Feb 07, 2023 11:20 UTC
  • Mapinduzi ya Iran; Muujiza wa Mwenyezi Mungu

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na katika kipindi kingine maalumu katika mfululizo wa vipindi vya Alfajiri Kumi kuelekea kilele cha maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliyopita ushindi 1979 kwa uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini MA.

Kipindi chetu cha leo kina anuani isemayo: "Mapinduzi ya Iran; Muuujiza wa Mwenyezi Mungu". Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa leo. Karibuni.

 

Tukirejea katika kitabu kitakatibu cha Qur'ani tunakutana na baadhi ya Aya ambazo zinabainisha mwendo na mipango ya Mwenyezi Mungu. Katika lugha ya dini, mwendo wa Mwenyezi Mungu ni ile azma na irada yenye hekima ya Mwenyezi Mungu katika mfumo na nidhamu ya ulimwengu. Matukio mbalimbali ulimwenguni hutokea kwa mujibu wa taqdiri, mipango na mwendo wa Mwenyezi Mungu na kwa mujibu wa kanuni maalumu. Qur'ani Tukufu inazitaja kanuni hizo kwa anuani ya mipango, kawaida na desturi za Mwenyezi Mungu ambazo ni thabiti na si zenye kubadilika.

Mwenyezi Mungu anasema: Huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu ulio kwisha pita zamani, wala hutapata mabadiliko katika mwendo wa Mwenyezi Mungu.

 

Kanuni hizi hazihusiani na matukio ya kimaumbile tu bali zinarejea hata katika maisha ya mtu binafsi na ya jamii ya wanaadamu. Katika Aya ya 54 katika Surat al-Imran Mwenyezi Mungu anasema:

Na Makafiri walipanga mipango na Mwenyezi Mungu akapanga mipango, na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa wenye kupanga.

Aya hii inabainisha moja ya desturi na mwendo wa Mwenyezi Mungu ambao ni kwamba, mipango ya maadui wa haki mbele ya tadbiri na mipango ya Allah ni dhaifu na yenye kushindwa na kugonga ukuta.

Aya hii ni miongoni mwa Aya za Qur'ani Tukufu ambazo zinabainisha njama za kutaka kumuua Nabii Issa Masia (as) zilizokuwa zimepangwa na kundi la Mayahudi. Kundi hilo lilikuwa limejipanga na lilitenga hata zawadi maalumu kwa ajili ya kukamatwa Nabii Issa na hata lilikuwa limeandaa mazingira ya kumuua kwa kumnyonga. Mwenyezi Mungu anasema:

Na Makafiri walipanga mipango na Mwenyezi Mungu akapanga mipango, na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa wenye kupanga.

 

Kuokoa Nabii Issa (as) na hila pamoja na njama za kutaka kumuua ilikuwa ni katika tadbiri na mipango ya Mwenyezi Mungu mkabala na njama na mipango ya maadui. Aya hii inakumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa wenye kupanga.

Tukitupia jicho vigingi na vizingiti ambavyo Mapinduzi ya Kiisamu ya Iran yamevivuka na kwa kuzingatia kiwango kikubwa cha njama na ukhabithi wa maadui dhidi ya mfumo huu tunaona kuwa, kubakia hai kwa Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unaotawaala hapa nchini ni kitu kinachoshabihiana na muujiza.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameifasiri na kuibainisha mara chungu nzima Aya ya 54 ya Surat Aal Imran ambapo amefafanua kwa mapana na marefu kuhusu kushindwa mipango michafu ya maadui dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Katika miaka ya mwishoni mwa utawala wa Kipahlavi kwa kuzingatia nguvu ya Shah pamoja na himaya na uungaji mkono mkubwa wa madola yenye nguvu ulimwenguni kwa utawala wake, ripoti za Mashirika ya Kijasusi ya Marekani (CIA), la utawala haramu wa Israel MOSSAD na hata Shirika la Kiintelijensia na Usalama wa Taifa LA Iran wakati huo SAVAK (Sazman-e Ettela'at va Amniat-e Keshvar) ni mambo ambayo kwa hakika yalikuwa na ishara ya wazi ya kuweko uthabiti wa kisiasa nchini Iran. Walikuwa wakiitaja Iran kwa jina la Kisiwa cha Uthabiti na kutokea harakati na vuguvugu la wananchi dhidi ya utawala lilionekana kuwa ni jambo muhali na lisilowezekana katu. Lakini katika hali ya kushangaza na isiyo ya kawaida na kwa kuzingatia malalamiko ya huko nyuma ya wananchi dhidi ya utawala wa Shah, cheche ya kuenea mapinduzi ikaanza Dei mwaka 1356 Hijria Shamsia katika mji wa Qom. Baada ya hapo, kukaibuka maandamano na malalamiko ya wananchi katika miji mbalimbali kwa sura mtawalia na mfululizo na hatimaye baada ya miezi 13, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yakapata ushindi tarehe 22 Bahman mwaka 1357 iliyosadifiana na tarehe 11 Februari 1979. Akthari ya wanamapambano hawakuwa wakidhani kwamba, ingewezekana kuuangusha utawala wa Shah wenye nguvu na uungaji mkono, tena kwa njia tu ya maandamano ukiacha siku tatu za mwisho ambapo wananchi walifanikiwa kudhibiti maghala ya silaha. Kwa amri ya Imam Khomeini wananchi wakachukua hatamu za kusimamia usalama wa miji na hivyo kuzuia kufanyika aina yoyote ya mapinduzi dhidi ya mapinduzi ya wananchi.

Kufanyika kura ya maoni na wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuchagua mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuunga mkono Katiba ni mambo muhimu ambayo yalifanyika katika kipindi cha chini ya miezi mitatu. Kujikita mizizi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu baina ya mipango yenye wigo mpana ya madola ya mashariki na magharibi kwa ajili ya kuitumbukiza nchi hii katika vurugu na sokomoko ni mfano wa wazi wa ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa waumini ya kuwasaidia na kuwafanya washinde. Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 47 ya Surat al-Rum:

Na ilikuwa ni haki juu yetu kuwanusuru Waumini.

Wapenzi wasikilizaji, kila mara kunapokuweko harakati ya kaumu na taifa fulani dhidi ya dhulma na kwa ajili ya kusimamisha utawala wa kiadilifu sambamba na kuhakikisha thamani za Kimwenyezi Mungu zinatawala na kushika hatamu, basi Mola Muumba hulitambua suala la kuwasaidia kuwa ni wajibu kwake.

 

Mfano mwingine wa mwendo na mipango ya Mwenyezi Mungu tuliushuhudia wazi pale yaliposhindwa mashambulio na vita vya kichokozi vya utawala wa zamani wa Iraq chini ya uongozi wa dikteta Saddam. Katika kipindi hicho, kibaraka Saddam alikuwa akipata himaya na ungaji mkono wa madola yote makubwa na yenye nguvu ya Ulaya, Marekani na Umoja wa Sovieti. Kupitia himaya hiyo, Saddam akaifanya Iran iingie katika vita vya kulazimishwa tena katika kipindi ambacho nchi ilikuwa katika kilele cha matatizo ya ndani. Katika wakati huo, hujuma za maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu hazikuishia tu katika vita, bali kuwaua viongozi wa ngazi za juu hapa nchini ni jambo lililokuwa katika ajenda ya makundi yaliyokuwa na mfungamano na Magharibi. Rais wa nchi, Waziri Mkuu, Mkuu wa Idara ya Mahakama, mawaziri, Wabunge na shakhsia mbalimbali waliuawa na kundi la kigaidi la Munafiqin katika kipindi cha chini ya miezi minne. Kila moja kati ya matukio haya kama lingetokea katika nchi yoyote ile, lingeweza kuvuruga kabisa mfumo wa kisiasa na kuleta ukosefu wa uthabiti katika nchi hiyo. Lakini nchini Iran hali ilikuwa kinyume kabisa. Wananchi walizidi kuwa na mapenzi makubwa na mapinduzi ya Kiislamu na kutaka kubakia kwake ambapo wakiwa na lengo la kutoa himaya na uungaji mkono kwa Imam Ruhullah Khomeini walijitokeza kwa wingi katika medani mbalimbali za vita na kuvumilia kila aina ya ugumu. Kila mara hujuma na njama za adui ziliposhadidi, basi adui alipata jibu na pigo kali zaidi kutoka kwa wananchi wa Iran.

Baada yan kumalizika vita vya kujihami vilivyodumuua kwa miaka minane, taifa la Iran likajikita katika kasi ya kujenga nchi na kupiga hatua katika nyanja mbalimbali za ustawi na maendeleo. Hata hivyo matatizo hayakupungua, kwani kadiri mizizi ya Mapinduzi ya Kiislamu ilivyozidi kuwa imara na kujikita, ndivyo maadui wa ndani na nje nao walivyokusanya nguvu zao kwa ajili ya kuyasambaratisha mapinduzi haya.

Katika miaka ya hivi karibuni, Iran imeandamwa na vikwazo vya kiuchumi vya kila namna ambapo hii leo vikwazo hivyo vimefikia katika hatua ya kiwango cha juu kabisa.

Njama za karibuni kabisa za maadui zenye wigo mpana zaidi dhidi ya Iran ni vita jumuishi ambavyo vimeanzishwa dhidi ya taifa hili miezi kadhaa iliyopita. Katika vita hivi, Marekani, utawala haramu wa Israel baadhi ya madola ya Ulaya na baadhi ya makundi pinzani ya mapinduzi ya Kiislamu yamekuwa yakitumia suhula nyingi na pana zaidi kwa ajili ya kutoa pigo kwa taifa hili kama vyombo vya habari na mawasiliano ya intaneti. Hata hivyo njama zote za maadui na mipango yao michafu dhidi ya mfumo wa Kiislamu imefeli na kugonga mwamba na hivi sasa Iran ya Kiislamu inaelekea katika kilele cha maadhimisho ya mwaka wa 44 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu hiki maalumu kilichokujieni kwa manasaba wa maadhimisho ya Alfajiri Kumi kuelekea katika kilele cha maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu umefikia tamati. Asanteni kwa kunitegea sikio na kwaherini.

Tags