UN yaongeza askari 2,500 wa kulinda amani nchini Mali
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeafiki kuongezwa askari 2,500 wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA ambapo kikosi hicho sasa kitakuwa na jumla ya askari jeshi 13,289 na askari polisi 1,920.
Nchi wanachama 15 wa baraza hilo jana Jumatano kwa kauli moja walipiga kura ya kuunga mkono rasimu ya azimio la Ufaransa la kutaka kutumwa askari zaidi katika nchi hiyo ya Kiafrika. Francois Delattre, balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa ambaye ndiye rais wa Baraza la Usalama la umoja huo mwezi huu amesema mbali na kuongezwa askari wa MINUSMA nchini Mali kwa shabaha ya kuwadhaminia usalama wananchi wa nchi hiyo, utekelezaji wa makubaliano ya amani ni katika vipaumbele vya Umoja wa Mataifa.
Itakumbukwa kuwa, Mei 29 msafara wa magari ya kikosi cha MINUSMA ulishambuliwa karibu na mji wa Sevare katikati mwa Mali na kusababisha vifo vya askari watano na mwingine mmoja kujeruhiwa vibaya, hujuma ambayo ililaaniwa vikali na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Askari wa kofia buluu wa Umoja wa Mataifa maarufu kwa jina la MINUSMA wako nchini Mali tangu mwaka 2013 kwa ajili ya kusaidia juhudi za kuleta utulivu katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Hata hivyo askari hao wamekuwa wakishambuliwa mara kwa mara na makundi yenye misimamo mikali katika maeneo hayo, kama vile kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Qaeda katika eneo la Maghareb AQIM.