Jenerali apaa na kukumbatiwa na Malaika
مِنَ الْمُؤْمِنِینَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّهَ عَلَیْهِ فَمِنْهُمْ مَنْ قَضَى نَحْبَهُ وَمِنْهُمْ مَنْ یَنْتَظِرُ وَمَا بَدَّلُوا تَبْدِیلًا
Miongoni mwa Waumini wapo watu waliotimiza waliyoahidiana na Mwenyezi Mungu. Baadhi yao wamekwishakufa, na baadhi wanangojea, wala hawakubadilisha (ahadi) hata kidogo. (Ahzab-23)
Alfajiri ya Ijumaa iliyopita Iran na Waislamu kwa ujumla walisikia habari ya kushtusha ya kuuawa shahidi Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Luteni Jenerali Qassem Soleimani katika shambulizi la kigaidi la helikopta za Marekani baada ya miaka mingi ya kupigana Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kadiri habari hii ilivyowafurahisha maadui wa Uislamu ndivyo hivyo hivyo ilivyoyakasirisha na kuyatia simanzi mataifa ya Kiislamu. Kwa hakika kupoteza mtu mkubwa na mujahid aliyesabilia maisha yake kwa ajili ya Uislamu kama Haji Qassem Soleimani ni msiba mkubwa si kwa taifa la Iran pekee bali Umma wa Kiislamu kwa ujumla. Hata hivyo jambo linaloweza kupunguza maumivu ya msiba huu mkubwa ni kwamba kamanda Solaimani mwenyewe alikuwa akisubiri kikombe cha kuuliwa shahidi kwa hamu na shauku kubwa.
Kaka yake Jenerali Qassem Soleimani anasimulia jinsi ndugu yake alivyokuwa na hamu kubwa ya kuuliwa shahidi na kupata daraja hiyo adhimu kwa miaka mingi akisema: Ni msiba mkubwa wa kupoteza askari huyu mkubwa wa Uislamu lakini inanipasa kusema kuwa, daima alikuwa na hamu na matarajio ya kuuliwa shahidi. Hili kwetu si jambo jipya kwani kila aliposafiri nje ya nchi hususan katika miaka ya vita vya hivi karibuni kwenye kuongoza mapambano dhidi ya magaidi na mabwana zao huko Iraq na Syria alikuwa na hamu kubwa ya kuuliwa shahidi katika medani za Jihadi. Mwenyezi Mungu alimbakisha hai ili apambane na mafisafi na mabeberu akisaidiana na wapigajihadi wenzake kutoka maeneo mbalimbali ya Umma wa Kiislamu na kung'oa mzizi wa makundi ya kitakfiri. Ilitarajiwa kuwa, mabeberu wasingeweza kustahamili kumuoa askari huyo wa Uislamu akiendelea kuhudumia dini yake, dola la Kiislamu na kiongozi wake. Kwa hakika alikuwa akiumia sana kuona kwamba bado hajapata daraja hii ya juu ya kuuliwa shahidi. Alikuwa akisubiri kupata daraja hii, na kuuliwa shahidi ndiyo malipo anayostahili. Sambamba na kutoa mkono wa pole kwa Umma wa Kiislamu kwa kumpoteza shujaa na hadimu wake mkubwa, ninampongeza sana yeye mwenyewe kwa kupata daraja hii adhimu. Natarajia kuwa maelfu ya Haj Qassem wengine watajitokeza hapa nchini kwetu na katika Umma wa Kiislamu na kutimiza malengo na matakwa ya Uislamu.
Katika fikra za Uislamu suala la kufa au kuuliwa shahidi ndiyo daraja ya juu kabisa anayoweza kufikia mwanadamu katika jitihada zake za kukwea ngazi za juu zaidi za kiroho na hakuna kitu bora zaidi kwa mtu anayeuawa shahidi katika njia ya haki kama wakati anapokuwa akikumbatia nishani na kutoa roho yake katika njia hiyo. Aya ya 169 ya Suratu Aal Imran inasema:
وَلاَ تَحْسَبَنَّ الَّذِینَ قُتِلُواْ فِی سَبِیلِ اللَّهِ أَمْوَاتًا بَلْ أَحْیَاء عِندَ رَبِّهِمْ یُرْزَقُونَ
Wala usiwadhanie waliouliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni maiti. Bali hao wako hai, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi. Wanafurahia aliyowapa Mwenyezi Mungu kwa fadhila yake, na wanawashangilia wale ambao bado hawajajiunga nao, walio nyuma yao, ya kwamba haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika. Kwa mujibu wa aya hizi za Qur'ani tukufu, shahidi huwa hai na anaruzukiwa kwa mola wake Mlezi.
Vilevile imepokewa kutoka kwa Mtume Muhammad (saw) kwamba amesema:
فَوْقَ کلِّ بِرٍّ بِرٌّ حَتّی یقْتَلَ الرَّجُلُ فِی سَبیلِ اللَّهِ، فَاذا قُتِلَ فِی سَبیلِ اللَّهِ- عزّوجلّ- فَلَیسَ فَوْقَهُ بِرٌّ
"Juu ya kila amali njema kuna amali njema zaidi hadi pale pale mtu anapouliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Anapouawa katika njia ya Allah huwa hakuna tena amali njema zaidi yake."
Wasii na khalifa wa Mtume Muhammad (saw), Ali bin Abi Twalib (as) anasema:
إِنَّ أکرَمَ المَوتِ القَتلُ، وَالَّذِی نَفسُ ابنِ أبِی طَالِبٍ بِیدِهِ لَألفُ ضَربَة بِالسَّیفِ اهوَنُ عَلَی مِن مِیتَة عَلَی الفِرَاشِ فِی غَیرِ طَاعَة اللهِ
"Mauti bora zaidi ni yale ya kuuawa (katika njia ya Allah). Naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu anayemiliki nafsi ya mwana wa Abu Twalib kwamba, kupigwa upanga mara alfu moja ni kwepesi zaidi kwangu mimi kuliko kufia kitandani bila ya kumtii Mwenyezi Mungu."
Uhakika huu umeashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khameni katika risala yake ya taazia pale aliposema: Kamanda adhimu na fahari ya Uislamu amepaa mbinguni. Jana usiku (usiku wa kuamkia Ijumaa) roho safi za mashahidi ziliikumbatia roho iliyotakasika ya Qassem Solaimani. Baada ya miaka mingi ya kupigana jihadi kwa ikhlasi na ushujaa katika medani mbalimbali za kupambana na mashetani na waovu wa dunia hii na miaka mingi ya hamu kubwa ya kupata daraja ya juu ya kuuliwa shahidi, hatimaye Soleimani amepata daraja hiyo ya juu kabisa na damu yake imemwagwa na watu wovu kuliko wote."
Wasifu wa Shahidi Soleimani:
Shahidi Qassem Soleimani alizaliwa tarehe 20 Esfand 1335 Hijria Shamsia (11 Machi mwaka 1957) katika kijiji cha milimani mkoani Kerman. Baada ya kukamilisha shule ya msingi akiwa na umri wa miaka 12, aliondoka kijijini kwake na kufanya kazi ya ujenzi huko Kerman. Wakati Saddam Hussein alipovamia ardhi ya Iran na kuanzisha vita, Soleimani alielekea katika medani ya vita na muda mfupi baadaye aliunda kikosi cha wapiganajii wa kujitolea kilichokuwa mashuhuri kwa jina la Divisheni ya 41 ya Tharullah akiwa kamanda wake. Katika kipindi chote cha vita vya kulazimishwa kikosi hicho cha Jenerali Soleimani kilikuwa na mchango mkubwa katika operesheni nyingi za vita zikiwemo opesheni za Walfajiri 8, Karbala 4, Karbala 5 na Tak Shalamche.
Jenerali Qassem Soleimani alijeruhiwa kwa mara ya kwanza tumboni na kwenye mkono wake kwa kipande cha risasi ya mzinga mwezi Azar mwaka 1360 katika operesheni ya kijeshi iliyotekelezwa kwa pamoja na jeshi la taifa na lile wa Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) iliyopewa jina la Twariqul Quds (yaani Njia ya Kuelekea Quds) huko magharibi mwa eneo la Susangerd. Majeraha hayo hayakumzuia kuendelea kupigana Jihadi katika medani za vita na aliendelea kuongoza Divisheni ya 41 ya Tharullah hadi vita baina ya Iran na Iraq vilipomalizika. Alirejea na kikosi chake katika mkoa wa Kerman na kuanza kupambana na makundi ya wahalifu katika mipaka ya mashariki mwa Iran. Haj Qassem Soleimani aliendelea kupambana na magenge ya wafanya magendo ya dawa za kulevya katika mpaka wa Iran na Afghanistan hadi alipoteuliwa na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote ya Iran, Ayatullah Ali Khamenei hapo mwaka 1376 Hijria Shamsia kuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah).
Mwaka 1398 Hijria Shamsia Ayatullah Khamenei alimpandisha daraja na kumtunuku cheo cha Meja Jenerali ili kuenzi huduma zake kubwa kwa taifa na kumtaja kuwa ni "shahidi aliye hai". Katika miaka ya hivi karibuni Jenerali alikuwa kinara wa mapambano dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh. Baada ya kuuawa shahidi Mohsen Hojaji afisa wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyekuwa akitoa ushauri wa kijeshi kwa wanamapambano wanaopigana dhidi ya kundi hilo la kigaidi huko Syria, Jenerali Soleimani aliahidi kwamba kundi la Daesh litaangamizwa kikamilifu miezi kadhaa ijayo na kweli alitimiza ahadi yake. Mwezi Esfand 1397 Amiri Jeshi Mkuu wa Iran Ayatullah Khamenei alimtunuku Haj Qassem Soleimani nishani ya Dhulfiqar. Nishani hii ndiyo ya juu zaidi ya kijeshi nchini Iran na ni mara ya kwanza kutolewa na Ayatullah Khamenei kwa Meja Jenerali. Katika ujumbe alioutoa baada ya kuuliwa shahidi Haj Soleimani, Ayatullah Khamenei amemtaja kuwa ni "mfano aali wa mtu aliyelelewa katika madrasa ya Uislamu na maktaba ya Imam Ruhullah Khomeini". Amesema: Alisabilia umri wake wote kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuuliwa kwake shahidi ni malipo ya juhudi zake kubwa katika kipindi hicho chote. Na kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, kuondoka kwake hakusitisha kazi zake wala hakusimamisha njia yake. Kisasi kikali kinawangoja watendajinai ambao mikono yao michafu imemwaga damu yake na mashahidi wenzake wa shambulizi hili."
Wapenzi wasikilizaji kuuliwa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu ni matokeo ya ushujaa na kuchagua njia ya kupambana na ukafiri, dhulma na ubeberu na kunadhamini amani ya jamii na kuipa uhai mpya. Kwa maneno mengine ni kuwa kuuliwa shahidi katika njia ya haki ni sawa na kutia damu mpya katika kiwiliwilii cha jamii na kuihuisha tena baada ya kuanza kunyong'onyea na kudhoofika. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Mtume Muhammad (saw) anawasifu mashahidi wanaouliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu akisema: Madhambi yote ya shahidi husamehewa na Mwenyezi Mungu kwa tone la kwanza kabisa la damu yake inayoanguka juu ya ardhi; wakati huo kichwa cha shahidi hupakatwa na malaika wawili ambao hufuta vumbi kwenye kipaji chake cha uso na kumkaribisha. Kisha huuvika mwili wake vazi la peponi. Huko peponi malaika huanza kushindana kwa ajili ya kumpaka uturi na marashi. Kabla ya roho ya shahidi kuachana na mwili wake huona nafasi yake peponi na roho yake huambiwa: Kaa katika nafasi yoyote unayoitaka wewe. Shahidi hutazama Arshi ya Mwenyezi Mungu na kupata furaha na radhi zake Mola Mlezi…"
Nam, kutokana na kujisabilia kwake katika njia ya Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya Uislamu, Mwenyezi Mungu, Mtume na Waislamu ndiyo maana Jenerali alipendwa sana na watu wote. Aliwajali sana watoto wa mashahidi waliouawa katika njia ya haki na daima alikuwa pozo na nguzo muhimu ya watu wanaodhulumiwa si nchini Iran pekee bali hata nje ya nchi hususan katika nchi za Iraq na Syria. Alikuwa mchamungu aliyefanya kila kitu kwa ikhlasi kubwa na alikuwa akisubiri kikombe cha kuuliwa shahidi tangu miaka mingi iliyopita. Mtoto wake Luteni Jenerali Qassem Soleimani anasimulia jinsi baba yake alivyokuwa na shauku kubwa ya kuuliwa shahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu akisema: Baba yangu alikuwa askari wa utawala wa Kiislamu wa faqihi mtawala. Alikuwa hivyo hivyo hadi dakika ya mwisho ya uhai wake. Alikuwa na hamu kubwa ya kupata daraja ya kuuliwa shahidi. Alikuwa akiifatuta daraja hiyo kwa miaka mingi na sasa ameipata. Ninampongeza sana. Wakati mwingine tulipokuwa tukizungumza nyumbani, alikuwa akiniambia kwamba, ninakimbia huku na kule nikitafuta daraja ya kuuliwa shahidi……
Katika wasia wake, Jenerali Soleimani amemwambia mke wake kwamba: "Mke wangu! Tayari nimeainisha sehemu ya kaburi langu katika eneo la makaburi ya mashahidi huko Kerman… Kaburi langu liwe la kawaida tu kama yalivyo makaburi ya marafiki zangu waliouawa shahidi. Juu la kaburi langu andika tu neno: Askari, Qassem Soleimani, na wala usindike neno lolote linaloakisi cheo.” picha
Naam, Jenerali alikuwa kielelezo halisi cha aya ya 207 ya Suratul Baqara inayosema:
وَمِنَ النَّاسِ مَن یَشْرِی نَفْسَهُ ابْتِغَاء مَرْضَاتِ اللَّهِ وَاللَّهُ رَؤُوفٌ بِالْعِبَادِ
Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.
Shetani mkubwa yaani Marekani imemuua kigaidi mwili wa Meja Jenerali Qassem Soleimani lakini roho, fikra na njia yake imepa uhai zaidi kwa damu yake iliyonywesheleza mti wa jihadi na harakatri za kupaga na mashetani na madhalimu. Maadui wanapaswa kuelewa kwamba, wakati rijali adhimu kama Haj Soleimani wanapouawa shahidi, bendeza zao kushikwa na maelfu ya Masoleimani na kuendelea kupepea, tena kwa ari na azma kubwa zaidi.
Sala na salamu za Mwenyezi Mungu, Malaika, Mitume na Mawali wote wa Mwenyezi Mungu zimshukie Haj Soleimani na mashahidi wengine waliosabilia nafsi zao kwa ajili ya Allah.