Namna Daesh wanavyotumia raia kama ngao vitani nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10072-namna_daesh_wanavyotumia_raia_kama_ngao_vitani_nchini_libya
Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya amesema kuwa, kundi la kigaidi la Daesh linawatumia raia kama ngao katika vita vinavyoendeshwa na serikali kwa ajili ya kuukomboa mji wa bandari wa Sirte.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 27, 2016 10:40 UTC
  • Fayez Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya.
    Fayez Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya.

Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya amesema kuwa, kundi la kigaidi la Daesh linawatumia raia kama ngao katika vita vinavyoendeshwa na serikali kwa ajili ya kuukomboa mji wa bandari wa Sirte.

Fayez Sarraj alisema hayo jana Jumapili wakati alipohojiwa na shirika la habari la Ufaransa na alijibu swali kuhusiana na kuzorota opereseheni ya kuusafisha kikamilifu mji wa Sirte kwa kusema: Vikosi vya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya vimo ndani ya mji wa Sirte, lakini ni vigumu kumaliza vita hivyo kwani magaidi wa Daesh wanatumia raia kama ngao ya kivita; na askari wa serikali wanalazimika kuchukua tahadhari kubwa katika operesheni zao. Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya ameelezea matumaini yake kwamba vita vya kuukomboa kikamilifu mji wa Sirte vitamalizika karibuni hivi kwani kundi la kigaidi la Daesh limeshazingirwa katika eneo moja maalumu lisilo na raia. Vikosi vya serikali ya umoja wa kitaifa huko Libya vilianzisha operesheni kubwa mwezi Mei mwaka huu kwa ajili ya kuukomboa mji wa Sirte ambao kundi la kigaidi la Daesh lilikuwa limeubadilisha kuwa ngome yake katika fukwe za Libya kwa karibu mwaka mzima sasa. Duru za hospitali ya serikali iliyotengwa kwa ajili wa kuwahudumia majeruhi zimesema kuwa, hadi hivi sasa askari 166 wa serikali wameshauawa na wengine 500 kujeruhiwa. Hata hivyo serikali ya Libya inasema kuwa, mji wa Sirte umeshakombolewa, lililobakia ni mapigano ya hapa na pale kati ya vikosi vya serikali na magaidi wa Daesh ambao wameshafurushwa mjini humo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya serikai, raia waliobakia katika mji wa Sirte wanakadiriwa kufikia 30 elfu. Ikumbukwe kuwa, idadi wa wakazi wa mji huo kabla ya kutekwa na magaidi wa Daesh mwezi Juni 2015 walikuwa ni karibu watu laki moja na 20 elfu. Serikali ya Libya aidha inasema kuwa, imefanikiwa kuua mamia ya wanangambo wa Daesh katika operesheni hiyo. Wakati huo huo komandi ya kijeshi ya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya imesema kuwa, jeshi la nchi hiyo limefikia makubaliano ya kusimamisha vita na baadhi ya makundi ya wapinzani katika mji wa Darnah wa mashariki mwa Libya. Taarifa zinasema kuwa mji wa Darnah umehabiriwa vibaya katika mapigano, huku miundombinu mikuu kama vile daraja maarufu la magharibi mwa mji huo, sehemu fulani ya vinu vya kuzalisha umeme, viwanja vya michezo n.k yote imeharibiwa vitani. Katika upande mwingine, vikosi vya kijeshi vinavyoongozwa na Khalifa Haftar vimefanikiwa kukomboa eneo la Ajdabia baada ya vita vikali na wanamgambo wa Daesh. Kwa upande wake, televisheni ya al Mayadeen ya nchini Lebanon imewanukuu viongozi wa Libya wakisema kuwa, vikosi vya serikali vimefanikiwa pia kukomboa maeneo mengi katika mji wa Benghazi. Pamoja na hayo, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya amesema kuwa, njia pekee ya kuweza kumaliza makundi ya kigaidi nchini humo ni kuundwa jeshi moja lenye nguvu ambalo litakuwa na uwezo wa kusimamia makundi na vikosi vyote vya ulinzi vya nchi hiyo. Sarraj amesema, wanaamini kuwa, kupambana na kundi la Daesh kutawezekana iwapo tu kutakuwa na jeshi moja lenye nguvu ambalo litatiiwa na wananchi na vikosi vyote vya ulinzi. Hivi sasa kuna makumi ya makundi yenye silaha nchini Libya na hilo limetokea baada ya nchi za Magharibi kuitelekeza Libya baada ya kupinduliwa Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011. Bila ya shaka ni kwa kuungana makundi yote hayo chini ya mwavuli wa serikali moja ndipo Libya itakapoweza kuwa na usalama wa kweli, vinginevyo habari za mapigano zitaendelea kuripotiwa kila siku kutoka katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.