Oct 13, 2022 08:04 UTC
  • Umoja katika Hadithi za Mtume wa Rehma

Bismillahil Rahmanil Rahim. Kwa jina la Mungu wa Muhammad (SAW) ambaye ametubariki na akatutambulisha Mtume wake, akateremsha Qur'ani kwake ili iwe hidaya na mwongozo kwa ajili ya wanaadamu wote.

Salamu na amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya Waislamu wote duniani. Salamu na amani Yake SW iwe kwa wapenzi wote wa Muhammad (SAW) na juu yenu nyinyi wapenzi wasikilizaji hususan katika siku hizi za Maulidi na maadhimisho ya kuzaliwa mbora wa viumbe na Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu.

Miaka 570 baada ya kuzaliwa Nabii Isa Masiih (as) na katika siku ya 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal Mwaka wa Tembo, dunia ilishuhudia tukio la kustaajabisha. Masanamu yote yaliyokuwa yakiabudiwa badala ya Mungu Mmoja yalianguka chini kifudifudi na kuvunjika vunjika. Kasri ya mfalme wa Kisasani, Kisra  (Khosrow), ilitetereka na nguzo zake 14 zikavunjika. Ziwa ambalo majusi walikuwa wakikusanyika kandokando yake kwa miaka mingi lilikauka, na mito ya maji ikatiririka katika ardhi ambayo hapo awali hakuna mtu aliyeshuhudia maji katika eneo hilo. Moto wa maabadi ya Fars ambao ulikuwa ukiwaka kwa kipindi cha miaka elfu moja, ulizimika na nuru iliyochomoza kutoka upande wa Hijaz ilienea na kuonekana duniani kote. Nuru ilitanda dunia nzima na mashetani wakapatwa na kiwewe na wasiwasi. Uchawi wa wachawi ulibatilika na ujuzi wa makuhani ukageuka na kuwa ujinga. Wafalme wa zama hizo walipatwa na kigugumizi na kujiuliza, kulikoni?! Sambamba na matukio hayo ya ardhini, huko mbinguni pia kulishuhudiwa matukio ya kustaajabisha. Mashetani walifukuzwa kutoka kwenye mbingu zote saba na kuzuiwa kusikiliza habari za mbinguni. Siku hiyo, viumbe vyote vya duniani na mbinguni, kuanzia Malaika hadi wanyama wa ardhini na baharini, hata miti, mawe na kadhalika, vilimtukuza na kumsabbih Mwenyezi Mungu na kufurahia tukio la kuzaliwa Muhammad (saw). Siku hiyo kito adhimu na adimu cha ulimwengu kiliweka mguu juu ya uso wa dunia, na kiumbe bora kuliko wote, pambo la Mitume, Muhammad bin Abdullah alikuwa amezaliwa.

Mabaki ya kasri ya Kisra

Mwenyezi Mungu SW alimfanya kipenzi na azizi baina ya wanaadamu na akampa ulinzi na himaya yake hadi alipofikisha umri wa miaka arubaini. Ni wakati huo ndipo alipomteremshia elimu na maarifa kutoka kwenye Lauhul Mahfudh, na akamwamuru kufikisha ujumbe wake kwa wanaadamu wote. Alimpa jukumu ya kuwaongoza na kuwaelekeza kwenye saada na ufanisi wa dunia na Akhera.

Maabadi ya Fars, Iran

Kwa siku kadhaa sasa wapenzi wasikilizaji tumo katika siku za sherehe na furaha kwa za kumshukuru Mwenyezi Mungu SW kutokana na neema yake kubwa ya kuzaliwa Mtume Wake wa mwisho na mbora wa viumbe, Muhammad Mwaminifu. Hata hivyo ili kuweza kushukuru ipasavyo neema yoyote ya Mwenyezi Mungu kuna udharura kwanza wa kuijua na kuitambua neema yenyewe. Na utangulizi wa kujua neema kubwa ya siku hizi za Rabiul Awwal, yaani kuzaliwa kwa Mtume wetu (saw) ni kuujua vyema Uslamu wenyewe. Uislamu una nguzo na matawi na kanuni ndogo ambazo zote ni wajibu kwa Waislamu kuzijua, lakini katika baadhi ya hadithi zilizopokelewa kutoka kwa Mtume kipenzi (saw) na Maimamu watoharifu katika kizazi chake, baadhi ya vipengele vimetambulishwa kuwa nguzo za dini ya Uislamu. Baadhi ya maulamaa wa madhehebu ya Ahlusunna wanasema, nguzo za dini ni tano nazo ni kushuhudia kwamba hakuna Mungu ila Allah SW na kwamba Muhammad ni mtume wake, kuswali, kufunga Swaumu, kutoa Zaka na kwenda Makka kuhiji kwa mwenye uwezo.  Imam Ja'far al Swadiq (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu watukufu wa Mtume (saw) anasema dini ya mja haikamiliki ila kwa kuamini mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuamini kwamba, Mwenyezi Mungu SW ni Mmoja na hana mshirika, kuamini Utume wa Nabii Muhammad (saw) na yote yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kutoa Zaka na kukubali wilaya na uongozi wa Aali na kizazi cha Muhammad (saw).

Qur'ani Tukufu imehimiza umoja na mshikamano baina ya Waislamu. Mwenyezi Mungu SW anautaja mshikamano na umoja kuwa ni sababu ya saada, maendeleo na ufanisi, na migawanyiko kuwa ni sababu ya kuporomoka na kuangamia. Kwa msingi huo umoja na mshikamano katika mafundisho ya Qur'ani ni miongoni mwa masuala ya wajibu na ya dharura kwa kila muumini wa dini hiyo. Mwenyezi Mungu SW anasema katika Aya ya 103 ya Suratu Aal Imran kwamba:

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِیعًا وَلَا تَفَرَّقُوا ۚ وَاذْکُرُوا نِعْمَتَ اللَّهِ عَلَیْکُمْ إِذْ کُنْتُمْ أَعْدَاءً فَأَلَّفَ بَیْنَ قُلُوبِکُمْ فَأَصْبَحْتُمْ بِنِعْمَتِهِ إِخْوَانًا

"Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu: mlivyokuwa maadui Naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu.…" Aya hii inawaamuru Waislamu kushikamana na kuwa kitu kimoja na kujiepusha na mifarakano na migawanyiko. Vilevile inautaja udugu na upendo baina ya Waislamu kuwa ni miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu.

Jamii ya Kiislamu ina mambo kadhaa muhimu yanayojenga umoja na mshikamano baina ya Waislamu. Miongoni mwa mambo hayo ni lengo la Waislamu wote la kusimamisha Tauhidi na ibada ya Mwenyezi Mungu Mmoja kote duniani, na Waislamu wote, Shia na Suni, wanakubaliana kwamba, Qur'ani Tukufu ndiyo ratiba na mwongozo wa kutimiza lengo hilo. Na zaidi ni kwamba, Waislamu wote pia wanaamini kuwa Mtume Muhammad (saw) ndiye Hadi na kiongozi wao. Kwa msingi huo umoja na mshikamano wa Umma wa Kiislamu daima umekuwa lengo na jambo linalohimizwa na kufuatiliwa na maulamaa wa Waislamu wa Shia na Suni.

Mtume (saw) daima alikuwa akiwahimiza Waislamu kuwa na umoja na mshikamano. Anasema katika mojawapo ya Hadithi zake kwamba:

من فارق الجماعة مات میتة جاهلیه

"Mtu anayejitenga na Waislamu wenzake hufa kifo cha kijahilia." Anasema katika Hadithi nyingine kwamba:

- المسلم اخو المسلم و من کان فی حاجة اخیه کان الله فی حاجتة.

"Muislamu ni ndugu ya Muislamu mwenzake, na anayekidhi haja ya ndugu yake, Mwenyezi Mungu humkidhia haja yake." Vilevile anasema:

من فارق الجماعة شبرأ خلع الله ربقة الاسلام من عنقه

"Mtu anayejitenga na Waislamu shibri moja, Mwenyezi Mungu huondoa mnyororo wa Uislamu shingoni mwake", kwa maana kwamba mtu huyo huwa ameondoka katika Uislamu.

Vilevile Mtume Muhammad (saw) amewausia Waislamu kuwafuata na kuwatii viongozi waliopewa majukumu ya uongozi na Mwenyezi Mungu SW na kwamba, uongozi kama huo ni msingi wa umoja na mshikamano wa Umma.

Khalifa na wasii wake, Imam Ali bin Abi Twalib (as) pia anamtaja Imam na kiongozi wa Umma katika jamii ya Kiislamu kuwa ni mithili ya kamba inayounganisha pamoja pingili za mnyororo mmoja, na pale kamba hiyo inapokatika, pingili za kamba hiyo hutawanyika huku na kule, na kamwe hazikutani tena. Imam Ali (as) amewausia Waislamu kupata ibra na somo katika hali iliyowapata Banii Israel ambao anasema walikuwa watawala na wenye nguvu wakati walipokuwa na umoja na mshikamano, na walisambaratika na kuvikwa vazi na udhalili na unyonge baada ya kuhitilafiana na kugawanyika katika makundi makundi. Mwenyezi Mungu SW aliwanyang'anya neema zake, na kilichobakia ni historia ya hatima yao ambayo sasa ni ibra na funzo kwa wanaadamu wengine.

Kwa msingi huo Mtume Muhammad (saw) ambaye tunasherehekea Maulidi na kuzaliwa kwake anatutahadharisha tusije tukapatwa na hatima kama hiyo akisema:

لاتختلفوا فان من کان قبلکم اختلفوا فهلکوا

"Msihitilafiane, kwani waliokuwa kabla yenu walihitilafiana na matokeo yake waliangamia."

Tags