Sep 23, 2023 06:24 UTC
  • Madhara ya kuendelea vita baina ya majenerali wa kijeshi nchini Sudan

Licha ya kupita miezi mingi, lakini ndio kwanza vita baina ya majenerali wa kijeshi vinaendelea nchini Sudan na hali ya kisiasa na kiuchumi ya nchi hiyo inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku. Cha kusikitisha ni kuwa pamoja na hali kuwa mbaya kiasi hicho, lakini bado pande hasimu zinaendelea kufanya ukaidi wa kutokubali kusimamisha mapigano.

Jenerali Abdel Fattah al Burhan, Kamanda wa Jeshi la Sudan (SA) kwa mara nyingine amevishutumu Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kuwa vinafanya jinai za kivita na havitaki suluhu na ameitaka jamii ya kimataifa kulihesabu kundi hilo na waitifaki wake kuwa ni magaidi.

Amesema, taifa la Sudan limetumbukia kwenye vita haribufu na kwamba RSF na waitifaki wake ndio wanaobeba dhima yote. Amewataja waitifaki wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kuwa ni wanamgambo wa makabila tofauti pamoja na mikono ya nje ya Sudan, ya kieneo na kimataifa. Ameonya kuwa mikono ya kieneo na kimataifa inayovisaidia Vikosi vya Msaada wa Haraka ndiyo inayochochea moto wa vita na kuangamizwa Sudan.

Vita vya kuwania madaraka baina ya majenerali wa kijeshi vinaisababishia hasara kubwa Sudan

Vita vya kuwania madaraka baina ya majenerali wa kijeshi vilianza tarehe 15 Aprili mwaka huu huko Sudan. Vita hivyo vyenye uharibifu mkubwa na ambavyo vinaiangamiza Sudan katika kila upande, ni baina ya jeshi la nchi hiyo SA linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan, na Vikosi vya Msaada wa Haraka, RSF, vinavyoongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo maarufu kwa jina la Hemedti. Pande hizo mbili zinafanya uharibifu mkubwa kwa ajili ya kudhibiti maeneo muhimu ya Sudan ikiwemo Ikulu ya mjini Khartoum, Komandi Kuu ya Vikosi vya Ulinzi na viwanja vya ndege vya kijeshi na vya kiraia. Katika kipindi cha siku za hivi karibuni, mapigano nchini Sudan yamepamba moto hasa pambizoni mwa Makao ya Komandi Kuu ya Jeshi mjini Khartoum. 

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo kila upande unaulaumu upande mwingine hasimu kuwa ndio unaopenda vita na usiotaka amani. Siku chache zilizopita, Jenerali Hemedti alitoa taarifa akimlaumu Jenerali al Burhan na jeshi la Sudan kuwa wanafanya mashambulizi ya kipunguwani dhidi ya raia, maeneo ya serikali na Ikulu ya mjini Khartoum. Sehemu moja ya taarifa hiyo ilisema, Jeshi la Sudan linashambulia kwa makusudi taasisi za serikali na miundombinu likiwemo Jengo la Wizara ya Mahakama, Jengo la Idara ya Kodi, Jengo la Idara ya Viwango, Shirika la Mafuta liitwalo al Nabil na maeneo mbalimbali ya makazi ya raia mjini Khartoum. Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya RSF, Jeshi la Sudan limefanya mashambulizi mengi ya anga ya kiholela dhidi ya maeneo hayo.

Jenerali Abdel Fattah el Burhan katika mazungumzo na rais wa Misri, Jenerali Abdel Fattah el Sisi

 

Cha kutilia maanani hapa ni kuwa, vita baina ya majenerali hao wa kijeshi vimefungua mlango wa uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya Sudan kiasi kwamba, nchi nyingi hivi sasa zinatanuliana misuli kwa namna ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja, kupitia uungaji mkono wa pande zinazopigana nchini humo. Hivi karibuni, Jenerali al Burhan alizishutumu nchi za ukanda huo kuwa zinachochea vita huko Sudan lakini hakutaja jina la nchi yoyote. Yeye mwenyewe lakini amefanya safari katika nchi mbalimbali za kieneo na kimataifa kama vile Misri na Uturuki. Wakati huo huo Majed al Ansari, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar hivi karibuni alitangaza rasmi kuwa, Jenerali al Burhan atatembelea pia Doha mji mkuu wa Qatar katika ziara yake ya mzunguko. Hayo ni katika hali ambayo tovuti ya Foreign Policy (FA) imeandika kwamba, kutokana na Sudan kuwa lango muhimu la kuingilia barani Afrika, nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kama Saudi Arabia na Muungano wa Falme za Kiarabu zinaunga mkono pande hasimu huko Sudan ili kuonesha nguvu na ushawishi wao. Kwa mujibu wa tovuti hiyo, wakati Saudia inamuunga mkono Jenerali al Burhan, Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) unamuunga mkono Jenerali Hemedti wa RSF.

Kiujumla ni kwamba hivi sasa Sudan imo kwenye lindi la machafuko na uangamizaji wa nchi. Kila upande unapigania kupora utajiri wa nchi hiyo na kuwasahau wananchi. Sudan ni nchi muhimu hasa kutokana na kuwa karibu na Bahari Nyekundu, Mto Nile na kupakana na nchi nyingi, kaskazini, kusini, mashariki na magharibi. Nchi hiyo ina utajiri mkubwa pia wa madini na maliasili kiasi kwamba biashara ya dhahabu katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, ndiyo iliyoainisha mustakbali wa kisiasa wa nchi hiyo. Utajiri wake wa mafuta na kuweko huko mabomba makuu ya kusafirishia mafuta ya nchi jirani ya Sudan Kusini, ni jambo jingine linalozidisha umuhimu wa Sudan. Kwa kuzingatia yote hayo, ni vigumu kuwa na matumaini ya kumalizika haraka vita nchini Sudan.

Tags