Kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Bibi Zainab AS
(last modified Tue, 31 Dec 2019 07:12:10 GMT )
Dec 31, 2019 07:12 UTC
  • Kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Bibi Zainab AS

Bibi Zainab (sa) alijipamba kwa sifa na fadhila nyingi nzuri na za kupigiwa mfano kadiri kwamba sifa hizo bora zilimfanya kuwa bibi mwema aliyepaswa kuigwa na watu wengine. Alikuwa na tabia, fadhila na maadili mema mengi yaliyofanya kuwa na sifa za kipekee miongoni mwa watu na jamii aliyoishi ndani yake.

Leo ni siku kuu ya kuzaliwa Bibi wa Karbalaa, Zainab (sa). Huyu ni yule yule bibi na mtukufu ambaye hata baada ya kuuawa kinyama wapendwa wa familia yake ambao ni Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw) lakini hakufuata njia nyingine isipokuwa ya kusubiri na kudumisha mapambano ya ndugu yake Imam Hussein (as). Huyu ni bibi ambaye alikuwa akizungumziwa sana na watu kutokana na kipawa chake kikubwa cha elimu na busara na jina lake limetajwa katika matukio muhimu ya historia ya Kiislamu. Zainab (sa) alikulia katika mazingira ya malezi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) na Uimamu wa baba yake Ali (as). Babu yake ni Mtume Mtukufu (saw), baba yake ni Imam Ali (as) mfano uliokamilika wa mwanadamu, na mama yake ni Fatwimat az-Zahra (as), dhihirisho halisi la umaasumu, utakasifu, subira na mapambano. Zainab alilelewa na kukulia katika mazingira hayo ya utakatifu na nuru ya umaanawi pamoja na mafundisho ya mbinguni. Huku tukikupeni mkono wa pongezi na hongera ndugu Waislamu, kwa mnasaba huu adhimu wa kusherehekea uzawa wa bibi huyu mtukufu wa kizazi cha Nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), tunakukaribisheni muwe pamoja nasi katika dakika hizi chache za kuzungumzia kwa ufupi maisha ya mtukufu huyu, karibuni.


Bibi Zainab (sa) alizaliwa katika nyumba ya Utume na Wahyi mwaka wa 5 Hijiria. Baada ya kujaaliwa bintu huyo mtukufu (sa), Mama yake Bibi Fatwimah na mumewe Ali (as) walifurahi sana, na kumwomba Mtume (saw) amchagulie jina mjukuu wake huyo mpendwa. Kwanza Mtume alimkumbatia kifuani kwake mjukuu wake huyo na baada ya kumtazama akawa anatokwa na machozi ya furaha na kumuadhinia masikioni na kisha akampa jina la 'Zainab.' Tokea utotoni, Zainab Kubra (sa) alipendwa sana na Mtume pamoja na watu wengine wa familia yake. Ali (as) alikuwa akimketisha miguuni kwake na kuzungumza naye kwa mapenzi makubwa. Mama yake, Bibi Fatwimah (as) pia alikuwa akimuonyesha mapenzi makubwa ya mama na kumfundisha masomo ya dini kwa huruma kubwa. Inasemekana kuwa siku moja Imam Ali alimuomba binti yake huyo mdogo atamke neno 'moja', naye akawa amelitamka lakini alipomtaka atamke neno 'mbili' akawa amesita na kukaa kimya. Imam Ali (as) akamuuliza sababu ya kimya hicho naye akajibu kwa kumwambia kwamba ulimi unaotamka 'moja; huwa hautamki 'mbili', hapo baba yake akawa ameshangazwa sana na maneno hayo na kutambua undani na kina cha Tauhidi na upweke wa Mwenyezi Mungu aliokuwa nao binti yake katika umri huo mdogo. Alifahamu vyema makusudio ya binti yake huyo. Kwa msingi huo ni wazi kuwa Bibi Zainab alimzingatia sana Mwenyezi Mungu tokea akiwa na umri mdogo wa utotoni.

Moja ya sifa nyingine muhimu za Bibi Zainab ni ushajaa na ujasiri wake wa kupigiwa mfano. Wataalamu na wanazuoni wa masuala ya maadili na akhlaki wanaugawa ushujaa katika makundi na daraja tatu. Daraja ya kwanza ni kutowaogopa watu na hasa wanaotumia nguvu na mabavu dhidi ya wenzao. Daraja ya pili na ambayo ni ya juu zaidi kuliko ya kwanza ni kudhibiti matamanio na matakwa ya nafsi inayoamrisha mabaya. Ama daraja ya tatu na ambayo ni ya juu zaidi kuliko ya kwanza na ya pili ni ushujaa unaomuwezesha mwanadamu kushinda misiba, matatizo, machungu na majaribio ya zama. Bibi Zainab alifikia kilele cha ushujaa huo wote.

Tangu utotoni, Zainab Kubra (sa) alishuhudia kwa karibu namna wazazi wake wawili, Imam Ali na Fatwimat Az-Zajra (as) walivyokuwa wakijishughulisha na ibada na swala za usiku. Yeye pia alikuwa miongoni mwa watu waliosimamisha swala hizo za usiku, kuomba dua na kunong'onezana na Mwenyezi Mungu. Kama walivyokuwa watu wa familia yake, Bibi Zainab (sa) alijifunza vizuri usomaji na kuilewa vyema Qur'ani, ambapo alitambua vyema kwamba lengo la kuumbwa mwanadamu ni kumuwezesha kufikia kilele cha ukamilifu na kumcha Mwenyezi Mungu, kama inavyosema Aya ya 56 ya Surat adh-Dhariyaat: Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.

Bibi Zainab (sa), alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na hamu kubwa ya ibada na uchaji Mungu na wala hakuacha kutekeleza ibada hiyo hata katika mazingira mahumu zaidi maishani mwake. Bibi huyo ambaye alikuwa amefikia kilele cha ibada na uchaji Mungu alikuwa na mfungamano na uhusiano maalumu wa ikhlasi na Muumba wake. Kilelel hicho cha ibada ya Bibi Zainab kinadhihirika wazi kupitia maneno aliyoaambiwa na kaka yake Imam Hussein (as). Imam Hussein ambaye ni maasumu, asiyetenda dhambi na aliye na fadhila maalumu mbele ya Mwenyezi Mungu, alipokuwa anaandoka kwenda kupambana na maadui wa Uislamu katika jangwa la Karbala, alimwambia dada yake huyo mcha-Mungu: 'Dada yangu mpendwa! Ninakuomba usitusahau kwenye swala zako za usiku, na tuombee dua kwenye swala hizo."

Imam Sajjad (as) pia anasema hivi kuhusiana na Zainab (sa): 'Hakika Shangazi yangu Zainab akiwa njiani kutoka Kufa kuelekea Sham alikuwa akiswali swala zake zote za wajibu na za mustahab na akiswali baadhi ya swala hizo katika baadhi ya nyumba akiwa ameketi chini kutokana na makali ya njaa na udhaifu.'


Sifa nyingine ya Bibi Zainab al-Kubra (sa) ni heshima na usafi wa kimaadili. Ni wazi kuwa sifa hii ndio kito cha thamani kubwa zaidi kwa mwanamke anyejiheshimu na kujali shakhsia yake. Zainab alijifunza sifa na somo hili muhimu kutoka kwa mama yake mpendwa Bibi Fatwimah (as). Zainab (sa) alilinda sifa hii muhimu hata katika mazingira magumu zaidi maishani. Katika kipindi cha kukamatwa mateka na akiwa njiani kutoka Karbala kuelekea Sham, alilinda hijabu yake kwa nguvu zake zote na hata mara nyingine alikuwa akiufunika uso wake kwa mkono wake ili abakie salama mebele ya wimbi la macho ya watu wasiopasa kumtazama. Kuhusiana na suala hilo, Dakta Aisha bint as-Shati' mwandishi wa kike wa Ahlu Suna anasema kuhusiana na maisha ya Bibi Zainab kwamba wanahistoria wengi wameshindwa kuzungumzia kwa undani maisha ya bibi huyo mtukufu kwa sababu alitumia umri wake mwingi akiwa ndani ya nyumba na kwamba inasikitisha kuona kuwa baada ya kuishi kwa miaka mingi katika hali hiyo, ni msiba wa Karbala ndio ulimtoa nje na kuonekana na watu.

Ni masikitiko makubwa kuona kwamba katika dunia ya leo, wakoloni mambo-leo na wanaohujumu utamaduni safi wa mwanadamu wamelenga heshima na utu wa mwanamke ili kuielekeza jamii ya mwanadamu kwenye ufuska na upuuzaji wa maadili ya kidini. Wanataka kufikia malengo yao ya kishetani kwa kuondoa haya na heshima kwenye maisha ya mwanamke na kueneza ufuska katika jamii. Wametambua kwamba iwapo wanataka kuharibu dini, wanapasa kuondoa haya, heshima na maadili katika utu wa wanawake. Ili kukabiliana na hali hiyo, wanawake wanapasa kujifunza soma la haya, heshima na utu wao kutoka kwa Bibi Zainab (sa), mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Nam, mwanamke anaweza kuwa msomi mkubwa, arif, mwanasiasa na mtu aliye na heshima na taathira kubwa katika jamii lakini wakati huohuo akawa amelinda heshima, maadili na utu wake katika jamii hiyo, kama alivyofanya Bibi Zainab (sa).

Wakati Zainab (sa) alipofikia umri wa kuolewa, aliolewa na Abdallah bin Ja'ffar, mtoto wa ami yake. Abdallah alikuwa na nafasi maalumu na asili safi ya kifamilia. Baba yake alikuwa Ja'ffar bin Abi Talib, mtoto wa ami ya Mtume (saw) na ndugu yake Imam Ali (as), ambaye aliuawa shahidi katika vita vya Mu'tah. Mama yake Abdallah alikuwa Asma bint Umais, mwanamke aliyejitolea kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu na ambaye kwa miaka mingi alivumilia machungu ya kuwa mbali na ardhi na watu wake baada ya kuhajiri na kuhamia katika nchi ya Uhabeshi (Ethiopia ya leo). Baada ya kuuawa shahidi mume wake, alivumilia matizo yaliyotokana na hali hiyo na hivyo kuonyesha sifa yake nyingine ya uvumilifu na ukakamavu mbele ya machungu. Abdalla bin Ja'ffar alilelewa na kukulia katika mazingira ya wazazi watukufu kama hao waliokuwa na sifa nzuri za kupigiwa mfano, kuhusiana na masuala ya kumcha na kumuogopa Mwenyezi Mungu. Zainab ambaye alikuwa na fikra ya hali ya juu, wakati wa kuolewa kwake na Abdallah bin Ja'ffar alitoa sharti moja tu nalo ni la kumtaka mumewe akubali aendelee kubakia siku zote za maisha yao pembeni ya ndugu yake Imam Hussein (as), sharti ambalo Abdallah alilikubali bila kusita.

Sifa nyingine nzuri na ya kupigiwa mfano ya Bibi Zainab (sa) ni ya kujitolea kwa njia ya Mwenyezi Mungu. Katika tukio la Karbala, Bibi huyo mtukufu alikuwa akijizuia kutumia hisa yake ya maji na kuwapa watoto waliokuwa wakitaabika kutokana na kiu ya maji. Akiwa njiani baina ya Kufa na Sham (Syria) licha ya kuwa alikumbwa na kiu na njaa kali lakini alionyesha mfano mzuri na wa kuvutia sana kuhusiana na sifa ya kujitolea mhanga. Imam Zain al-Abideen (as) anasema: 'Shangazi yangu Zainab (katika kipindi cha kukamatwa mateka) alikuwa akiwagawia watoto hisa yake ya chakula kilichokuwa kikitolewa, na usiku na mchana alikuwa akitupa kila mmoja wetu kipande cha mkate.' Matukio magumu yaliyotokea katika maisha yake yote yaliyojaa misiba na machungu, kama vile ya maradhi ya mama yake, kupigwa upanga baba yake, kupewa sumu kaka yake Hassan (as) na hatimaye tukio chungu la Karbala yalimfanya Zainab kuwa mfano wa muuguzi na siku ya kuzaliwa kwake imetangazwa nchini Iran kuwa Siku ya Wauguzi.


Tunaweza kusema mwishoni mwa kipindi hiki kwamba Bibi Zainab (sa) alikuwa dhihiridho na nembo halisi ya sifa zote bora kimaadili. Subira, mapambano, ukakamavu, imani, takwa, kujitolea, heshima, maadili na utu wa mwanamke ni miongoni mwa sifa ambazo wasomi na wataalamu wa masuala ya kiakhlaqi wamezitaja kuwa zilinawiri na kung'ara zaidi katika shakhsia ya mtukufu huyo. Najm Deen Abi al-Hassan mwandishi wa kitabu cha Ansaab at-Talibeen anasema kuwa Bibi Zainab (sa) alikuwa na sifa nyingi bora na kuwashinda watu wengi katika sifa hizo.

Wapenzi wasikilizaji, kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa heri na fanaka kwa wapenzi wote wa haki na ukweli duniani kwa mnasaba huu adhimu wa kukumbuka kuzaliwa Bibi Zainab (sa), mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw) na tunamwomba Mwenyezi Mungu Mrehemevu atupe taufiki ya kuweza kuhamu zaidi sira na maisha ya bibi huyu mtukufu, ili tuweze kutekeleza mafundisho yake mema kwenye maisha yetu. Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.