Makumi wauawa katika shambulizi la magaidi wa ISWAP Nigeria
(last modified Thu, 27 Jul 2023 10:19:28 GMT )
Jul 27, 2023 10:19 UTC
  • Makumi wauawa katika shambulizi la magaidi wa ISWAP Nigeria

Makumi ya watu wameuawa nchini Nigeria katika shambulizi la kundi la kigaidi la ISIS au Daesh tawi la Afrika Magharibi (ISWAP).

Duru za kiusalama ziliripoti habari hiyo jana Jumatano na kueleza kuwa, watu wasiopungua 25 wameuawa katika hujuma ya magaidi wa ISWAP katika jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa nchi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, magaidi hao wamewaua wafugaji 18 katika kijiji kimoja kilichoko wilayani Kukawa, na wengine 7 katika kijiji jirani mpakani mwa Chad.

Habibu Ardo, mmoja wa wafugaji katika eneo hilo amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, wapiganaji hao wa ISWAP wamefanya mashambulizi hayo wakiwa juu ya pikipiki zipatazo 15 katika vijiji hivyo viwili wilayani Kukawa katika jimbo la Borno.

ISWAP ni tawi lililojitenga na kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo lilianzisha uasi nchini Nigeria mwaka 2009 na hatimaye kupanua hujuma na mashambulio yake ya kigaidi katika nchi jirani zinazopakana na Ziwa Chad, za Cameroon, Niger na Chad.

Wanachama wa kundi la kigaidi la ISWAP

Katika miezi ya karibuni, maelfu ya wanachama wa kundi la kigaidi la ISWAP pamoja na wenzao wa Boko Haram wamekuwa wakijisalimisha kwa maafisa usalama huko kaskazini mwa Nigeria.

Takwimu za Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (Ecowas) zinaonyesha kuwa, eneo la Afrika Magharibi limesajili mashambulizi ya kigaidi zaidi ya 1,800 katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu 2023.