Jul 04, 2025 03:11 UTC
  • Ijumaa, Julai 4, 2025

Leo ni Ijumaa tarehe 8 Mfunguo Nne Muharram 1447 Hijria sawa na tarehe 4 Julai 2025.

Katika siku kama ya leo tarehe 8 Muharram mwaka 61 Hijria maji yalimalizika kabisa katika mahema ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein (as) na watu wengine wa familia yake katika jangwa lenye joto kali la Karbala.

Kharazmi katika kitabu cha Maqtalul Hussein na Khiyabani katika Waqaiul Ayyam wameandika kuwa: "Katika siku ya nane ya mwezi Muharram mwaka 61 Imam Hussein na masahaba zake walikuwa wakisumbuliwa na kiu kali, kwa msingi huo Imam Hussein alichukua sururu na akapiga hatua kama 19 nyuma ya mahema kisha akaelekea kibla na kuanza kuchimba ardhi. Maji matamu ya kunywa yalianza kutoka na watu wote waliokuwa pamoja naye walikunywa na kujaza vyombo vyao kisha maji yakatoweka na hayakuonekana tena."

Habari hiyo ilipofika kwa Ubaidullah bin Ziad alimtumia ujumbe Umar bin Sa'd akimwambia: "Nimepata habari kwamba Hussein anachimba kisima na kupata maji ya kutumia, hivyo baada ya kupata risala hii kuwa macho zaidi ili maji yasiwafikie na zidisha mbinyo na mashaka dhidi ya Hussein na masahaba zake."   

Katika siku kama ya leo miaka 249 iliyopita, yaani tarehe 4 Julai mwaka 1776 wawakilishi wa majimbo 13 ya awali ya Marekani walisaini "Azimio la Uhuru" wa nchi hiyo katika mji wa Philadelphia.

Ardhi ya Marekani kwa maelfu ya miaka ilikuwa makazi ya Wahindi Wekundu. Mwishoni mwa karne ya 15 wavumbuzi wa Ulaya waliwasili Marekani na nchi mbalimbali za Ulaya zikavamia na kukalia kwa mabavu kila eneo la nchi hiyo.

Wazungu hao wa Ulaya waliandamana na mamilioni ya watumwa kutoka Afrika ambao walitumiwa katika kazi ngumu za mashambani na viwandani.

Miaka 79 iliyopita katika siku kama ya leo, visiwa vya Ufilipino vilijitangazia uhuru kutoka kwa Marekani.

Fernando Magellan mvumbuzi wa Kireno pamoja na wenzake ndio waliokuwa Wazungu wa kwanza kutoka Ulaya kuwasili katika ardhi ya Ufilipino na hiyo ilikuwa mwaka 1521. Katika kipindi cha nusu karne baadaye, Uhispania ikawa imeidhibiti ardhi yote ya nchi hiyo.

Mkoloni Muhispania alipora mali na utajiri wa Ufilipino kwa muda wa karne tatu. 

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita yaani 13 Tir mwaka 1350 Hijria Shamsiya alifariki dunia mwalimu mkubwa wa fasihi wa Iran, Dakta Muhammad Muin, baada ya kufanya juhudi kubwa za miaka mingi katika nyanja za utamaduni na mila za Kifarsi.

Dakta Muin alizaliwa katika mji wa Rasht kaskazini mwa Iran. Alijifunza fasihi ya Kiarabu ujanani na baada ya kukamilisha masomo yake katika skuli ya Darul-Funun alielekea katika Chuo Kikuu cha Tehran na kujiunga na masomo katika kitengo cha fasihi na falsafa.

Mwaka 1321 Hijria Shamsiya Ustadh Muin alianza kufanya kazi ya kufundisha na utafiti katika Chuo Kikuu cha Tehran akiwa mhitimu wa kwanza wa shahada ya udaktari wa lugha na fasihi ya Kifarsi.

Na katika siku kama ya leo miaka 15 iliyopita,  Ayatullah Sayyid Muhammad Hussein Fadhlullah mmoja wa maulama mashuhuri na marja taqlidi wa Kiislamu alifariki dunia.

Allama Fadhlullah alizaliwa mwaka 1935 katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq katika familia ya kidini yenye asili ya Lebanon. Sayyid Fadhlullah alianza kujifunza elimu ya dini katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Najaf, Iraq akiwa bado kijana mdogo. Alijishughulisha na uandishi wa makala na vitabu na alikuwa mshairi.

Ayatullah Fadhlullah alikuwa miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah, na jambo hilo liliikasirisha sana Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ambazo zilifanya majaribio kadhaa ya kutaka kumuua.

Ayatullah Muhammad Hussein Fadhlullah ameandika vitabu vingi vya thamani ikiwemo tafsiri ya Qur'ani ya "Min Wahyil Qur'an."