Siku ya Kimataifa ya Maziwa ya Mama
https://parstoday.ir/sw/radio/world-i13507-siku_ya_kimataifa_ya_maziwa_ya_mama
Tunajua kwamba Qur'ani tukufu ndio kitabu kikubwa zaidi cha Mwenyezi Mungu SW bali tunaweza kusema kwamba, kitabu hicho kina ratiba kamili ya maisha ya mwanadamu. Hii ni kwa sababu mbali ya kutoa mafundisho ya masuala ya malezi, maadili na masuala ya kidini na kiroho, kitabu hicho kinampa mwanadamu habari muhimu za kielimu na kisayansi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 18, 2016 03:14 UTC
  • Siku ya Kimataifa ya Maziwa ya Mama

Tunajua kwamba Qur'ani tukufu ndio kitabu kikubwa zaidi cha Mwenyezi Mungu SW bali tunaweza kusema kwamba, kitabu hicho kina ratiba kamili ya maisha ya mwanadamu. Hii ni kwa sababu mbali ya kutoa mafundisho ya masuala ya malezi, maadili na masuala ya kidini na kiroho, kitabu hicho kinampa mwanadamu habari muhimu za kielimu na kisayansi.

Suala la lishe hususan chakula safi na halali ni miongoni mwa mambo yaliyopewa mazingatio makubwa sana katika Qur'ani tukufu. Kitabu hicho mbali na kuzungumzia misingi muhimu inayohusiana na lishe na vyakula ambavyo vinadhamini uzima wa mwili na roho ya mwanadamu, kimetaja baadhi ya vyakula ambayo wasomi wamesisitiza sana umuhimu na thamani zao za kilishe na kitiba na kuandika vitabu na makala nyingi kuhusu vyakula hivyo.

Vyakula mbalimbali sambamba na kudhamini mahitaji ya mwili, vina nafasi muhimu katika kutoa kinga na kutibu maradhi kutokana na sifa makhsusi za vyakula hivyo. Katika baadhi ya aya zake, Qur'ani tukufu wakati mwingine inatoa maagizo ya moja kwa moja kuhusu faida za kitiba za baadhi ya vyakula kama inavyozungumzia faida za asali kwenye aya ya 69 ya Suratu Nahl inayosema: "Ndani yake kuna matibabu kwa wanaadamu…". Au kwa mfano katika aya za 24 mpaka 26 za Suratu Maryam pale Mwenyezi Mungu SW anapomuusia Bibi Maryam, mama wa Nabii Issa Masiih atumie tende na maji baada ya kujifungua, au anapomuusia Nabii Yunus (as) kutumia boga baada ya kutolewa ndani ya tumbo la samaki akiwa mgonjwa kama zinavyohadithia aya za 144 hadi 146 za Suratu Yunus.  

Siku ya Maziwa ya Mama

Shirika la Afya Duniani (WHO) liliitangaza wiki moja ya kuanzia tarehe 31 Julai hadi Agosti 6 Agosti kuwa ni Wiki ya Kimataifa ya Maziwa ya Mama. Hati ya shirika hilo inasema: "Kutokana na umuhimu wa lishe ya maziwa ya mama kwa mtoto mdogo, kina mama wanapaswa kuwanyonyesha watoto wao kwa kipindi cha miaka miwili na kuanza kuwapa chakula wakiwa na miezi sita sambamba na maziwa ya mama. Hata hivyo mtoto anapaswa kuendelea kunywa maziwa ya mama hadi atakapokamilisha miaka miwili".

Kwa mnasaba wa maadhimisho ya wiki hii tunatupia jicho umuhimu wa maziwa ya mama katika mtazamo wa Qur'ani tukufu.

Maziwa ya mama ni mfano wa hekima, rehma na upendo wa Mwenyezi Mungu Muumba kwa mwanadamu na viumbe vingine. Qur'ani tukufu inasisitiza sana umuhimu wa mama kumnyonyesha mtoto kwa kipindi cha miaka miwili yaani miezi 24. Aya ya 14 ya Suratu Luqman inasema: Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili.

Vilevile Qur'ani tukufu inasema katika aya ya 233 ya Suratul Baqara kwamba:

وَالْوَالِدَاتُ یُرْضِعْنَ أَوْلَادَهُنَّ حَوْلَیْنِ کَامِلَیْنِ...

Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili kwa anayetaka kutimiza kunyonyesha.

Wito huo wa Qur'ani wa kuwanyonyesha watoto wachanga miaka miwili kamili ambao ulitolewa karne 14 zilizopita ni miongoni mwa miujiza ya kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa sababu, utafiti iliofanyika katika miongo kadhaa ya hivi karibuni umethibitisha kwamba, faida kubwa zaidi za kunyonya mtoto mchanga zinapatikana kwa kunyonya kipindi cha miaka miwili. Kwa kutilia maanani aya hizo za Qur'ani, tabibu na mwanafikra wa Kifaransa, Maurice Bucaille, anasema: "Mimi ninadhani kwamba, tukitilia maanani kipindi Qur'ani ilipoandikwa (yaani karne 14 zilizopita) basi kuwepo kwa aya hii inayotoa maelezo ya kipindi cha kunyonyesha mtoto mdogo ndani ya Qur'ani si jambo lililobuniwa na fikra ya mwanadamu".

Muujiza huu wa Qur'ani uliodhihirika karne 14 zilizopita wakati wanadamu hawakuwa na zana za kisasa za utafiti, mbali na kuonesha tadbiri na adhama ya Mwenyezi Mungu, unadhihirisha jinsi dini hii ilivyolipa umuhimu suala la uzima wa kimwili na kiroho wa jamii ya mwanadamu.

Katika utamaduni wa Kiislamu maziwa yameelezwa kuwa ni sababu ya shifaa na tiba, suala ambalo pia limesisitizwa na elimu ya utabibu na udaktari. Utafiti wa wasomi unaonesha kuwa, maziwa yana aina mbalimbali za vitamini, maji, madini ya naitreti (nitrate), mafuta, sukari, madini ya chuma kama sodiamu, madini aina ya magnesiamu, zinki, manganese, shaba, chuma na nusu metali kama vile florini, hidrojeni, kiberiti, fosforasi, boroni na kadhalika. Vilevile maziwa yana karibu enzyme 19, oksijeni na nitrojeni, asidi citric na kadhalika. Lita moja ya maziwa inakidhi nusu ya mahitaji ya proteini na nusu ya mafuta yanayohitajiwa na mwili, calcium na vitamini B2 yote, nusu ya vitamin A na thuluthi moja ya vitamin B1 inayohitajiwa na mwili. Katika uwanja huu maziwa ya mama yana umuhimu mkubwa zaidi.

Siku ya Kimataifa ya Maziwa ya Mama

Daktari Muhammad Ridha Taqipoor ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Udaktari nchini Iran ameashiria hadithi ya Mtume Muhammad (saw) inayosema: Mtoto mchanga hana maziwa bora kuliko maziwa ya mama yake", na kusema: Lishe ya maziwa ya mama peke yake ndio ufunguo wa dhahabu wa uzima na njia salama na ya kudumu. Maziwa ya mama hayana kifani, ni kamili na yasiyo na mbadala na huzidisha kinga ya mwili ya mtoto ya kukabiliana na maradhi ya aina mbalimbali ya kuambukiza.   

Mwakilishi wa Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) nchini Iran, Dr Will Parks amesema katika sherehe ya ufunguzi wa benki ya kwanza ya maziwa nchini Iran kwamba: Lishe ya maziwa ya mama huwa sawa na fimbo ya muujiza kwa mtoto. Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2013, lishe ya maziwa ya mama kwa watoto wachanga wenye chini ya miaka miwili imekuwa na taathira kubwa zaidi katika kuzuia vifo vya watoto wachanga na inaweza kuzuia vifo vya zaidi ya watoto laki nane wenye umri wa chini ya miaka 5 katika nchi zinazostawi. Dr Will Parks anaendelea kusema: Kiwango hicho ni sawa na asilimia 13 ya watoto wote wanaofariki dunia na kuongeza kuwa, lishe ya mazima ya mama si tu kwamba inasaidia kumbakisha hai mtoto mdogo, bali pia ina nafasi kubwa katika kukuwa kwa ubongo salama na kuzidisha uwezo wa kuelewa na kujifunza kwa mtoto na kadhalika.  

Vitabu vingi vya marejeo na hata uchunguzi uliofanyika umebaini kwamba, kunyonyesha mtoto kwa kipindi cha miaka miwili kuna nafasi muhimu sana katika uzima wa mama na mtoto. Uchunguzi wa elimu ya tiba umebaini kuwa, maziwa ya mama yanasaidia sana katika kupunguza maradhi ya viungo vya kupumua, njia za mkojo, hupunguza vifo vya ghafla vya watoto wachanga wanaonyonya, hupunguza unene kupita kiasi, matatizo ya mzio, magonjwa hatari ya matumbo, matatizo ya pumu, na magonjwa ya moyo na mishipa wakati wa utu uzima.

Vilevile uchunguzi unaonesha kuwa, kunyonyesha mtoto mchanga kuna mchango mkubwa katika kuzuia magonjwa mbalimbali kwa mama anayenyonyesha. Uvumbuzi mpya unaonesha kuwa, kunyonyesha mtoto mchanga hupelekea kukatika haraka damu ya fuko la uzazi baada ya kujifungua, kupungua uwezekano wa kupatwa na saratani ya matiti, saratani ya kizazi (ovarian cancer), saratani ya endometriamu au saratani ya ukuta wa ndani wa mfuko wa uzazi (Endometrial cancer) na magonjwa mengine ya mishipa na moyo.     

Mama na mtoto wake

Kwa kutilia maanani ukweli huo, wataalamu wanasema kuwa, sisitizo la Qur'ani tukufu la mama kumnyonyesha mtoto ni kielelezo cha jinsi dini ya Uislamu ilivyotilia maanani afya na haki za mama na mtoto. Katika kulinda utulivu wa kiroho na kinafsi wa mama, Qur'ani tukufu pia inasisitiza kuwa, baba ana wajibu wa kudhamini gharama za kimaisha za mama kama chakula, mavazi na kadhalika katika kipindi cha kunyonyesha ili mzazi huyo aweze kunyonyesha mtoto wake kwa utulivu kamili. Sehemu moja ya aya ya 233 ya Suratul Baqara inasema: Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili kwa anayetaka kutimiza kunyonyesha. Na ni wajibu wa baba yake chakula cha kina mama na nguo zao kwa mujibu wa ada..."

Miongoni mwa faida muhimu za maziwa ya mama kwa mtoto katika mtazamo wa Qur'ani tukufu ni kuimarisha uhusiano wa kiroho kati ya mama na mtoto wake. Hii leo kunasisitizwa sana suala la mama anayejifungua kubakia katika chumba kimoja na mwanaye na kwamba wawili hao wasitenganishwe na kuwekwa katika vyumba viwili tofauti baada ya mama kujifungua, bali mtoto mchanga awekwe pembeni ya mama yake jambo ambalo kwa msemo wa wataalamu linajulikana kwa istilahi ya "rooming-in. Sura kamili ya suala la kuwa pamoja mwana na mama ni ile ya mama kumpakata mwanaye. Mama kuwa karibu sana na mwanaye kwa kumpakata, kumkumbatia, kumgusa, kumtazama na kumpa maziwa huwa na taathira kubwa katika kuongezeka kwa homoni za prolactin na oxytocin, na wakati bora zaidi wa kupatikana hali hiyo ni pindi mama anapokuwa anamnyonyesha mtoto mchanga.

Image Caption

Imepokewa kutoka kwa Imam Ja'far Swadiq (as) ambaye ni miongoni mwa Maimamu watoharifu katika kizazi cha Mtume wetu Muhammad (saw) kwamba amesema: "Upande wa kushoto wa mama ndio sehemu bora zaidi kwa ajili ya kumnyonyesha mtoto". Imethibiti katika utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Cornell huko New York nchini Marekani kwamba, kwa kuwa moyo wa mwanadamu unapatikana upande wake wa kushoto na uhusiano wa mtoto na mama unafungamana na mapigo ya moyo ya mama yake, basi upande wa kushoto wa mama ndio bora zaidi wakati wa kumyonyesha mtoto.

Katika upande mwingine aya za Qur'ani tukufu na hadithi zilizopokewa kutoka kwa Mtume (saw) na Aali zake zinasisitiza kuwa, hitilafu za baba na mama zisifanywe sababu ya kumnyima mtoto haki ya kunyonya na haki zake nyingine. Baba wanakatazwa kuwadhuru watoto wao kiroho na kimwili kwa kuwachukua vichanga hao kutoka kwa mama zao kutokana na hitilafu za kifamilia; vivyo hivyo kina mama hawapasi kuwanyima watoto waziwa na kutowanyonyesha kwa visingizio mbalimbali kutokana na hitilafu za aina hiyo.