki, Mwenyezi Mungu alitimiza hoja yake kwa wanadamu kwa kuwathibitishia kuwa hakuna kitabu kingine kilicho kikamilifu kama hicho ambacho kinaweza kuwakidhia haja zao na kuwatatulia matatizo katika maisha yao ya kila siku. Bila shaka muundo na maana ya Aya za Qur'ani inabainisha wazi kwamba kitabu hicho hakikuandikwa na mwanadmu bali ni muujiza wa kudumu ambao uko nje ya uwezo wa mwanadamu. Kupita zaidi ya karne 14 za  kuwepo hai Uislamu ulimwenguni kunathibitisha wazi hakika kwamba, kwa kuwa na mantiki sahihi ya kielimu, maarifa ya kina na mafundisho ya kimaadili na kielimu, Qur'ani ndicho kitabu bora zaidi kwa ajili ya kuendesha maisha ya mwanadamu. Ni katika kivuli cha mafundisho na miongozo ya kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu ndipo daima kikawa na sura ya kung'ara na mvuto maalumu wa haki na hivyo kuendelea kuwavutia wengi duniani. Katika kukiarifisha kitabu hiki chenye thamani, Mwenyezi Mungu mwenyewe anasema katika sehemu ya  Aya za 41 na 42 za Surat Fussilat: ....bila ya shaka ni Kitabu chenye nguvu na utukufu. Hautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake. Kimeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa.


Ujumbe wa Qur'ani ni wa moja kwa moja na uko wazi kwa ajili ya watu wote. Kwa kuzingatia mafundisho yake ya msingi ya kutenda wema, kuzingatia maadili bora, kujitenga na maovu, kuimarisha upendo na amani na kutotumia mabavu, ni wazi kuwa kitabu hiki cha mbinguni kinaweza kuchukuliwa kuwa nguzo na msingi muhimu wa kuendeshea maisha ya wanadamu katika nyanja zote za maisha binafsi, ya kijamii, kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa.  Ni kutokana na ukweli huo ndipo Mtume Mtukufu (saw) akatunasihi tuikimbilie Qur'ani kila tunapokabiliwa na matatizo tofauti maishani. Ni wazi kuwa kusoma Qur'ami katika mwezi mtukufu wa Ramadhani kuna sifa na thamani maalumu ambazo hazipatikani katika miezi mingine ya kawaida. Mwezi huu humuandalia mwanadamu mazingira safi ya kuweza kuvuta pumzi mpya ya uhai wa kimaanawi na hivyo kumkurubisha zaidi kwa Mola wake. Njia bora zaidi ya kufikia lengo hilo ni kupitia Qur'ani Tukufu. Kuhusiana na suala hilo Mtume Mtukufu (saw) anasema katika hotuba yake ya mwisho aliyoitoa katika mwezi wa Shaaban kabla ya kuingia mwezi wa Ramadhani kuwa kusoma Aya moja tu ya Qur'ani katika mwezi huu ni sawa na kusoma Qur'ani nzima katika miezi mingine ya kawaida.

Mwezi wa Ramadhani ni mwezi ambao ndani yake kiliteremshwa kitabu kitakatifu cha Qur'ani. Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 185 ya Surat al-Baqarah: Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi.

Kuteremshwa Qur'ani katika mwezi wa Ramadhani kunabainisha wazi sifa maalumu za mwezi huu ambao umetoa fursa maalumu za kuwezesha kitabu hicho kitakatifu kuteremshwa humo. Kama ambavyo vitabu vingine vyote vya mbinguni pia viliteremshwa katika mwezi huu mtukufu. Imam Swadiq (as) amenukuliwa katika Hadithi akisema: 'Torati iliteremka usiku wa sita katika mwezi wa Ramadhani, Injili iliteremka usiku wa kumi na mbili wa mwezi wa Ramadhani, Zaburi iliteremka usiku wa kumi na nane wa mwezi wa Ramadhani nayo Qur'ani ikateremshwa usiku wa Leilatul Qadr.' Ni kutokana na hilo ndipo Imam Ali (as) akasema katika hotuba yake ya 110 katika Nahjul Balagha: 'Jifundisheni Qur'ani kwa sababu ndiyo hadithi nzuri kabisa na jitahidini kuifahamu kwa kuwa ni msimu wa machipuo ya nyoyo.'

Sehemu kubwa ya baraka za mwezi wa Ramadhani inafungamana moja kwa moja na utukufu wa Qur'ani. Katika mwezi huu, wanaofunga saumu hupanda mbegu zenye nuru za Qur'ani kwenye nyoyo zao ili ziweze kumea na kustawi katika kivuli cha Aya za kitabu hicho kitakatifu. Sauti za usomaji Qur'ani misikitini, nyumbani na mitaani hupamba mwei huu na kuongeza maradufu umaanawi wake. Kwa hakika manufaa ya mwezi huu hupatikana katika kivuli cha kutafakari na kuizingatia kwa makini Qur'ani Tukufu.

Eeh Mwenyezi Mungu! Mswalie Mtume Muhammad na Aali zake na utufanye tuwe miongoni mwa watu wanaoshikamana na kamba ya Qur'ani, kupata utulivu katika kivuli chake na kuongozwa na miale yake inayong'ara ya wongofu.

 

Tags