Wanachama wa BRICS wakubaliana kuhusu utaratibu wa kupanua kundi hilo
Dr. Naledi Pandor, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afrika Kusini, ametangaza kuwa nchi wanachama wa BRICS zimeafikiana kuhusu misingi muhimu ya kupanuliwa kundi hilo. Wanachama wa sasa wa BRICS ni Russia, China, Brazil, India na Afrika Kusini.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesema kuhusu utaratibu na upanuzi wa BRICS kwamba: "Tumefikia makubaliano juu ya upanuzi (wa kundi hili). Kuhusu hili, tuna hati ambayo tumeidhinisha. Hati hii inaweka miongozo, kanuni na taratibu za kuchunguza nchi zinazotaka kujiunga na BRICS."
Rais Xi Jinping wa China pia amekaribisha wazo la kupanua kundi hilo katika mkutano wa siku tatu wa BRICS na kuthibitisha kuwa nchi 20 tayari zimeomba uanachama na kuwa nyingine nyingi pia zinakaribishwa kujiunga na kundi hili kwa ajili ya maendeleo yao zenyewe.

Jumuiya ya BRICS ni nembo ya "ubunifu wa utawala na muundo mpya katika uwanja wa kimataifa" iliyoundwa na mataifa yanayoinukia katika kukabiliana na ulimwengu wa kambi moja ya utawala. Matakwa ya pamoja ya wanachama wa BRICS, ambao huzalisha robo ya utajiri wa dunia na kuchangia asilimia 42 ya watu wote duniani, ni nguvu kubwa zaidi ya kimataifa ya kisiasa na kiuchumi, hasa dhidi ya Marekani na Umoja wa Ulaya. Kiashiria muhimu zaidi cha BRICS ni nafasi yake ya kiuchumi, kifedha na vile vile upeo na ushawishi wa kikanda na kimatifa wa wanachama wake, jambo ambalo limeipelekea kujulikana kama kundi la "nguvu za kiuchumi zinazoibuka". Hivi sasa, mbali na wanachama wakuu 5, nchi 23 zimeomba rasmi kujiunga na kundi hilo ilihali nyingine 6 zimeonyesha nia ya kujiunga na kundi hilo kwa njia isiyo rasmi. Nchi hizo ni pamoja na Iran, Indonesia, Saudi Arabia, Kuwait, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Misri, Syria, Morocco, Belarus, Kazakhstan, Cuba, Bolivia, Nigeria, Argentina, Venezuela, Thailand, Vietnam, Algeria, Palestina, Ethiopia, Honduras na Mexico, nchi ambazo zinatajwa kama BRICS Plus.
Pendekezo la kuundwa BRICS Plus lilitolewa kwa mara ya kwanza na Rais Xi Jinping wa China katika mkutano wa kilele wa kundi hilo uliofanyika nchini humo mwaka uliopita, kama utaratibu wa kuzileta karibu nchi hizo kabla ya kupewa uanachama kamili kwenye kundi hilo. Iran inataka kuwa mwanachama wa BRICS, na ndio maana Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu akashiriki katika kikao cha viongozi wa kundi hilo mjini Johannesburg. Akifafanua kwamba, kuwa na uhusiano wa karibu na nchi zote huru ni katika vipaumbele vya sera za kigeni za Iran, Rais Raisi amesema: Kundi la BRICS limeweza kuzileta pamoja nchi huru zilizo na lengo la pamoja la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kupiga vita siasa za upande mmoja, na bila shaka ni moja ya asasi zenye nguvu zinazoinukia duniani, jumuiya ambayo ina marafiki wengi duniani.
Mnamo mwaka 2009, madola yanayoinukia kiuchumi duniani yalianzisha jumuiya ya kisiasa na kiuchumi bila ya uwepo wa nchi za Magharibi, ambayo inaitwa BRICS. Zikiwa kwenye kilele cha kundi la BRICS, China na Russia zinataka kukomesha udhibiti wa dola na uwezo wa kiuchumi wa nchi za Magharibi katika mahusiano ya kibiashara. Wanachama wa BRICS pia wameelezea mara kwa mara na kwa sauti kubwa matakwa yao ya nchi za kusini mwa dunia kupewa uwakilishi unaofaa katika taasisi za kimataifa kama vile Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Shirika la Fedha la Kimataifa IMF au Shirika la Biashara Duniani WTO.

Kuhusiana na hilo, viongozi wa BRICS siku ya Jumanne, ikiwa ni siku ya kwanza ya mkutano wao wa kumi na tano huko Johannesburg, mji mkuu wa kiuchumi wa Afrika Kusini, walisisitiza katika hotuba zao haja ya kupunguza utegemezi wa nchi wanachama kwa sarafu ya dola, kuboresha uhusiano wao wa kiuchumi na njia za kuongeza mvuto wa fedha na utoaji mikopo kwa kutumia fedha za ndani kupitia Benki Mpya ya Maendeleo ya kundi hilo. Nchi za BRICS zina sababu nyingi za kubuni sarafu mpya.
Changamoto za hivi karibuni za kifedha duniani na sera za hujuma za kigeni za Marekani zimezipelekea nchi za BRICS kuchunguza uwezekano huo. Licha ya kupunguza utegemezi wa kimatifa kwa sarafu za dola na euro katika miamala ya kiuchumi na kibiashara, pia zinataka kulinda maslahi yao ya kiuchumi. Utambulisho na malengo ya BRICS, yamezivutia sana nchi nyingine zinazoendelea na hivyo kuzishawishi kuomba uanachama katika kundi hilo, na bila shaka kuidhinisha utaratibu wa nchi mpya kupewa uanachama katika BRICS inachukuliwa kuwa hatua muhimu katika mchakato mzima wa kupokea wanachama wapya katika kundi hilo la kimataifa.