Ijumaa, Septemba 5, 2025
Leo ni Ijumaa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1447 Hijria sawa na Septemba 5 mwaka 2025.
Katika siku kama ya leo miaka 1500 inayosadifiana na tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal miaka 53 kabla ya Hijria, kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu akiwemo Mas'udi, alizaliwa Mtume Muhammad SAW.
Wanachuoni wengine wa Kiislamu wanaamini kwamba, Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal mwaka huohuo. Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kipindi cha kuanzia tarehe 12 hadi 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal kila mwaka kuwa ni Wiki ya Umoja kati ya Waislamu kote duniani.
Wiki ya umoja ni fursa nzuri ya kuzikurubisha nyoyo za Waislamu na kuimarisha umoja na mshikamano wao katika kukabiliana na maadui wa Umma wa Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 1206 iliyopita, inayosadifiana na 12 Rabiul Awwal 241 Hijria, alifariki dunia Imam Ahmad bin Hanbal, mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu katika mji wa Baghdad, Iraq ya leo.
Ahmad bin Hanbal alizaliwa mwaka 124 Hijria, katika mji wa Baghdad na kujipatia elimu ya kidini katika mji huo kutoka kwa maulamaa wakubwa akiwemo Imam Shafii. Imam Hanbal amesafiri katika miji kadhaa kama vile Kufa, Basra, Makka, Madina, Sham na Yemen kwa minajili ya kukusanya hadithi za Bwana Mtume SAW.
Ahmad bin Hanbal ni mwasisi wa Madhehebu ya Kisuni ya Hanbal na ameacha kitabu mashuhuri cha hadithi, kiitwacho Musnad.

Siku kama hii ya leo miaka 168 iliyopita alifariki dunia Auguste Comte mwanafalsafa na mwanahisabati wa Kifaransa.
Comte alizaliwa mwaka 1798. Alishirikiana kwa muda fulani huko Paris na Henri de Saint Simon, mwanafalsafa mashuhuri wa zama hizo na baadaye Comte alianza kufundisha. Auguste Comte alikuwa mwasisi wa mfumo wa elimu jamii.
Comte ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha The Positive Philosophy of Auguste Comte.

Miaka 138 iliyopita mwafaka na tarehe 5 mwezi Septemba mwaka 1887, mto mkubwa wa Huang He huko China ulianza kufurika maji. Mafuriko hayo makubwa yalisababishwa na kujaa maji katika mto huo kwa zaidi ya mwezi mmoja. Zaidi ya watu laki tisa walipoteza maisha katika mafuriko hayo na taathira zake mbaya. Aidha miji kadhaa, mamia ya vijiji na mashamba mengi yaliharibiwa baada ya kukumbwa na mafuriko ya mto Huang He huko China. ***
Miaka 120 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 5 Septemba mwaka 1905, Mkataba wa Portsmouth ulitiwa saini na hivyo kuhitimisha vita kati ya Russia na Japan.
Februari 8 mwaka 1904, vikosi vya majeshi ya Japan vilifanya mashambulio ya kushtukiza dhidi ya meli za kivita za Russia na kuyadhibiti maeneo ya Manchuria ambayo yalikuwa chini ya mamlaka ya Russia.
Russia ilipata vipigo mfululizo katika vita hivyo. Hatimaye kwa upatanishi wa Marekani, katika siku kama ya leo pande mbili zilitia saini mkataba wa Portsmouth na huo ukawa mwisho wa vita kati ya Japan na Russia.

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita Ayatullah Ali Quddusi Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mapinduzi ya Kislamu nchini Iran aliuawa shahidi katika mlipuko wa bomu lililotegwa na kundi la kigaidi la MKO.
Shahidi Quddusi alipata elimu yake kutoka kwa wasomi na wanavyuoni kama Ayatullah Burujerdi, Allama Tabatabai na Imam Ruhullah Khomeini MA na kufikia daraja ya Ijtihad. Shahidi Quddusi alishiriki vilivyo katika masuala ya kidini na mfano wa wazi wa mchango wake ni kuasisi skuli ya mafunzo ya kidini ya Haqqani. Mwaka 1341 Hijria Shamsia alisimama kupambana na utawala dhalimu wa Shah na akatiwa jela kwa kipindi fulani.
Ayatullah Quddusi alisabilia miaka ya mwishoni mwa umri wake katika juhudi za kuimarisha mfumo mchanga wakati huo wa Kiislamu hapa nchini na hatimaye aliuawa shahidi na magaidi wa kundi la MKO katika siku kama hii ya leo.

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita inayosadifiana na tarehe 5 Septemba 1993, moja ya misikiti ya kustaajabisha katika Ulimwengu wa Kiislamu ulifunguliwa rasmi huko Casablanca nchini Morocco.
Msikiti huo umejengwa kwa mtindo wa kisasa na una minara inayoakisi usanifu majengo wa hali ya juu wa Kiislamu. Eneo la uwanja wa msikiti huo lina uwezo wa kuchukua waumini 75,000.
Pembeni ya msikiti huo kumejengwa maktaba kubwa na Chuo Kikuu cha Kidini. Msikiti huo unahesabiwa kuwa moja ya misikiti mikubwa na maridadi sana katika Ulimwengu wa Kiislamu.
