Oct 11, 2023 11:54 UTC
  • Palestina, Mhimili wa Umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu

Karibuni kutegea sikio kipindi cha juma hili cha Makala ya Wiki ambacho kitazungumzia Palestina kama mhimili wa umoja baina ya Waislamu wote.

Katika miaka ya hivi karibuni, maadui wa Uislamu wamejaribu kuzuia umoja baina ya Waislamu kwa kuzusha hitilafu baina ya madhehebu mbalimbali za Kiislamu. Japokuwa katika baadhi ya nyakati maadui hao wamefanikiwa kwa kiasi fulani katika njia hiyo, lakini mafanikio hayo yalikuwa ya muda mfupi, na kutokana na kuwa macho Waislamu, mipango hiyo ya maadui kama Marekani, Uingereza, Ufaransa na utawala wa Kizayuni wa Israel imefeli na kugonga mwamba. 

Suala la ukombozi wa Quds na Palestina ni miongoni mwa masuala yanayowakutanisha pamoja Waislamu. Imetimia miaka 75 tangu Wazayuni walipoikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina. Katika kipindi hicho chote, Waislamu wa Palestina hawakuacha mapambano ya kukomboa ardhi yao takatifu. Ingawa baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu wamekuwa wakifanya mapatano na Wazayuni maghasibu, lakini watu waliodhulumiwa wa Palestina walitambua ukweli kwamba, kuendeleza mapambano ndiyo njia pekee inayoweza kubadilisha mlingano wa nguvu katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kwa maslahi yawanaodhulumiwa. Kwa msingi huo, kutimizwa lengo la ukombozi wa Quds Tukufu na wananchi wa Palestina kutawezekana tu kupitia njia ya mapambano, umoja na uungaji mkono kamili wa Umma wa Kiislamu na watetezi wa haki kote duniani.

Quds Tukufu 

Katika mwelekeo huo, wanamageuzi wengi wamefanya juhudi kubwa kuwasaidia Waislamu wa Palestina kwa kuitikia wito wa Qur'ani Tukufu, na sasa tunashuhudia matokeo mazuri. Aya za 39 hadi 40 za Suratu al Haj zinasema: Wameruhusiwa kupigana wale wanaopigwa vita, kwa sababu wamedhulumiwa. Na kwa hakika, Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia. Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa wanasema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu. 

Imam Ruhullah Khomeini alikuwa mmoja wa wanamageuzi wakubwa ambaye katika siku ya tarehe 13 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka 1979 alitangaza "Siku ya Kimataifa ya Quds", akisema katika ujumbe wake kwa Waislamu duniani kwamba: Nawaomba Waislamu wote duniani na nchi za Kiislamu tuungane kukata mkono wa utawala ghasibu wa (Israel) na waungaji mkono wake, na ninawaomba Waislamu wote duniani kuifanya Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambayo ni mojawapo ya siku za Laitatul Qadr inayoweza kuamua hatima ya watu wa Palestina, kuwa "Siku ya Quds" na kutangaza mshikamano wa kimataifa wa Waislamu katika kutetea haki za kisheria za Waislamu wa Palestina."

Mwendazake, Imam Khomeini, Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Ujumbe huu wa Imam Khomeini ulikuwa mwanzo wa umoja wa Waislamu wa madhebu za Shia na Suni katika kadhia ya Palestina na masuala mengine. Kwa kadiri kwamba, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: “Suala la Palestina ambalo kwa dhana ya Wazayuni na waungaji mkono wao, lilihesabiwa kuwa limekwisha na halitajadiliwa tena, liligeuka na kuwa kadhia nambari moja ya Ulimwengu wa Kiislamu kutokana na harakati ya Imam Khomeini na mabadiliko aliyoyasababisha katika upeo wa Umma wa Kiislamu... Hii leo Palestina ni kitovu cha mazingatio ya mataifa ya Kiislamu." Kielelezo cha umoja na mazingatio hayo ni mshikamano wa wapiganaji Waislamu wa madhehebu ya Shia wa Hizbullah na Hamas na Jihad Islami za Kisuni na makundi mengine ya Iraq, Afghanistan, Pakistan na nchi nyingine, ambao wote wameungana katika mapambano dhidi ya Mzayuni ghasibu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, Ayatullah Ali Khamenei 

Sambamba na ukweli kwamba Palestina ni ardhi takatifu na kibla cha kwanza cha Waislamu, pia ni jambo muhimu zaidi linalounganisha pamoja nguvu za Umma wa Kiislamu. Hakuna sehemu yoyote katika Ulimwengu wa Kiislamu ambayo imeshughulisha fikra za Waislamu kama Palestina tangu mwanzoni mwa kubaathiwa Mtume (SAW) hadi leo.      

Hii leo suala la kukombolewa Palestina si ndoto au dhana tupu; kwani kwa upande mmoja, utawala wa Kizayuni hivi sasa umezungukwa na mataifa ya Kiislamu ambayo yameungana na yanataka kuuangamiza utawala huo wa kibaguzi na ghasibu; na kwa upande mwingine, kumejitokeza nyufa na migawanyiko mikubwa ndani ya utawala huo na hakuna motisha iliyobaki baina ya watu kwa ajili ya kuutetea. 

Kuhusiana na suala hilo, Jenerali mashuhuri wa Kizayuni anayejulikana kwa jina la Amos Gileadi amekiri kuwepo umoja na mshikamano baina ya Waislamu wa Shia na Suni katika kadhia ya Palestina na kusisitiza kuwa: "Hivi sasa tunashuhudia kuundwa umoja baina ya Masuni na Mashia ili kutimiza lengo la kutokomeza Israeli."

Gilead, ambaye anahesabiwa kuwa mmoja wa majenerali wenye misimamo mikali wa utawala wa Kizayuni wa Israel, alisema katika mahojiano na redio ya taifa ya utawala wa Kizayuni (Reshet Bet) kwamba "Hamas ya Kisuni na Hizbullah ya Kishia zimeungana ndani ya mfumo wa kidini na mitazamo ya kizalendo kuiangamiza Israeli".

Marekani, kama muungaji mkono muhimu zaidi wa utawala wa Kizayuni, daima imekuwa ikifanya jitihada za kuimarisha utawala huo, na imejaribu kusimamia mfumo wa kimataifa kwa kuzingatia matakwa yake. Hata hivyo, sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za nchi hiyo ambazo ni matokeo ya mienendo ya kibeberu, kiburi na ghururi, zimeifanya ishindwe kutatua masuala ya kimataifa kwa misingi ya busara, haki na uadilifu na kusababisha matatizo makubwa katika mfumo wa kimataifa kwa kuchochea vita, mauaji, ubaguzi na uhasama. Huo ulikuwa mwanzo wa kuundwa mfumo mpya katika uga wa kimataifa, unaoandamana na fursa mpya na unaotoa nafasi muhimu kwa ulimwengu wa Kiislamu. Kwa msingi huo, wanafikra wanaamini kuwa, Ulimwengu wa Kiislamu unaweza kushinda udhaifu na changamoto zilizopo na kupata nafasi yake makhsusi katika mfumo mpya wa dunia kwa kutegemea uwezo wake, na kuzigeuza changamoto kuwa fursa. Wanasisitiza kuwa, umoja na uwezeshaji wa Kiislamu ndiyo njia pekee ya kujiondoa kwenye matatizo na changamoto zinazoukabili Umma wa Kiislamu. Miongoni mwa mambo yanayoweza kuimarisha zaidi umoja huo ni kushikamana pamoja chini ya kivuli cha Kalima ya Tauhidi, kushikamana na Qur'ani Tukufu, Mtume Muhammad (SAW) na Maimamu watoharifu katika kizazi chake.

Katika muktadha wa umoja na mshikamano wa Kiislamu, hususan katika kipindi cha sasa ambapo utawala wa Kizayuni wa Israel unafanya mashambulizi ya kikatili dhidi ya watu wa Palestina hasa katika Ukanda wa Gaza, makundi yote na harakati za mapambano za madhehebu mbalimbali, zinawajibika kudhihirisha umoja huo kivitendo na kuwanusuru Waislamu na wanadamu wenzao wanaodhulumiwa. Wanapaswa wote kuwa chini ya bendera ya Kalima ya Tauhidi na kuweka mbele ya macho na akili zao Aya ya 30 ya Suratu Fussilat inayosema: Hakika wale ambao wamesema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu, kisha wakawa na msimamo imara, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa.

Naam, umoja na mshikamano huu uliosimama juu ya Kalima ya Tauhidi na imani ya kutokukubali kurukuu mbele ya nguvu yoyote isiyo ya Allah SW ndio unaowawezesha wanamapambano wa Hamas, Hizbullah, Jihad Islami na kadhalika kusimama kidete na kukabiliana na mashine ya vita ya utawala wa Kizayuni wa Israel unaosaidiwa na madola ya Magharibi, hususan Marekani.

Tags